WAZIRI wa Uchukuzi, Dk Harrison
Mwakyembe, ameanza kufanya ziara ya kushitukiza jana saa 10 alfajiri
katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Mwalimu Julius Nyerere (JNIA),
kuangalia mwenendo mzima wa usafirishaji wa mizigo.
Katika ziara hiyo alitembelea vitengo
mbalimbali, kikiwemo cha ukaguzi wa mizigo na abiria pamoja na kitengo
cha kamera, ambako hivi karibuni kulipita dawa za kulevya za mabilioni.
Dk Mwakyembe amefanya ziara hiyo siku
tatu baada ya kuahidi kuhakikisha inawatia mbaroni watu wanaojihusisha
na usafirishaji wa dawa za kulevya kupitia viwanja vya ndege, kikiwemo
hicho chenye jina la Baba wa Taifa.
Meneja wa Usalama wa wanjani huo,
Clemence Jingu, alikiri Dk Mwakyembe kufanya ziara hiyo ya kushitukiza,
ambapo alioneshwa maeneo pamoja na hatua mbalimbali zinazochukuliwa
uwanjani hapo wakati wa ukaguzi wa mizigo.
Mtoa habari wetu alisema Dk Mwakyembe, alitembelea eneo ambalo dawa za kulevya zilipita na kukamatiwa nchini Afrika Kusini.
Alisema Dk Mwakyembe aliona hali ya
ukaguzi katika eneo hilo ilivyokuwa, na kubaini dawa hizo zilionekana
katika mizigo lakini kulikuwa na uzembe au njama zilizotokana na maofisa
waliokuwa wakikagua.
Kwa mujibu wa mtoa habari huyo, Dk
Mwakyembe alipita katika eneo hilo, ambalo lilikuwa na ofisa wa Polisi
ambapo alielezwa kuwa siku hiyo mbwa wanaotumika kubaini dawa hizo,
walicheleweshwa kufika.
Dawa hizo za kulevya aina ya Crystal
Methamphetamine zenye thamani ya zaidi ya Sh bilioni 6.8, zilikamatwa
nchini Afrika Kusini hivi karibuni wakati zikisafirishwa kutoka
Tanzania.
Kwa mujibu wa taarifa zilizopatikana
kutoka nchini humo, wanawake wawili walikamatwa katika Uwanja wa Ndege
wa Kimataifa wa Oliver Tambo, Afrika Kusini, wakitokea Tanzania.
Wanawake hao walikamatwa wakiwa na
mabegi sita ambayo yalipokaguliwa yalikutwa na kilo 150 za dawa hizo,
ambazo pia zinajulikana kama ‘Tik’.
Akitoa ahadi ya kukabiliana na biashara
hiyo wiki hii, Dk Mwakyembe amesema anajitoa mhanga kuhakikisha Wizara
yake inawatia mbaroni watu wanaojihusisha na usafirishaji wa dawa za
kulevya, kupitia uwanja wa ndege wa Mwalimu Julius Nyerere.
“Nitajitoa mhanga juu ya biashara hiyo
na siogopi vitisho vya watu, maana mimi nilishakufa siku nyingi,
hatuwezi kuidhalilisha nchi yetu kiasi hicho.
“Dawa za kulevya sasa zinasafirishwa
kupitia kiwanja cha ndege, ambacho kimepewa jina la mtu muhimu katika
nchi yetu, Mwalimu Nyerere, ni aibu kwa nchi yetu na Taifa letu, kuona
uwanja huo unatumika kwa biashara hiyo, nipeni muda, mimi ndiye Waziri
wa Uchukuzi, hatutakubali hali hii,” alisema na kuongeza: “Pale uwanjani
kuna ofisi nne, Polisi, Uhamiaji, Usalama wa Taifa na watu wa Mamlaka
ya Viwanja vya Ndege, wote nimewaagiza wanipe taarifa, walikuwa
wanafanya nini hadi dawa hizo zinapita uwanjani hapo?”
Alisema anawapa notisi watu wote
wanaosafirisha dawa za kulevya kupitia uwanjani hapo, watambue kuwa
alishajitoa mhanga kupambana na dawa za kulevya, maana ni biashara
inayodhalilisha Taifa.