Watu wawili ambao ni askari mgambo, wamekimbilia kusikojulikana bado, wanatafutwa na polisi baada ya kumpiga kwa fimbo kichwani na kumwua mkulima aliyetambulika kwa jina la Gigwa Malegi (55, Msukuma) na mkazi wa kijiji cha Iyonyo.
Taarifa iliyotolewa na Kaimu Kamanda wa Polisi mkoa wa Mbeya, Kamishna Msaidizi wa Polisi, Barakael Masaki inasema kuwa mauaji hayo yalitokea tarehe Mosi Julai, 2013 majira ya saa moja jioni katika kijiji cha Totowe wilayani Chunya, Mbeya.
Taarifa hiyo imewataja watuhumiwa kuwa ni Focus Fabian na Charles (jina la pili halijafahamika bado).
Imeelezwa kuwa chanzo cha kupigwa na kuuawa marehemu kinatokana na kukutwa akilisha mifugo (ng'ombe) kaitka eneo oevu kandoni mwa ziwa Rukwa.
Kamanda Masaki ametoa wito kwa jamii kuacha tabia ya kujichukulia sheria mkononi badala yake amewasihi watatue matatizo yao kwa mazungumzo na kwa kufuata sheria.
Ametoa wito kwa watuhumiwa kujisalimisha mikononi mwa askari mara moja ama yeyote mwenye taarifa za watuhumiwa, azitoe mara moja katika mamlaka husika ili hatua za kisheria zichukuliwe.