Katibu wa Jumuiya na Taasisi za Kiislamu Tanzania, Sheikh Ponda Issa
Ponda amesema alichanganyikiwa kiasi cha kushindwa kujielewa kwa muda
baada ya kupigwa risasi.
Akizungumza katika mahojiano maalumu na Mwananchi kwenye wodi binafsi ya
Taasisi ya Tiba ya Mifupa Muhimbili (Moi) alikolazwa jana, Sheikh Ponda
alisema kutokana na hali hiyo hakumbuki matukio yaliyofuata baada ya
hapo.
“Sikumbuki hata nilipata huduma ya kwanza hospitali gani kwa sababu
sikuwa katika hali ya kawaida. Mambo mengine yaliyotendeka kabla ya
kujeruhiwa ninayakumbuka vizuri,” alisema Ponda ambaye inasadikiwa
kwamba alipigwa risasi ya begani, Ijumaa iliyopita mjini Morogoro.
Alisema alihutubia katika Kongamano la Waislamu kwa muda mfupi
akizingatia muda uliokuwa umetolewa kumaliza mkutano huo na baada ya
hapo alishuka na kupanda kwenye gari binafsi ambalo lilizingirwa na
polisi ndipo akaamua kushuka na kuanza kutembea kabla ya kujeruhiwa.
Mahojiano maalumu na Sheikh Ponda
Swali: Je, watu waliokupa huduma ya kwanza mara baada ya kujeruhiwa walikuta risasi iliyokujeruhi?
Jibu: Nilipigwa risasi kwa nyuma ikatokea mbele kwa hiyo
haikubaki mwilini wala haikuonekana ilipoangukia kwa wakati huo maana
kulikuwa na purukushani.
Swali: Ulipata wapi huduma ya kwanza?
Jibu: Kwa kweli kwa sasa siwezi kukumbuka nilihudumiwa wapi kwa
sababu mara baada ya kujeruhiwa sikuwa katika hali yangu ya kawaida,
nilichanganyikiwa.
Swali: Utathibitisha vipi kama ulipigwa risasi?
Jibu: Bahati nzuri ni kwamba tukio hili lilitokea kweupe wapo
wengi walioshuhudia, kwa hiyo wanaweza kusaidia kuthibitisha na ushahidi
mwingine ni jeraha hili.
Swali: Nini msimamo wako baada ya tukio?
Jibu: Nitaendelea kuzungumzia haki za Waislamu na siwezi kurudi
nyuma. Pamoja na kwamba wananiona mimi ni mtu mchochezi lakini wanaeneza
chuki dhidi yangu kwa njia wanazojua wao. Nitaendelea, risasi
haitaninyamazisha.
Swali: Umehusishwa kufanya uchochezi Zanzibar, unalizungumzia vipi hilo
Jibu: Zanzibar nilichozungumza ni kuhusu kesi dhidi ya viongozi
wa Kundi la Uamsho. Watu wamewekwa ndani kwa miezi tisa sasa, kwa mujibu
wa sheria za nchi yetu, kesi wanayoshtakiwa ina dhamana, sasa nikauliza
kwa hao viongozi, kwa nini hawazingatii sheria?
Kesi zina muda mrefu hazitolewi uamuzi, nikawasisitiza wazingatie
misingi ya sheria kwa kuwa hivyo wanavyowatendea wananchi wajue kwamba
hawastahili kupewa tena ridhaa ya kuongoza nchi, nilifikisha ujumbe
wangu.
Swali: Kuna tukio la kumwagiwa tindikali mabinti wawili wa
Uingereza lililotokea Zanzibar, ambalo wewe pia unahusishwa, hili
unalizungumziaje?
Jibu: Sijaona huo ushahidi ambao wanahangaika kunihusisha na
tukio hilo, nahusishwa vipi? Matukio ya kumwagiwa tindikali yamekuwa
yakijitokeza mara kwa mara huko kabla sijakwenda kuhutubia. Vyombo vya
dola vifanye kazi yake vyema ili kubaini ukweli wa jambo hili.
Pia Mwananchi ilizungumza na mke wake, Sheikh Ponda, Hadija Ahmad ambaye alikuwa ameketi pembeni ya kitanda alicholazwa mumewe.
Swali: Unazungumziaje tukio hili la kujeruhiwa kwa mumeo?
Jibu: Hili ni dhumuni la Serikali, lililenga moja kwa moja
kumdhuru ili kunyamazisha harakati zake za kutetea wanyonge. Ni tukio la
kupangwa, halijatokea bahati mbaya. Serikali inamfuatilia sana hivyo
ililenga kumnyamazisha.
Namshauri Rais (Jakaya Kikwete), kuhakikisha kwamba haki za wanyonge
zinawafikia, asije akafikiri hili lililotokea kwa Sheikh Ponda ni
suluhisho, ni vyema kufanya mazungumzo ili kuweka mabadiliko.
Alivyowaponyoka polisi
Mtu wa karibu wa Sheikh Ponda alisimulia jinsi walivyomsafisha kiongozi
huyo kutoka Morogoro hadi Dar es Salaam na kukwepa vizuizi vya polisi
ambao walikuwa wakiendelea kumsaka.
“Msafara ulikuwa na magari mawili. Moja lilitumika kwa uangalizi,
lingine lilimbeba Sheikh Ponda. Tulipofika Chalinze tulikuta kizuizi
tukakikwepa kwa kupitia Msata kisha Bagamoyo hadi Dar es Salaam na
kumfikisha Muhimbili,” alisema.
Waigomea polisi
Msemaji wa familia ya Sheikh huyo, Isihaka Rashid alisema hawaitambui
tume iliyoundwa na polisi kwa kuwa jeshi hilo ndilo linalotuhumiwa.
“Tunachofanya hivi sasa ni kukusanya ushahidi wetu, kwa bahati nzuri
tayari tumepata mkanda wa tukio lenyewe ambao utatuwezesha kumbaini
aliyemshambulia Sheikh Ponda.
“Hatuwezi kuhitaji majibu ya hiyo tume yao na hata leo kuna maofisa wa
polisi kutoka Makao Makuu na Kituo cha Kati, Dar es Salaam walifika
wakitaka kumhoji eti kuhusu uchochezi lakini alikataa kuzungumza hadi
mwanasheria wake awepo, wakaondoka,” alisema Rashid.
Mwananchi