Sunday, September 8, 2013

JWTZ LATOA ONYO KALI KWA VYOMBO VYA HABARI VINAVYOANDIKA HABARI ZA UONGO KUHUSU MZOZO WA DRC

JESHI la Wananchi wa Tanzania (JWTZ), limevitaka vyombo vya habari kuacha kuandika taarifa za mgogoro wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC), badala yake taarifa rasmi zitakuwa zikitolewa na jeshi hilo kila baada ya wiki mbili.

Katazo hilo limetolewa jana jijini Dar es Salaam na Meja Erick Komba wakati akizungumza na waandishi wa habari kuhusu maendeleo ya mgogoro huo.

Alisema hali hiyo inatokana na jeshi hilo kubaini kuwa baadhi ya vyombo vya habari nchini vinaandika habari za uchochezi zinazotaka kuziingiza vitani nchi ya Tanzania na Rwanda.

Meja Komba alisema hategemei kama kutakuwa na chombo chochote cha habari kitakachotoa habari kuhusu maendeleo ya mgogoro huo bila kupata taarifa rasmi kutoka jeshi hilo.

Alionya kuwa chombo chochote kitakachokwenda kinyume kitakuwa kina tatizo.
Meja Komba alisema wananchi wanapaswa kuelezwa kuwa kikosi cha Tanzania kilichoko DRC ni sehemu ya Brigedia ya SADC, iliyotoa mchango wake katika Jeshi la Umoja wa Mataifa (Monusco).

Alitaja majukumu ya kikosi hicho kuwa ni kuzuia waasi wa M23 na wengine kujitanua, kuvunja nguvu zao na kuyapokonya silaha makundi yote ya waasi.
“Kwa kuzingatia kuwa kikosi chetu kiko chini ya majeshi ya Monusco, inamaanisha kuwa operesheni hiyo ni ya Umoja wa Mataifa,” alisema.

Aliongeza kuwa Tanzania haikupeleka kikosi chake DRC kwa ajili ya kupigana na M23, pia ieleweke kuwa haina tatizo na Rwanda kuhusiana na operesheni hiyo ambapo Rwanda ilitoa ridhaa kikosi cha Tanzania kwenda DRC.

Meja Komba alisema Rwanda ni miongoni mwa wanachama wa nchi za Maziwa Makuu, ambayo imesaidia kwa kuruhusu kikosi cha Tanzania kupitisha vifaa na zana katika nchi yake kupeleka DRC.

“Tanzania inashiriki katika operesheni hiyo ya ulinzi wa amani nchini DRC kutokana na mgogoro kati ya serikali na waasi hususan kikundi cha M23,” alisema.
Mgogoro huo ulianza Aprili mwaka jana, ambapo kikundi cha M23 kilijitoa katika jeshi la serikali na kuanzisha mapigano yaliyosababisha hali ya usalama nchini DRC kuwa mbaya.

Katika hatua nyingine, Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Bernard Membe Benard, amesema kuwa marais Jakaya Kikwete na Paul Kagame wa Rwanda wamemaliza tofauti zilizokuwa zimejitokeza kati yao hivi karibuni.
Marais hao walikutana na kufanya kikao cha faragha jijini Kampala nchini Uganda juzi baada ya mkutano wa viongozi wa nchi za Maziwa Makuu na baadaye kutoa taarifa kwa waandishi wa habari.

Kuzorota kwa mahusiano kati ya viongozi hao kulikuja kufuatia kauli ya Rais Kikwete ya kumtaka Rais Kagame kukaa meza moja na vikundi vya waasi wa nchi yake vilivyo nchini Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo, ushauri ulioonekana kumkera Rais Kagame.

Akizungumza na waandishi wa habari jana jijini Dar es Salaam, Membe alisema marais hao walitumia mazungumzo yao yaliyochukua muda wa saa moja kujadiliana na kueleweshana mambo mbalimbali yaliyosababisha kutoelewana.
“Baada ya mkutano huo ambao uliwapa fursa za kuchambua, kujadili na kurejesha mahusiano ya kihistoria kati ya nchi hizi mbili, marais wetu walitoka na nyuso za furaha,” alisema.

Moja ya maazimio ya kikao chao ni kuwa na vikao vingine kati ya Rwanda na Tanzania katika siku zijazo.

“Kwa kweli kikao kati ya Rais Kikwete na Rais Kagame kimeondoa majungu yote, kimekata fitina, uongo na maneno ya kuchombeza yaliyokuwa yakitawanywa na watu mbalimbali hapa nchini na hata kule Kigali,” alisema.

Mbali ya kikao hicho pia Rais Kikwete alifanya kikao kingine cha faragha na Rais wa Uganda Yoweri Museveni ambapo walipata muda wa kujadiliana kwa kina kuhusu mambo mbalimbali kuhusu nchi zao na mambo ya migogoro katika nchi za Maziwa Makuu.

Akizungumzia yale yaliyokubaliwa katika mkutano wa viongozi wa nchi za Maziwa Makuu, Membe alisema kuwa mkutano huo kwanza ulimruhusu Rais Museveni aendelee kusuluhisha vita ya serikali ya DRC na waasi.

Alisema kuwa viongozi hao walilaani mashambulizi ya M23 yaliyojeruhi na kumuua Meja Mshindo wa Tanzania aliyekuwa miongoni mwa askari walioko nchini Congo katika kusimamia amani chini ya Umoja wa Mataifa.