ALIYEKUWA mjumbe wa Kamati Kuu (CC) ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Dk. Kitila Mkumbo, amemuumbua Mbunge wa Kigoma Kaskazini, Kabwe Zitto, akisema kuwa aliufahamu mkakati wa usaliti uliokuwa ukifanyika ndani ya chama.
Dk. Kitila, Zitto na Samson Mwigamba, aliyekuwa Mwenyekiti wa CHADEMA Mkoa wa Arusha, walivuliwa uongozi na Kamati Kuu ya chama mwaka jana, wakituhumiwa kuandaa mkakati wa siri wa usaliti.
Viongozi hao walipewa tuhuma zao kwa maandishi na kutakiwa kujibu ndani ya siku 14, kisha Kamati Kuu ilikutana na kuwahoji, ambapo Dk. Kitila na Mwigamba wamevuliwa uanachama rasmi juzi, huku Zitto akikimbilia mahakamani kuweka pingamizi asijadiliwe uanachama wake.
Akitoa taarifa ya uamuzi wa Kamati Kuu iliyoketi kwa siku mbili jijini Dar es Salaam, Katibu Mkuu wa CHADEMA, Dk. Willibrod Slaa, aliwaambia waandishi wa habari jana kuwa Dk. Kitila alifika mbele ya kikao na kuhojiwa.
“Itakumbukwa kuwa katika kikao cha Novemba 2013, Dk. Kitila na Zitto walikataa katakata kuhusika kwa Zitto katika maandalizi ya mkakati wa mabadiliko.
“Aidha, Zitto alidai mbele ya Kamati Kuu kwamba alikuwa ameusikia mkakati huo kwa mara ya kwanza kwenye Kamati Kuu, na amerudia kauli hiyo mara nyingi na hadharani tangu avuliwe nafasi zake za uongozi,” alisema.
Kwa mujibu wa Dk. Slaa, wakati wa mahojiano na wajumbe wa Kamati Kuu, Dk. Kitila alikiri kwamba yeye na waandishi wenzake wa mkakati huo walimpa Zitto taarifa na kwamba alikuwa anaufahamu.
“Ukweli huu pia umethibitishwa na mawasiliano ya barua pepe iliyotumwa na Zitto mwenyewe kwa mtu anayeitwa ‘CHADEMA Mpya 2014’ tarehe 27 Oktoba 2013, karibu mwezi mmoja kabla ya kikao cha Kamati Kuu ya Novemba iliyowavua madaraka,” alisema.
Aliongeza kuwa Dk. Kitila baada ya kuonyeshwa waraka wa chama juu ya mabadiliko ya katiba ya chama uliotumwa na aliyekuwa Naibu Katibu Mkuu wa chama wakati huo, Shaibu Akwilombe, Julai 2006, unaothibitisha kwamba mabadiliko ya katiba yaliondoa ukomo wa uongozi, alikataa akidai tayari wamepeleka malalamiko yao kwa Msajili wa Vyama.
Dk. Slaa alifafanua kuwa baada kuonyeshwa nyaraka mbalimbali za matumizi ya fedha zilizoidhinishwa na Kamati Kuu zikihusu manunuzi na michango ya Mzee Jaffer Sabodo na watu binafsi, Dk. Kitila ambaye wakati huo alikuwa mmoja wa wajumbe pamoja na Zitto, juzi hakuwa na lolote la kuiambia Kamati Kuu.
Alisema kuwa Dk. Kitila pekee ndiye alifika kwenye Kamati Kuu na kujitetea kwa mdomo. Kwamba katika utetezi wake wa maandishi, licha ya kukiri kushiriki katika maandalizi ya kile kinachoitwa Mkakati wa Mabadiliko 2013, juzi alikataa katakata kuhusika.
“Licha ya kukiri katika kikao cha Kamati Kuu ya Novemba 2013, kwamba walioshiriki kuandaa mkakati huo ni pamoja na mtu anayejulikana kama M2, mara hii alisema waraka husika ulikuwa siri.
“Na haukuwahi kusambazwa wala kushirikisha wanachama au viongozi wa CHADEMA isipokuwa mimi binafsi na Mwigamba,” alisema.
Dk. Slaa alieleza kuwa wakati utetezi wake ukiwa hivyo, Novemba mwaka jana, Dk. Kitila alidai kutomfahamu kabisa M2, lakini mara hii aliiambia Kamati Kuu kwamba anamfahamu fika M2, lakini hayuko tayari kumtaja mbele ya kamati hadi atakapowasiliana naye.
Uamuzi
Dk. Slaa alisema baada ya kusikiliza utetezi huo na kumhoji muhusika kwa kirefu, Kamati Kuu imeridhia bila shaka kwamba mkakati wa mabadiliko 2013 haukuwa na lengo la kumwezesha Zitto kutwaa nafasi ya mwenyekiti wa chama taifa peke yake.
“Mkakati huo ulikuwa na malengo makubwa zaidi ya kukibomoa chama kwa kukichafua kwa wananchi na kuwachafua viongozi wake wa juu kwa kutumia tuhuma za uongo za ufisadi.
“Kamati Kuu imeridhika kwa ushahidi wa nyaraka mbalimbali zilizoandaliwa na Zitto mwenyewe ama na mawakala wake kutumia vitambulisho bandia katika mitandao ya mawasiliano ya kijamii, kwamba mkakati wa kukibomoa chama umeandaliwa na kutekelezwa kwa muda mrefu,” alisema Dk. Slaa.
Alitaja hujuma nyingine iliyofanywa na Zitto moja kwa moja ni kuwaengua wagombea wa chama katika chaguzi mbalimbali kama ilivyotokea katika majimbo ya Mpanda Mashariki, Musoma Vijijini na Singida Mjini.
“Kamati Kuu imeazimia kwamba kuanzia tarehe ya uamuzi wake, Dk. Kitila na Mwigamba wafukuzwe uanachama wa CHADEMA na vile vile Zitto amekishitaki chama kinyume na matakwa ya katiba yake na kanuni zake,” alisema.
Kwamba Mahakama Kuu imeamuru vikao vyote vya chama visijadili wala kuamua suala lolote linalohusu uanachama wa Zitto.
Hivyo, viongozi wa ngazi zote za chama, wanachama, mashabiki na wapenzi wa CHADEMA popote walipo ndani na nje ya nchi wasishiriki mikutano na shughuli za kisiasa zitakazofanywa na Zitto.
Mamluki CCM
Wakati Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam ikitarajiwa kutoa uamuzi wake leo wa ama uanachama wa Zitto ujadiliwe au usijadiliwe na chama chake hadi kesi ya msingi aliyoifungua isikilizwe, CCM imeandaa vijana mamluki wa kumsindikiza mahakamani.
Tanzania Daima limedokezwa kuwa mkakati huo unaratibiwa na Umoja wa Vijana wa chama hicho (UVCCM) kwa kuwatumia wanafunzi wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam.
Vinara wa mkakati huo ni vijana waliotimuliwa uanachama wa Baraza la Vijana la CHADEMA (BAVICHA) na kisha kujiunga na CCM.
Vijana hao, juzi walifanya kikao na wanachuo wafuasi wa CCM, wakiwahamasisha wafike kwa wingi mahakamani leo mapema kabla ya vijana wa CHADEMA kuwasili.
Mamluki hao waliambiwa wajifanye ni wanachama wa CHADEMA wanaomuunga mkono Zitto katika kesi yake dhidi ya chama chake.
Tayari mamluki hao walihakikishiwa fedha za nauli ya kwenda na kurudi pamoja na kujikimu kwa chakula na mambo mengine.
Tanzania Daima lilidokezwa kuwa fedha hizo zilikuwa zimeahidiwa kukabidhiwa jana baada ya vijana hao kujiorodhesha ili wajulikane idadi yao.
Kiongozi wa mkakati huo, aliwaeleza vijana hao kuwa watakapowasili mahakamani saa 12:00 asuhubi, watatakiwa kumuona yeye au makada wengine waliotimuliwa CHADEMA ambao watakuwa na kadi zaidi ya 100 za CHADEMA na watazigawa ili baada ya hukumu ya kesi hiyo wazichane na kuzitupa