Na Mwandishi wetu,Dodoma
Baadhi ya wajumbe wa Bunge la
Maalum la Katiba ambao ni waumini wa
dini ya Kiislamu, wametaka suala la mahakama ya kadhi iingizwe kwenye katiba
mpya.
Mvutano huo ulijitokeza jana wakati
wakichangia mjadala wa rasimu ya katiba baada ya kamati 12 za bunge hilo
kumaliza kuwasilisha taarifa za mapendekezo yao.
Mmoja wa wajumbe hao, Shekh
Hamid Jongo, aliitaka katiba itamke kwamba kutatungwa sheria ambayo itaeleza kwamba masuala ya ndoa, mirathi na
talaka yataamuliwa kwa mujibu wa imani
ya dini ya kiislamu.
Alisema katika sura ya 10 ibara ya 150 (3) ya rasimu
ya mabadiliko ya katiba inaleza kwamba mahakama ndio chombo cha mwisho cha
kutoa haki na katika dini ya kiislamu mambo ya ndoa, mirathi, wakfu na talaka yanaamuliwa kidini, hivyo utoaji haki kwa
mambo hayo ni ibada.
Aidha alisema kutambulika kwa mahakama ya
kadhi kisheria hakuzuii watu wa madhehebu mengine na wao kudai mambo
wanayoyataka kuwemo katika katiba.
“Waislamu mambo ya mirathi,
talaka, ndoa ni ibada yetu na kamba yanakataliwa
kuamuliwa katika mahakama ya kadhi,” alisema.
Naye mjumbe mwingine,Dk. Zainab
Gama, alisema umefika wakati sasa kilio cha Waisalamu cha kutaka mahakama ya
Kadhi kutambulika kisheria kisikilizwe
ili kunusuru amani iliyopo.
“Chonde chonde nchi yetu hii
ina amani tusiruhusu watu kutumia udhaifu ulipo kuvunja sheria, pamoja na
kwamba Waislamu wameruhusiwa kuanzisha mahakama za kadhi lakini mahakama hizi hazitambuliki
kisheria,”alisema.
Alisema mambo yanayoamuliwa na mahakama za
kadhi yanapofikishwa katikamahakama za kawaida hutupiliwa mbali.
Kwa upande wake, Shamimu Khan, yeye alitaka
kujua kigugumizi kiko wapi kutokana na kushindwa kuingiza mahakama ya kadhi
katika katiba na sheria za nchi.
Alisema kilichopo sasa Waislamu wanapigwa
danadana kwamba suala la mahakama ya
kadhi litawekwa kwenye sheria na kusema jambo hilo haliwezekani kama limeshindwa kutambulika
katika sheria mama ambayo ni katiba.
Mbwana Salum Mbanda yeye
alitaka mahakama ya kadhi itambuliwe kikatiba na Serikali igharamie katika
uendeshaji wake.
Mjumbe mwingine, Hamisi Ally Togwa, alisema
pamoja na ibara ya 32 ya katiba kueleza
uwepo wa uhuru wa imani ya kuabudu dini yoyote lakini Waislamu wamekuwa wakiikosa haki hiyo
kwa muda mrefu.
Baada ya kuchangia, suala hilo liliibua
mvutano ambapo baadhi ya wajumbe walipinga mahakama hiyo kutambulika kikatiba
akiwemo Ave Maria Semakafu na Jasson Rweikiza.
Rweikiza alisema ni makosa kwa Katiba
kuzungumzia mahakama ya kadhi wakati serikali haina dini.
Suala jingine lililoibuka ni uraia
pacha ambapo baadhi ya wajumbe walipendekeza
uraia pacha uruhusiwe kikatiba.
Aliyekuwa wa kwanza kuunga mkono uraia pacha ni Mbunge wa kuteuliwa na Rais, Zakia Meghji
ambaye alisema Watanzania wenye uraia wa nchi za nje, walilazimika kufanya
hivyo kutokana na sababu mbalimbali.