RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Jakaya Kikwete, amesema yeye hana tatizo kukutana na wajumbe wa Bunge Maalum la Katiba kutoka Umoja wa Katiba ya Wananchi (UKAWA).
“Wanajua jinsi ya kukutana nami, ili tuweze kutafuta namna ya kumaliza tofauti hizi,”alisema wakati akizungumza na wanafunzi wa Chuo Kikuu Mzumbe Morogoro, viongozi na wakazi wa vijiji jirani na chuo.
Aidha alisema ana matumaini kuwa mchakato wa katiba unaoendelea utaweza kuwapatia Watanzania katiba mpya.
“Mimi naishi kwa matumaini. Naamini kuwa tutafika mwisho vizuri. Mchakato ni mgumu lakini barabara ndefu haikosi kona. Tukidhamiria kweli tutafika tuendako vizuri,” alisema.
Aliwambia mamia ya wanachuo, watumishi wengine wa chuo hicho: “Maoni yenu ndiyo maoni yangu. Ni jambo la kusikitisha kuwa tofauti hizi za viongozi wa siasa zinaleta mfarakano wa namna hii. Tokea mwanzo niliwaambia kuwa wakiruhusu kushindana na kuviziana katika mchakato huo watakwama.”
“Aidha, niliwaambia kuwa Katiba inayotafutwa siyo katiba ya CCM, ama ya CHADEMA, ama ya NCCR, ama ya CUF. Niliwaambia kuwa hii ni katiba ya wananchi wa Tanzania. Ni vyema tukakubaliana kuwa yenye kutugawa tukayaacha kwa sasa na kukubali kwa yale ambayo hatuna tofauti,” alisema.
Mapema wanafunzi wa chuo hicho waliunga mkono mchakato wa Bunge Maalumu la Katiba wakisema wanaridhishwa na hatua iliyofikiwa na mwendo mzima wa bunge hilo na kuwa mwafaka unawezekana kuhusu vipengele viliyobakia na kupatikana kwa theluthi mbili za kupitisha katiba mpya.
Katika risala hiyo iliyosomwa na Rais wa Chama cha Wanafunzi wa Chuo Kikuu cha Mzumbe, Boniface Maige Juma, wanafunzi hao walisema ni vyema mchakato huo ukaungwa mkono na kila Mtanzania ili kuuwezesha kuleta neema na matarajio yanayokusudiwa.
“Tunaridhishwa na hatua iliyofikiwa na Bunge Maalum la Katiba. Tunaamini kuwa mwafaka unawezekana kwa vipengele vingine vya rasimu ya katiba. Aidha, tunaamini kuwa theluthi mbili za kupitisha katiba mpya zinawezekana kupatikana,” alisema.