TANZANIA NA RWANDA
Rais Yoweri Museveni wa Uganda amesema yuko tayari kuwapatanisha Marais Jakaya Kikwete wa Tanzania na Paul Kagame wa Rwanda baada ya viongozi hao kukaripiana vikali katika miezi ya hivi karibuni. Rais Museveni amesema Maendeleo ya Jumuiya ya Afrika Mashariki yanahitaji viongozi wa jumuiya hiyo kuzungumza kwa sauti moja na kuwa na ushirikiano wa karibu. Ameongeza kuwa, mivutano kati ya Rais Kikwete na Rais Kagame imetoa mwanya kwa viongozi wengine wa Afrika kulisema kwa ubaya eneo la Afrika Mashariki. Hii ni katika hali ambayo, Jana Alhamisi Waziri Mkuu wa Tanzania, Mizengo Pinda alifichua kwamba Rais Kikwete amemuomba Rais Museveni kusaidia kuondoa suitafahamu iliyoko kati yake na Rais Kagame. Pinda alisema Tanzania na Rwanda zina historia kongwe ya ushirikiano wa kisiasa, kiuchumi na kijamii na kwamba vita vya maneno kati ya viongozi wa nchi mbili hizo vimekuwa na athari mbaya kieneo na kimataifa. Mivutano ya Rwanda na Tanzania ilianza baada ya Rais Kikwete kupendekeza kuwa, serikali ya Kigali ifanye mazungumzo na waasi wa FDLR jambo lililoonekana kumuudhi Rais Kagame.