Wednesday, July 3, 2013

RAIS WA MISRI ASEMA HATOJIUZULU....

Rais wa Misri Mohamed Morsi ametangaza kwamba hatajiuzulu licha ya madai kutoka kwa idadi kubwa ya waandamanaji ambao wanamtaka aondoke madarakani.

Bw. Morsi alitoa hotuba kwenye televisheni ya taifa Jumanne  jioni na  kuwakumbusha Wamisri kwamba alichaguliwa kidemokrasia zaidi ya mwaka mmoja uliopita. Alisema ana nia ya kufanya kazi zake kwa kanuni za katiba licha ya maandamano makubwa yanayodai kujiuzulu kwake.

Rais  huyo wa Misri pia alisema jeshi linatoa  vitisho vya kutaka  kuingilia kati matatizo ya kisiasa nchini humo. Jeshi  limeonya kwamba litaweka mwongozo wa hali ya baadae nchini Misri ikiwa tofauti kati ya bwana Morsi na wapinzani wake hazitatatuliwa ifikapo leo Jumatano. 

Helikopta ziliruka katika anga ya uwanja wa Tahrir Square, huku waandamanaji wakizishangilia. Maandamano yanazidi kuongezeka huku upinzani ukipata mori  baada ya  jeshi kumtaka rais Morsi kufikia makubaliano ya kugawana mamlaka nao.
Rais wa Misri Mohammed Morsi akihutubia wananchi kupitia televisheni July 2, 2013.
Mmoja wao Mohammed Shaaban anasema rais Morsi anaweza kusema lolote kwa watu waliopo Tahrir Square, lakini  wao ndiyo wenye maamuzi  kwa sasa.

Wachambuzi wa maswala ya kisiasa wanasema waandamanaji wanahisi haya ni mapinduzi ya pili na kwamba walichokidai Januari mwaka wa 2011, ikiwa ni pamoja na   mahitaji ya kimsingi, uhuru na haki bado hayajatekelezwa.

Nazo Uingereza na Ujerumani zimekariri wasiwasi wao kwa  rais wa Marekani Barack Obama juu ya mzozo huo hapo jana na kuhimiza kuwepo kwa suluhisho la amani.