Showing posts with label siasa. Show all posts
Showing posts with label siasa. Show all posts

Wednesday, August 27, 2014

JK:Nipo tayari kukutana na UKAWA



RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Jakaya Kikwete, amesema yeye hana tatizo kukutana na wajumbe wa Bunge Maalum la Katiba kutoka Umoja wa Katiba ya Wananchi (UKAWA).
 “Wanajua jinsi ya kukutana nami, ili tuweze kutafuta namna ya kumaliza tofauti hizi,”alisema wakati akizungumza na wanafunzi wa Chuo Kikuu Mzumbe Morogoro, viongozi na wakazi wa vijiji jirani na chuo.
Aidha alisema ana matumaini kuwa mchakato wa katiba unaoendelea utaweza kuwapatia Watanzania katiba mpya.
“Mimi naishi kwa matumaini. Naamini kuwa tutafika mwisho vizuri. Mchakato ni mgumu lakini barabara ndefu haikosi kona. Tukidhamiria kweli tutafika tuendako vizuri,” alisema.
Aliwambia mamia ya wanachuo, watumishi wengine wa chuo hicho: “Maoni yenu ndiyo maoni yangu. Ni jambo la kusikitisha kuwa tofauti hizi za viongozi wa siasa zinaleta mfarakano wa namna hii. Tokea mwanzo niliwaambia kuwa wakiruhusu kushindana na kuviziana katika mchakato huo watakwama.”
 “Aidha, niliwaambia kuwa Katiba inayotafutwa siyo katiba ya CCM, ama ya CHADEMA, ama ya NCCR, ama ya CUF. Niliwaambia kuwa hii ni katiba ya wananchi wa Tanzania. Ni vyema tukakubaliana kuwa yenye kutugawa tukayaacha kwa sasa na kukubali kwa yale ambayo hatuna tofauti,” alisema.
Mapema wanafunzi wa chuo hicho waliunga  mkono mchakato wa Bunge Maalumu la Katiba wakisema wanaridhishwa na hatua iliyofikiwa na mwendo mzima wa bunge hilo na kuwa mwafaka unawezekana kuhusu vipengele viliyobakia na kupatikana kwa theluthi mbili za kupitisha katiba mpya.
Katika risala hiyo iliyosomwa na Rais wa Chama cha Wanafunzi wa Chuo Kikuu cha Mzumbe, Boniface Maige Juma, wanafunzi hao walisema ni vyema mchakato huo ukaungwa mkono na kila Mtanzania ili kuuwezesha kuleta neema na matarajio yanayokusudiwa.

 “Tunaridhishwa na hatua iliyofikiwa na Bunge Maalum la Katiba. Tunaamini kuwa mwafaka unawezekana kwa vipengele vingine vya rasimu ya katiba. Aidha, tunaamini kuwa theluthi mbili za kupitisha katiba mpya zinawezekana kupatikana,” alisema.

Friday, January 10, 2014

UPDATES:TAARIFA YA JOHN MNYIKA KUJIZULU!




Jana mitandao ya kijamii ilijazwa taarifa kwamba jana jioni, John Mnyika (Mb) alimwandikia barua ya kujiuzulu Katibu  Mkuu wa CHADEMA.



Ofisa Habari Mwandamizi wa CHADEMA, Tumaini Makene (0752 691569) alijibu kwa kukanusha kuhusu taarifa hizo na kuongeza kuwa kwa muda uliotajwa, Mhe. Mnyika alikuwa katika shughuli za chama akitimiza majukumu yake.

Akasema taarifa hizo ni mradi wa kutengeneza uongo unaofadhiliwa na watu kwa sababu ya, “kuwasumbua wanachama na Watanzania, lakini pia kutaka kuonesha kuwa kundi la wasaliti na wanafiki ndani ya chama linaungwa mkono na watu makini ndani ya chama ambao kama wangekuwa upande wao, wangesaidia kundi hilo kuondoa taswira hasi linalopata mbele ya jamii. Wanatafuta uhalali walioupoteza kwa kufanya harakati za kusaliti mapambano.
Mioyoni mwao wanaumia kweli kweli kuonekana wanaungwa mkono na watu wasio wanachama wa CHADEMA, ambao wengine wanalazimika kwenda kuwanunua pale feri Posta na Kariakoo ili waje kuwashangilia Mahakamani na kukimbia barabarani.
Tunajua wanaumia kutumia mamilioni kukodi watu kuja kulia kwenye msiba wasioujua wala usiokuwa wa kwao, huku wakidai ujira hadharani.
aliandika Makene kwenye tovuti ya MwanaHalisiForum
Kubenea katika tovuti hiyo aliandika, “Nathibitisha ifuatavyo: Nimeongea na Mnyika muda huu, amenihakikishia kuwa habari hiyo siyo ya kweli. Hajajiuzulu na wala hana sababu ya kujiuzulu.  Anasema, hawezi kuungana na watu wanaokivuruga chama. Anaipenda Chadema na anaamini ndiyo chama bora kwa

Monday, January 6, 2014

Dk. Kitila amkana Zitto.....Adai alikuwa anaufahamu mkakati wa Usaliti aliokuwa akiufanya Zitto ndani ya Chama..!!

ALIYEKUWA mjumbe wa Kamati Kuu (CC) ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Dk. Kitila Mkumbo, amemuumbua Mbunge wa Kigoma Kaskazini, Kabwe Zitto, akisema kuwa aliufahamu mkakati wa usaliti uliokuwa ukifanyika ndani ya chama.
Dk. Kitila, Zitto na Samson Mwigamba, aliyekuwa Mwenyekiti wa CHADEMA Mkoa wa Arusha, walivuliwa uongozi na Kamati Kuu ya chama mwaka jana, wakituhumiwa kuandaa mkakati wa siri wa usaliti.

Viongozi hao walipewa tuhuma zao kwa maandishi na kutakiwa kujibu ndani ya siku 14, kisha Kamati Kuu ilikutana na kuwahoji, ambapo Dk. Kitila na Mwigamba wamevuliwa uanachama rasmi juzi, huku Zitto akikimbilia mahakamani kuweka pingamizi asijadiliwe uanachama wake.
Akitoa taarifa ya uamuzi wa Kamati Kuu iliyoketi kwa siku mbili jijini Dar es Salaam, Katibu Mkuu wa CHADEMA, Dk. Willibrod Slaa, aliwaambia waandishi wa habari jana kuwa Dk. Kitila alifika mbele ya kikao na kuhojiwa.
Itakumbukwa kuwa katika kikao cha Novemba 2013, Dk. Kitila na Zitto walikataa katakata kuhusika kwa Zitto katika maandalizi ya mkakati wa mabadiliko.

Aidha, Zitto alidai mbele ya Kamati Kuu kwamba alikuwa ameusikia mkakati huo kwa mara ya kwanza kwenye Kamati Kuu, na amerudia kauli hiyo mara nyingi na hadharani tangu avuliwe nafasi zake za uongozi,” alisema.
Kwa mujibu wa Dk. Slaa, wakati wa mahojiano na wajumbe wa Kamati Kuu, Dk. Kitila alikiri kwamba yeye na waandishi wenzake wa mkakati huo walimpa Zitto taarifa na kwamba alikuwa anaufahamu.
Ukweli huu pia umethibitishwa na mawasiliano ya barua pepe iliyotumwa na Zitto mwenyewe kwa mtu anayeitwa ‘CHADEMA Mpya 2014’ tarehe 27 Oktoba 2013, karibu mwezi mmoja kabla ya kikao cha Kamati Kuu ya Novemba iliyowavua madaraka,” alisema.
Aliongeza kuwa Dk. Kitila baada ya kuonyeshwa waraka wa chama juu ya mabadiliko ya katiba ya chama uliotumwa na aliyekuwa Naibu Katibu Mkuu wa chama wakati huo, Shaibu Akwilombe, Julai 2006, unaothibitisha kwamba mabadiliko ya katiba yaliondoa ukomo wa uongozi, alikataa akidai tayari wamepeleka malalamiko yao kwa Msajili wa Vyama.
Dk. Slaa alifafanua kuwa baada kuonyeshwa nyaraka mbalimbali za matumizi ya fedha zilizoidhinishwa na Kamati Kuu zikihusu manunuzi na michango ya Mzee Jaffer Sabodo na watu binafsi, Dk. Kitila ambaye wakati huo alikuwa mmoja wa wajumbe pamoja na Zitto, juzi hakuwa na lolote la kuiambia Kamati Kuu.
Alisema kuwa Dk. Kitila pekee ndiye alifika kwenye Kamati Kuu na kujitetea kwa mdomo. Kwamba katika utetezi wake wa maandishi, licha ya kukiri kushiriki katika maandalizi ya kile kinachoitwa Mkakati wa Mabadiliko 2013, juzi alikataa katakata kuhusika.
“Licha ya kukiri katika kikao cha Kamati Kuu ya Novemba 2013, kwamba walioshiriki kuandaa mkakati huo ni pamoja na mtu anayejulikana kama M2, mara hii alisema waraka husika ulikuwa siri.
Na haukuwahi kusambazwa wala kushirikisha wanachama au viongozi wa CHADEMA isipokuwa mimi binafsi na Mwigamba,” alisema.
Dk. Slaa alieleza kuwa wakati utetezi wake ukiwa hivyo, Novemba mwaka jana, Dk. Kitila alidai kutomfahamu kabisa M2, lakini mara hii aliiambia Kamati Kuu kwamba anamfahamu fika M2, lakini hayuko tayari kumtaja mbele ya kamati hadi atakapowasiliana naye.
Uamuzi
Dk. Slaa alisema baada ya kusikiliza utetezi huo na kumhoji muhusika kwa kirefu, Kamati Kuu imeridhia bila shaka kwamba mkakati wa mabadiliko 2013 haukuwa na lengo la kumwezesha Zitto kutwaa nafasi ya mwenyekiti wa chama taifa peke yake.
“Mkakati huo ulikuwa na malengo makubwa zaidi ya kukibomoa chama kwa kukichafua kwa wananchi na kuwachafua viongozi wake wa juu kwa kutumia tuhuma za uongo za ufisadi.
Kamati Kuu imeridhika kwa ushahidi wa nyaraka mbalimbali zilizoandaliwa na Zitto mwenyewe ama na mawakala wake kutumia vitambulisho bandia katika mitandao ya mawasiliano ya kijamii, kwamba mkakati wa kukibomoa chama umeandaliwa na kutekelezwa kwa muda mrefu,” alisema Dk. Slaa.
Alitaja hujuma nyingine iliyofanywa na Zitto moja kwa moja ni kuwaengua wagombea wa chama katika chaguzi mbalimbali kama ilivyotokea katika majimbo ya Mpanda Mashariki, Musoma Vijijini na Singida Mjini.
Kamati Kuu imeazimia kwamba kuanzia tarehe ya uamuzi wake, Dk. Kitila na Mwigamba wafukuzwe uanachama wa CHADEMA na vile vile Zitto amekishitaki chama kinyume na matakwa ya katiba yake na kanuni zake,” alisema.
Kwamba Mahakama Kuu imeamuru vikao vyote vya chama visijadili wala kuamua suala lolote linalohusu uanachama wa Zitto.
Hivyo, viongozi wa ngazi zote za chama, wanachama, mashabiki na wapenzi wa CHADEMA popote walipo ndani na nje ya nchi wasishiriki mikutano na shughuli za kisiasa zitakazofanywa na Zitto.

Mamluki CCM
Wakati Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam ikitarajiwa kutoa uamuzi wake leo wa ama uanachama wa Zitto ujadiliwe au usijadiliwe na chama chake hadi kesi ya msingi aliyoifungua isikilizwe, CCM imeandaa vijana mamluki wa kumsindikiza mahakamani.
Tanzania Daima limedokezwa kuwa mkakati huo unaratibiwa na Umoja wa Vijana wa chama hicho (UVCCM) kwa kuwatumia wanafunzi wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam.
Vinara wa mkakati huo ni vijana waliotimuliwa uanachama wa Baraza la Vijana la CHADEMA (BAVICHA) na kisha kujiunga na CCM.
Vijana hao, juzi walifanya kikao na wanachuo wafuasi wa CCM, wakiwahamasisha wafike kwa wingi mahakamani leo mapema kabla ya vijana wa CHADEMA kuwasili.
Mamluki hao waliambiwa wajifanye ni wanachama wa CHADEMA wanaomuunga mkono Zitto katika kesi yake dhidi ya chama chake.
Tayari mamluki hao walihakikishiwa fedha za nauli ya kwenda na kurudi pamoja na kujikimu kwa chakula na mambo mengine.
Tanzania Daima lilidokezwa kuwa fedha hizo zilikuwa zimeahidiwa kukabidhiwa jana baada ya vijana hao kujiorodhesha ili wajulikane idadi yao.
Kiongozi wa mkakati huo, aliwaeleza vijana hao kuwa watakapowasili mahakamani saa 12:00 asuhubi, watatakiwa kumuona yeye au makada wengine waliotimuliwa CHADEMA ambao watakuwa na kadi zaidi ya 100 za CHADEMA na watazigawa ili baada ya hukumu ya kesi hiyo wazichane na kuzitupa

Wednesday, December 25, 2013

 

Kuelekea kusheherekea sikukuu za Xmass na Mwaka Mpya Waziri wa Uchukuzi Dr Harrison Mwakembe amefanya ukaguzi wa tiketi kwa mabasi mbalimbali yaendayo mikoani ilikubaini mabasi yaliyo toza gharama kubwa za nauli katika kipindi hiki cha Xmass na mwaka mpya.
Baadhi ya mabasi yaliyokamatwa kwa makosa ya kuzidisha nauli aliamuru kurudishiwa nauli zilizozidi kwa abiria wao,zoezi hilo limefanyika alfajiri eneo la Visiga mkoa wa Pwani,kurudishiwa nauli kwa abiria kumeenda sambamba na faini ya shilingi laki mbili na nusu kwa kila basi lililofanya kosa hilo

Monday, December 23, 2013

Mkakati mpya wa kumng'oa Mizengo Pinda....wabunge 26 watia saini fomu maalumu ya kutaka Bunge limng'oe



Baadhi ya wabunge wameanzisha mkakati wa kumwondoa madarakani, Waziri Mkuu, Mizengo Pinda katika kile wanachodai kuwa hawaridhishwi na utendaji wake serikalini. 
 
Hiyo ni dalili kwamba kung’oka kwa mawaziri wanne kutokana na matokeo ya ripoti ya utekelezaji wa Operesheni Tokomeza Ujangili hakujamnusuru Pinda, kwani baadhi ya wabunge wanaendelea na msimamo kwamba naye ajiuzulu kwa kushindwa kuwasimamia wenzake.
 
Mawaziri waliong’oka baada ya Rais Jakaya Kikwete kutengua uteuzi wao kutokana na ripoti iliyowasilishwa na Kamati ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Mazingira ni Mawaziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, Shamsi Vuai Nahodha, wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Dk Emmanuel Nchimbi, Maendeleo ya Mifugo na Uvuvi, Dk Mathayo David Mathayo na Maliasili na Utalii, Balozi Khamis Kagasheki.
 
Hatua hiyo ya Rais Kikwete inatafsiriwa na wengi kama njia ya kuwapoza wabunge na kumwokoa Pinda ambaye ikiwa atang’oka itamaanisha kuundwa upya kwa Baraza la Mawaziri.
 
Habari ambazo zimelifikia gazeti hili jana zinasema wabunge 26 wametia saini fomu maalumu ya kutaka Bunge litumie mamlaka yake ya kikatiba kumng’oa Pinda kwa kumpigia kura ya kutokuwa na imani naye.
 
Kwa mujibu wa Ibara ya 53 A(1) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya 1977, Bunge linaweza kupitisha azimio la kura ya kutokuwa na imani na waziri mkuu, endapo itatolewa hoja kupendekeza hivyo.
 
Kwa mujibu wa Ibara hiyo, hoja ya kumpigia kura ya kutokuwa na imani na waziri mkuu inapaswa kuungwa mkono na wabunge wasiopungua asilimia 20 ya wabunge wote.
 
Mbunge wa Kasulu Mjini (NCCR-Mageuzi), Moses Machali alisema hili jana kuwa ukusanyaji saini za wabunge aliouanzisha Ijumaa jioni unakwenda vizuri.
 
“Kung’oka kwa mawaziri wale wanne inatosha kuthibitisha kuwa Pinda amepoteza uhalali wa kuwa Waziri Mkuu kutokana na kushindwa kuwasimamia walio chini yake,” alisema Machali.
 
“Rais tunaweza kumuacha, lakini Pinda ndiye mtendaji mkuu wa shughuli za Serikali. Kama wapo mawaziri wameboronga ni wazi na yeye anaingia moja kwa moja katika hilo kapu,” alisema na kuongeza:
 
“Kama kweli tunataka taifa lisonge mbele kutoka hapa tulipo ni lazima tumuondoe Pinda…….. amekuwa mpole mno, mzito kufanya uamuzi na analea matatizo.”
 
Hata hivyo, alisema wabunge waliosaini fomu hiyo, wote wanatoka kambi ya upinzani na kusema wabunge wengi wa CCM aliowafuata kuwaomba watie saini wanaogopa au wanasita kufanya hivyo.

“Nataka niwaambie wabunge wa CCM hebu tusimame katika masilahi ya umma… Serikali inapofanya vibaya wanaoumia ni wananchi wetu bila kujali ni mwanachama wa chama gani,” alisema.
 
Pinda tayari amesema wazi kwamba yuko tayari kujiuzulu wadhifa wake iwapo Rais Kikwete ataamua kumuondoa na kwamba hata Rais asipochukua hatua hiyo ni ruksa kwa wabunge kutumia mamlaka yao ya kikatiba ya kumuondoa kwa njia ya kura ya kutokuwa na imani naye.
 
Wabunge wengine
Mbunge wa Mwibara (CCM), Kangi Lugola ambaye alikuwa mwiba kwa Pinda bungeni alisema: “Haya ni mambo ya ajabu sana, tutaendelea kubadilisha glasi lakini mvinyo ni uleule”.
 
Alisema uwajibikaji wa Serikali unaanzia kwa Waziri Mkuu na kusema anamuomba Rais atafakari ombi lake la kumfuta kazi Pinda.
 
“Tufike mahali tuambiane ukweli bila kumung’unya maneno kama kweli tunataka kuisaidia nchi yetu na Serikali yetu ya Chama cha Mapinduzi ambayo inapendwa na kuaminiwa na Watanzania,” alisema Lugola.
 
Mbunge wa Iringa Mjini (Chadema), Mchungaji Peter Msigwa  alisema anavyomuona Pinda na kutafsiri utendaji wake, anadhani kuwa viatu vya uwaziri mkuu vinampwaya.
 
“Haiwezekani mara mbili ndani ya Bunge mawaziri wang’oke halafu wewe ubaki… wanapoboronga katika utendaji wao lazima pia umguse kiranja wao (Pinda) na hili bado tutalia nalo,” alisema Msigwa na kuongeza:
 
“Tulitarajia Waziri Mkuu awe wa kwanza kutafakari na kujipima kama kweli anastahili kubaki hasa baada ya madudu yale ambayo yameichafua Serikali mbele ya umma.”
 
Mbunge wa Kigoma Kaskazini (Chadema), Zitto Kabwe alisema wakati umefika kwa Waziri Mkuu, Pinda kukaa pembeni na kumwachia Rais Kikwete aunde safu nyingine.
 
“Pinda ni mtu wangu. Tunaheshimiana na sina chuki naye. Kwanza yeye ni mmoja wa watu ninaotuhumiwa kuwapa jimbo apite bila kupingwa na kuniletea matatizo kwenye chama changu.
 
“Hivyo sina chuki naye maana pia anatoka kanda yetu. Hata hivyo, hali ya sasa ya nchi inahitaji kupumua. Ampe nafasi Rais aunde Serikali upya.”

Alisema kuna tatizo kubwa la uongozi ndani ya nchi na kuwa mambo hayaendi licha ya juhudi mbalimbali pamoja na Bajeti ya Serikali kuongezeka kila kukicha.
 
“Huduma hazifiki kwa wananchi. Serikali ni kama haipo, nchi imevimba na inahitaji kupumua. Mwaka 1990 Rais Mwinyi (Ali Hassan Mwinyi,) alikumbwa na hali kama hii na Warioba alijiuzulu ili kumpa nafasi kuunda upya Serikali. Alimrudisha Warioba lakini mawaziri wengi waliondoka,” alisema Zitto.
 
Aprili mwaka jana katika mazingira yanayofanana na ya mkutano wa 14 wa Bunge uliomalizika Jumamosi, wabunge 74 wakiwamo wa CCM walitia saini fomu ya kutaka kumng’oa Pinda.
 
Hata hivyo, aliepuka zahama hiyo, baada ya Rais Kikwete kufanya mabadiliko katika baraza lake la mawaziri mwezi mmoja baadaye na kuwaondoa mawaziri sita na manaibu waziri wawili waliokuwa wakishinikizwa kuachia ngazi.
 
Mawaziri hao walikuwa William Ngeleja (Nishati na Madini), Mustafa Mkulo (Fedha), Ezekiel Maige (Maliasili na Utalii), Omar Nungu (Mawasiliano), Dk Cyril Chami (Viwanda na Biashara) Dk Hadji Mponda (Afya na Ustawi wa Jamii).

  Manaibu walikuwa Dk Athuman Mfutakamba (Uchukuzi) na Dk Lucy Nkya (Afya na Ustawi wa Jamii).

>>Mwananch

Friday, December 20, 2013

Nchimbi, Nahodha, Kagasheki na Mathayo Wavuliwa uwaziri Bungeni...

Rais Jakaya Kikwete leo ametengua uteuzi wa mawaziri wanne kufuatia shutuma nzito dhidi yao katika sakata la Operesheni Tokomeza Ujangili. 

Mawaziri waliopoteza ajira zao usiku huu ni pamoja na Khamis Kagasheki (Maliasili na Utalii), David Mathayo (Mifugo na Uvuvi), Emmanuel Nchimbi (Mambo ya Ndani) na Shamsi Vuai Nahodha (Ulinzi na JKT).
 
Akizungumza Bungeni Dodoma usiku huu, Waziri Mkuu Mizengo Pinda alikiri kulikuwa na matatizo makubwa katika usimamizi wa zoezi hilo.
 
Tulifanya operesheni kwa nia nzuri,” alisema Waziri Mkuu Pinda. “Tatizo ni namna operesheni hiyo ilivyotekelezwa.”
Katika mdahalo uliogusa nyoyo za wabunge na wachambuzi mbalimbali wa siasa leo, wabunge waliueleza umma jinsi ambavyo Operesheni hiyo ilitumika kutesa, kunyanyasa na kuua raia wasio na hatia na kuwadhulumu mali zao.

Sunday, December 15, 2013

DR SILAA AFUNGUKA."TUKISHIKA DOLA TUTARUHUSU UTENGENEZAJI WA GONGO"..SOMA ZAIDI HAPA




Katibu Mkuu wa Chadema, Dk.Willbroad Slaa
Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) kimetoa mpya baada ya kueleza kuwa kitakapofanikiwa kushika dola kitaruhu Shirika la Viwanda Vidogo Vidogo (SIDO) kutengeneza mitambo ya kutengenezea pombe aina ya gongo.

Katibu Mkuu wa Chadema, Dk.Willbroad Slaa, akizungumza na wananchi wa Jimbo la Kasulu Vijijini alisema kama gongo itatengenezwa kwa mitambo maalum itaondoa mianya ya rushwa kwa polisi ambao wamekuwa wakiwakamata wanaotengeneza kwa kificho na kuwafanya vitega uchumi vyao.


"Gongo sasa hivi ni haramu sababu inatengenezwa kwa kificho katika mazingira machafu, tukishika dola tutataka SIDO itengeneze mitambo ya kutengeneza gongo ili iwe katika hali ya usafi," alisema.


Mitambo hiyo itakayotengenezwa na SIDO itakapouzwa itaiingizia mapato serikali pia wauzaji wa gongo watafanya biashara hiyo kwa amani tofauti na sasa ambapo wanaifanya kwa kificho na wakikamatwa fedha zote wananufaika polisi.


Dk. Slaa alisema hata suala la kukamata watu wanaotengeneza silaha linapaswa kuangaliwa upya kwani wanaokamatwa wakifanya kazi hiyo wangekuwa wanashikiliwa kwa muda na baadaye wanapelekwa katika kiwanda cha serikali cha kutengenezea silaha ili watuhumiwa hao wapeleke ujuzi huo huko badala ya kuwafunga jela.


Dk. Slaa alisema matatizo yote yanatokana na wasomi kutofikiri namna ya kuisogea nchi mbele kimaendeleo.


"Nchi hii imelala, imechoka sababu waliopewa madaraka wamelala, wamejisahau hawatambui kuwa wamepewa nafasi hizo ili kuwatumikia wananchi," alisema.
 

CHANZO: NIPASHE

Friday, December 13, 2013

Rais Kikwete aongoza kikao cha Kamati Kuu ya CCM mjini Dodoma leo


Mwenyekiti wa CCM Rais Dkt.Jakaya Mrisho Kikwete akingoza kikao cha kamati kuu ya CCM kilichofanyika katika makao makuu ya CCM Mjini Dodoma mchana huu.Kushoto ni Rais wa Zanzibar Dkt.Ali Mohamed Shein na kulia ni katibu Mkuu wa CCM Bwana Abdulrahman Kinana

Thursday, December 12, 2013

"Zitto Anipe majina ya Vigogo walioficha Mabilioni Uswiss ili nimsaidie kuwataja...Sihitaji Kinga yeyote ile".....LEMA

Dodoma, Tanzania. Mbunge wa Arusha Mjini, Godbless Lema wakati akichangia  taarifa ya Kamati ya Sheria na Katiba muda mfupi uliopita  amemtaka Mbunge wa Kigoma Kaskazni Zitto Kabwe kumkabidhi AG majina ya watu wote walioficha fedha Uswis ambayo alisema anayo.

 
Lema ameliambia Bunge kama Zitto na serikali wameshindwa kuwataja watu hao, wampe Lema majina hayo ili awataje.

Amefafanua kwamba hatahitaji kinga yeyote kuwataja wezi hao walioficha fedha Uswis ndani ya Bunge au nje ya Bunge

Saturday, December 7, 2013

WAZIRI MKUU MIZENGO PINDA ADAIWA KUWA NI MZIGO TU KWENYE SERIKALI YA KIKWETE..RAIS AOMBWA AMFUKUZE



SAKATA la mawaziri kuandamwa kwa kutowajibika limezidi kushika kasi ambapo safari hii, Rais Jakaya Kikwete ametakiwa kumfukuza kazi Waziri Mkuu, Mizengo Pinda kwa madai ya kuwa mchawi wa maendeleo ya nchi na mzigo namba moja. 


Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa, Hawa Ghasia naye anadaiwa kuwa mzigo mwingine kwa taifa kutokana na kubariki ufisadi katika wizara yake.
 
Kauli hiyo ilitolewa jana na Mbunge wa Mwibara, Kangi Lugola (CCM) alipokuwa akichangia katika hoja mbalimbali kuhusu kamati tatu za Bunge zilizowasilishwa bungeni juzi.
 
Kamati zilizowasilisha hoja zao ni ile ya Hesabu za Serikali za Mitaa, Kamati ya Bajeti na Kamati ya Hesabu za Serikali.
 
Lugola alisema kama Rais Kikwete asipowafukuza kazi Pinda na Ghasia, CCM itakuwa shakani kurejea madarakani katika uchaguzi mkuu mwaka 2015.
 
“Mimi nawashangaa wabunge wenzangu mnaosimama hapa na kutumia nguvu zenu nyingi kuishauri serikali… hii serikali inayoongozwa na chama changu haishauriki, kwa kipindi kirefu ina watu wasiojua majukumu yao.
 
“Ni ngumu kuishauri serikali kutokana na kuwa na mawaziri wasiojua majukumu yao, kwa kutojua wanachokifanya wameamua kutohudhuria vikao muhimu vya kujadili taarifa za kamati,” alisema.
Lugola alisema katika kikao cha jana, mawaziri sita na manaibu wawili ndio waliohudhuria, hivyo waliobaki kukosa fursa ya kusikiliza michango mbalimbali inayotolewa na wabunge.
 
“Mimi ni mbunge wa CCM, na pengine haya ninayotaka kuyasema yanaweza yasiwapendeze wabunge wenzangu wa CCM, lakini ndivyo nilivyo, ndivyo Mungu alivyoniumba, naomba wanisamehe. Nchi nyingine katika Bunge Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) anapowasilisha taarifa, ndiyo wakati nchi nzima masikio ya watu yanakuwa bungeni, lakini kwetu ni tofauti,” alisema.
 
Wakati Lugola akichangia bungeni, walikuwepo mawaziri wanne tu na manaibu wawili, huku nafasi za mawaziri zikiwa wazi.
 
Waliokuwepo bungeni ni Waziri wa Maji, Profesa Jumanne Maghembe, Hawa Ghasia, Sofia Simba, Shamsi Vuai Nahodha, Mhandisi Charles Kitwanga na Janet Mbene.
 
“Lakini cha kushangaza kuanzia jana Waziri Mkuu ameenda kuhudhuria mahafali wakati jambo muhimu kama hili linazungumzwa bungeni. Hata hivyo pamoja na kuwa mheshimiwa spika jana (Juzi ) uliwatetea mawaziri kuwa walikuomba ruhusa, lakini mimi hainiingii akilini kuwa waliomba ruhusa mawaziri wote na kubaki mawaziri wanne na manaibu wawili,” alisema Lugola.
 
Alibainisha kuwa kwa busara za kawaida spika asingekubali kuwaruhusu mawaziri hao wakati kuna jambo la muhimu  linajadiliwa kwa mustakabali wa taifa na watu wake.
 
Lugola alisema TAMISEMI ina mtandao mkubwa wa utumiaji wa fedha ambao hauwezi kuwatenganisha Waziri Mkuu na Waziri Ghasia ambapo asilimia 70 ya fedha za bajeti hupelekwa huko.
 
Alisema kuwa licha ya wizara hiyo kutengewa fedha nyingi, bado serikali imekuwa ikisuasua kushughulikia masuala mbalimbali ya wananchi wa kipato cha chini.
 
Lugola aliwataka wabunge wasiendelee kuwasaliti Watanzania kwa kubariki ufisadi unaofanywa na viongozi wa TAMISEMI inayoongozwa na Waziri Mkuu, Pinda.
 
Alibainisha kuwa kwa sasa serikali haishauriki, na jambo hilo linaonekana wazi kwakuwa imeendelea kulipa mishahara hewa kwa waliofariki, huku Watanzania wakiteseka kwa umaskini.
 
Lugola aliongeza kuwa serikali imekuwa ikibariki ununuzi usiokuwa na nyaraka jambo ambalo ni wizi, lakini unalindwa na viongozi.
 
“Mchawi wetu katika maendeleo serikalini, tatizo kubwa ni Waziri Mkuu amekuwa mpole mno, hawajibiki…, matatizo yanatokea ndani ya nchi yupo wapi? Wananchi Mwibara umaskini unakithiri, fedha zinaliwa ambazo zingewapa madawati, watu wangepata madawati na maji, wangevua kwa uvuvi wa kisasa, Waziri Mkuu, jamani nakulilia huko wapi uwajibikaji wako ndani ya serikali?” alisema.
 
Naye Mbunge wa Musoma Mjini, Vicent Nyerere (CHADEMA), alisema serikali imeshindwa kufanya kazi, hivyo ni vema Watanzania wakafanya uamuzi wa kuiondoa madarakani kwa kutumia sanduku la kura.
 
Alisema kinachoonekana kwa Serikali ya CCM ni kubariki ufisadi kutokana na viongozi waliopo madarakani kushindwa kuwawajibisha wanaobainika kufanya ufisadi kwa sababu ya kulindana.
 
Nyerere alisema aliyekuwa Waziri Mkuu, Edward Moringe Sokoine, alikuwa na uwezo wa kuwawajibisha waliobainika kufanya ubadhirifu wa mali za umma.
 
“Hapa serikali mnaweza kujipima kuwa hata nyinyi wenyewe mmeishajikatia tamaa kutokana na kukosa huduma za kiafya na ndiyo maana hata alipotokea babu wa Loliondo viongozi wote mlikimbilia huko kwenda kupata kikombe,” alisema Nyerere.
 
Katika mjadala huo ambao umeibua hisia kali kwa wabunge, ambao kwa asilimia kubwa wamekuwa wakilalama kuwa TAMISEMI kuna ufisadi mkubwa ambao unafanyika huku serikali ikiwa imenyamaza kimya.
 
Katika mjadala huo wabunge walikuwa wakihoji sababu za watendaji wanaotuhumiwa kufanya ubadhirifu kuhamishwa vituo vyao vya kazi badala ya kufikishwa kwenye vyombo vya sheria.
 
Mara kwa mara wabunge na viongozi wa CCM wamekuwa wakiwalalamikia mawaziri kwa kushindwa kuwajibika, hivyo kuisababisha serikali kuchukiwa na wananchi.
 
Wiki mbili zilizopita Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM, Nape Nnauye alikaririwa akiwataja mawaziri wanne ambao wanatakiwa kutoa majibu ya uwajibikaji wao kwenye Kikao cha Kamati Kuu (CC) ya chama hicho kinachotarajia kufanyika wakati wowote kuanzia sasa.
 
Nape aliwataja mawaziri hao kuwa ni Waziri wa Kilimo Chakula na Ushirika, Christopher Chiza, naibu wake Adam Malima, Waziri wa Uvuvi na Mifugo, David Mathayo na Waziri wa Maji, Jumanne Maghembe

Sunday, December 1, 2013

Baada ya Kutimuliwa CHADEMA,Chuo Kikuu UDSM nao wamtimua Dk. Kitila kwa kukiuka taratibu za Kisheria



Taarifa zinasema kuwa uongozi wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam umemvua kwa muda Mhadhiwa Mwandamizi wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Dk Kitila Mkumbo madaraka ya kuongoza Kitivo cha Elimu cha Chuo Kikuu Kishiriki cha Elimu cha Dar es Salaam (DUCE).

Hatua hiyo inatajwa kuchukuliwa baada ya uongozi wa UDSM kupata taarifa kwenye vyombo vya habari kuwa Dk Kitila Mkumbo alikuwa kiongozi wa chama cha siasa, CHADEMA wakati angali ni mtumishi wa umma, jambo ambalo Uongozi wa chuo hicho umekariri kuwa ni kinyume cha sheria ya nchi na Serikali kwa mfanyakazi wa umma kushika wadhifa katika chama cha siasa.

Kutokana na uamuzi wa chuo hicho, Dk Kitila aliandikiwa na kukabidhiwa barua ya kusimamishwa kwake wadhifa huo.

Dk Kitila bado ataendelea kuwa Mhadhiri Mwandamizi kwenye kitivo hicho

Saturday, November 30, 2013

Rais Kikwete awasili jijini Kampala kuhudhuria mkutano wa EAC....Maada kuu watakazoongelea ni pamoja na Sarafu moja ya jumuiya ya Afrika Mashariki

Rais Dkt.Jakaya Mrisho Kikwete akisalimiana na wakuu wa vyombo vya ulinzi na Usalama wa Uganda muda mfupi baada ya kuwasili katika uwanja wa ndege wa Entebbe nchini Uganda kuhudhuria mkutano wa wakuu wa nchi za jumuiya ya Afrika Mashariki.
*****************

Wakuu wa nchi zinazounda jumuiya ya Africa Mashariki wanakutana leo tarehe 30 Novemba huko Kampala, Uganda.

 Wakuu hao ni pamoja na Rais Jakaya Kikwete wa Tanzania, Yoweri Mseveni wa Uganda, Paul Kagame wa Rwanda, Pierre Nkuruzinza wa Burundi na Uhuru Kenyatta wa Kenya.
 
 Masuala watakayozungumzia leo ni pamoja na soko la pamoja, umoja wa forodha, shirikisho la kisiasa na umoja wa sarafu ambapo leo watatia saini mkataba wa kuwa na sarafu moja

Sunday, November 24, 2013

JANUARY MAKAMBA APEWA MAKAVU LIVE NA LADY JAY DEE SOMA ALICHOMWAMBIA....

Lady Jaydee aka Anaconda amemshukia January Makamba live mara baada ya mheshimwa huyo kuandika post inayo husu kupromte wamamuziki  na wasanii  wa Tanzania kupitia twitter yake.  Hebu cheki mambo yalivyo kuwa.

HII NDIYO TAARIFA YA ZITTO KABWE LEO KWA VYOMBO VYA HABARI. MARA BAADA YA KUPOKONYWA MADARAKA YOTE MAKUBWA NDANI YA CHADEMA!



 1. Utangulizi Katika kikao chake cha siku mbili kilichofanyika tarehe 20 - 22 Novemba 2013, Kamati Kuu ya CHADEMA, pamoja na mambo mengine, iliazimia kunivua nafasi zangu zote za uongozi ndani ya chama. 



Kwa mujibu wa taarifa ya chama iliyotolewa katika mkutano na waandishi wa habari siku ya Ijumaa tarehe 22 Novemba 2013, ilielezwa kwamba sababu za kuvuliwa uongozi mimi na Dk Kitila Mkumbo ni uhaini na hujuma kwa chama kutokana na waraka unaojulikana kama mkakati wa uchaguzi 2013.
 


 Ukweli ni kwamba waraka uliotajwa si sababu ya mimi kuvuliwa nafasi zangu za uongozi kama ilivyojadiliwa katika Kikao cha Kamati Kuu . Sababu za kufukuzwa kwangu kama zilizojadiliwa katika kikao cha Kamati Kuu ni tuhuma lukuki ambazo si mara yangu ya kwanza kuzisikia zikijadiliwa ndani na nje ya vikao vya chama. 



Hitimisho la tuhuma hizi ni kwamba mimi nimekuwa nikikisaliti chama kwa kutumika na CCM na Usalama wa Taifa. Nitazianisha tuhuma hizi na kuzijibu kama ambavyo nimekuwa nikizijibu katika vikao mbalimbali vyama.
  Ninatambua kwamba chama changu kinapita katika wakati mgumu sana sasa hivi. Nataka nitamke mapema sana kwamba mimi Zitto Zuberi Kabwe sitokuwa chanzo cha CHADEMA kuvunjika. 
Hiki ndicho chama kilichonilea na kunifikisha hivi nilivyo. Ningependa chama hiki mtoto wangu atakapokuwa mtu mzima na atakapoamua kujiunga na siasa aingie CHADEMA. 
Bado nina imani kubwa na chama changu na ninaamini ndicho kinachostahili kuendesha nchi jana, leo na kesho.
  2. Kuhusu tuhuma mbalimbali zinazo elekezwa kwangu Zipo tuhuma nyingi ambazo zimekuwa zikirudiwarudiwa katika vikao vya chama na nje ya vikao na baadhi ya viongozi wenzangu.
 Tuhuma hizi zinalenga kuonyesha kwamba mimi ni mbinafsi na kwamba ninapokea rushwa ili kukihujumu chama changu. 
Nitazianisha tuhuma kwa kifupi na kuzijibu kama ambavyo nimekuwa nikizijibu katika vikao mbalimbali vya chama.
  i) Tuhuma kwamba sikushiriki kumpigia kampeni mgombea wetu wa urais katika uchaguzi wa mwaka 2010. Ningependa kueleza yafuatayo kuhusu jambo hili: 

  • Mimi nilikuwa mgombea wa ubunge katika Jimbo la Kaskazini huko Kigoma.
  • Pamoja na kuwa mgombea wa ubunge, nilifanya kampeni katika majimbo mengine 16 katika mikoa mbalimbali, ikiwemo Dar es Salaam, Mtwara, Pwani, Shinyanga, Mara na Rukwa. Hakuna kiongozi yeyote wa juu aliyefanya kampeni katika majimbo mengi kama mimi, ukiacha mgombea urais.
  • Kote nilipopita nilimpigia kampeni wagombea wetu wa udiwani, ubunge na Rais.
  • Katika Mkoa wa Kigoma nilizunguka na mgombea urais katika kata zote za Kigoma Kaskazini na majimbo yote manane ya Mkoa wa Kigoma.


 ii) Tuhuma kwamba katika Mkoa wa Kigoma nilishindwa kuwapigia kampeni wagombea wetu kiasi kwamba peke yangu ndiye niliyeshinda katika uchaguzi huo. Ukweli ni kwamba niliwapigia sana kampeni wagombea wetu, na hivyo ndivyo wapiga kura wa Kigoma walivyoamua.
  iii) Tuhuma kwamba nilishiriki kuwashawishi wagombea wetu katika baadhi ya majimbo kujitoa katika uchaguzi wa mwaka 2010 ili kuwapisha wagombea wa CCM wapite bila kupingwa kwa njia ya rushwa. Majimbo yanayotajwa ni pamoja na Sumbawanga, Musoma Vijijini na Singida Mjini.
 Kama nilivyokwisha kueleza katika vikao mbalimbali vya chama jambo hili si la kweli na hakuna popote ambapo watoa tuhuma hizi wamewahi kutoa ushahidi kwamba nilifanya jambo hili. 
Nipo tayari kwa uchunguzi ndani ya chama na watoa tuhuma waje na ushahidi bayana wa jambo hili. Si afya kwa chama kuendelea kurudiarudia tuhuma hizi kila mara tangu mwaka 2010 bila uchunguzi wowote kufanyika na jambo hili lifikie mwisho.
  iv) Tuhuma kwamba nimekuwa sishiriki katika operesheni mbalimbali za chama: Ukweli ni kwamba nimeshiriki sana katika operesheni mbalimbali za chama ndani na nje ya nchi. Kwa mfano, mwaka 2011 tulikuwa na operesheni kubwa katika mikoa ya Kanda ya Nyanda za Juu Kusini na nilikwenda katika mikoa yote tuliyotembelea.
 Mwaka 2012 baada ya hoja ya mkonge bungeni nilifanya ziara Mkoa wa Tanga. Mwaka 2012 kulikuwa na operesheni kubwa moja katika mikoa ya kusini ya Mtwara na Lindi. Operesheni hii sikushiriki kwa sababu nilikuwa nchini Marekani kufungua matawi kwa mwaliko wa Watanzania wanaoishi huko.
  v) Tuhuma kwamba nimekidhalilisha chama kwa tamko la PAC kwamba Hesabu za Vyama hazijakaguliwa na Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG): Katika jambo hili ninatuhumiwa kwamba mimi kama Naibu Katibu nilipaswa kuwasiliana kwanza na viongozi wa chama 'kuwatonya' ili wajiandae. 

Kwamba kutokuwatonya kumekidhalilisha chama na kukiweka kundi moja na CCM na nastahili kuadhibiwa vikali kwa kuwa katika taarifa yangu nilikuwa na nia mbaya na chama chetu. Maelezo yangu niliyoyatoa na ambayo ningependa kuyakariri hapa kuhusu jambo hili ni kama ifuatavyo: 

  • Utawala bora hautaki mimi kutumia nafasi yangu ya uenyekiti wa PAC kulinda chama changu na kuonea vyama vingine. Kufanya hivyo ni kuendeleza tabia zile zile ambazo tunazipinga na ambazo tunapigania kuzibadilisha
  • Napenda kusisitiza kwamba hakuna chama ambacho kimewahi kukaguliwa na Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Serikali (CAG). Natambua kwamba mahesabu ya chama changu yamekuwa yakikaguliwa na wakaguzi wa nje kwa utaratibu tuliojiwekea. Lakini matakwa ya kisheria ni kwamba mahesabu ya vyama vya siasa hayajakaguliwa na CAG, na hili ni kosa la kisheria, bila kujali kosa hili ni la nani.


 vi) Tuhuma kwamba mimi ni mnafiki katika kukataa kwangu kuchukua Posho za Vikao Mtakumbuka kwamba mimi nilikataa kuchukua posho tangu mwaka 2011 kama ishara ya kuonyesha kwa vitendo msimamo wa chama chetu wa kupinga posho za kukaa na matumizi mengine yasiyofaa katika fedha za umma kama ilivyoanishwa kwenye Ilani yetu ya mwaka 2010-2015. Mtakumbuka kwamba hivi karibuni Mheshimiwa Lema amenishutumu kwamba kukataa kwangu kuchukua posho ni unafiki kwa sababu ninapokea posho kubwa zaidi katika mashirika ya umma ambapo mimi ni mwenyekiti wa kamati husika. Ninapenda kueleza yafuatayo kuhusu jambo hili: 

  • Sipokei posho yeyote ya vikao (sitting allowance) ndani na nje ya Bunge tangu mwaka 2011. Hii ni pamoja na vikao vyote katika Kamati za Bunge ninavyohudhuria. Mtu yeyote mwenye ushahidi vinginevyo auweke hadharani.
  • Swala la kukataa posho (sitting allowance) ni swala la kiilani katika chama chetu, na kwangu ni swala la kimisingi zaidi. Katika Wilaya yangu vifo vya kina mama wajawazito ni 1900 kati ya wanawake 100,000 wenye ujauzito. Vifo hivi vinatokana na ukosefu wa huduma kwa sababu ya bajeti finyu. Ndiyo maana nilifurahi sana kwa chama chetu kuliweka swala la kupunguza matumizi ya Serikali katika Ilani, na kuondoa posho za wabunge, ambao tayari wanapokea mishahara mikubwa, kungesaidia sana kupatikana fedha ambazo zingeokoa vifo vingi vya kina mama.
  • Jambo hili si suala la ugomvi baina yangu na Mheshimiwa Lema. Ni suala la msingi katika chama chetu.


 3Usambazaji wa Ripoti ya Siri kuhusu Zitto Kabwe Hivi karibuni kulisambazwa waraka unaoitwa ripoti ya siri kuhusu mimi ukibeba lundo la tuhuma kwamba nimehongwa fedha nyingi ili kukihujumu chama changu. Waraka huu ulidaiwa kuwa umechomolewa kutoka makao makuu ya CHADEMA. 
Jambo hili pia lilijadiliwa katika kikao cha juzi kwa kifupi, na majibu ya viongozi wa chama ilikuwa ni kwamba waraka huu haukuandaliwa wala kusambazwa na makao makuu. Katika mchango wangu nililalamikia mambo matatu yafuatayo: 

  1. Kwamba baadhi ya waliokuwa wanasambaza waraka ule walikuwa ni viongozi wa chama chetu. Bahati mbaya hadi leo hakuna hata mmoja ambaye amekwishachukuliwa hatua za kinidhamu. Ninaamini kwamba kuna siku watu hao watachukuliwa hatua kwa mujibu wa taratibu za chama chetu.
  2. Kwa kuwa chama kimekana rasmi kuhusika na waraka huu, nitaendelea na taratibu za kisheria ili kuhakikisha kwamba wote waliohusika kutengeneza hekaya ile wanachukuliwa hatua stahiki za kisheria.


 4. Hitimisho Ninatambua kwamba kuna watu walitegemea leo ningejibu mapigo na ningewazodoa watu kwa majina kama ilivyo kawaida katika siasa za Tanzania.
 Natambua pia kwamba, kama ilivyo kawaida wakati wa migogoro katika vyama vya siasa hapa Tanzania, kuna watu walitegemea leo ningetangaza 'maamuzi magumu'.
 Natambua kwamba wapo ambao wangependa kupata nafasi ya kuendelea kutumia suala hili katika harakati zao za kudhoofisha mapambano ya demokrasia na uthabiti wa siasa za ushindani nchini mwetu. 
Napenda wanachama wa CHADEMA na wapenda demokrasia na siasa safi wote nchini watambue kwamba mimi bado ni mwanachama mwaminifu wa chama hiki na nitakuwa wa mwisho kutoka kwenye chama hiki kwa hiari yangu. Nitafuata taratibu zote ndani ya chama katika kuhitimisha jambo hili.
  Naomba wanachama waelewe kwamba mimi kama binadamu ninaumia ninapopigwa. Tuhuma ninazorushiwa ni kubwa na zinanikwaza. Tuache siasa za uzushi ili tujenge chama chetu na nchi yetu, ili hatimaye tuwakomboe Watanzania wenye matarajio na imani kubwa kwa chama chetu.
  Kama mwanasiasa kijana niliyekaa katika siasa kwa muda sasa yapo mengi mazuri nimeyafanya. Lakini kuna maeneo nilipojikwaa na yapo makosa niliyofanya kisiasa katika maisha yangu ya siasa.
  
 Kinachoendelea ndani ya chama chetu ni mapambano ya kukuza demokrasia. Ni mapambano baina ya wapenda demokrasia dhidi ya wahafidhina, waumini wa uwajibikaji dhidi ya wabadhirifu na wapenda siasa safi dhidi ya watukuzao siasa majitaka.
  Hii ni changamoto kubwa ndani ya chama chetu inayohitaji uongozi shupavu kuikabili. Nitasimama daima upande wa demokrasia. 
Kama alivyopata kunena mmoja ya wanasiasa maarufu, 'kiwango cha juu kabisa cha uzalendo katika nchi ni kukubali kutofautiana kimawazo', na ninatamani huu ndio uwe utamaduni wa chama chetu.
  Kabwe Zuberi Zitto, Mb Dar es Salaam. 24 Novemba, 2013