HUU ndio mtindo wa kawaida wa Jeshi la Polisi: kupiga, kujeruhi, kuua na kukanusha kwa nguvu zote.
Jeshi likiona makundi ya watu ambao lina
mzio nao linapiga mabomu kuzusha tafrani; halafu linapiga virungu wale
wanaowayawaya kutokana na macho kuwasha na kwa kuwa kila mtu huanza
kukimbia hovyo ili kuokoa maisha zinapigwa risasi za moto. Waliojeruhiwa
huchanganyikiwa hivyo huwa vigumu kujua risasi zimetoka wapi.
Hata pale maafa yanapomkuta mtu mmoja
mmoja hujengwa mazingira iwe vigumu kujua ukweli hasa nani anahusika
polisi au wahuni wa kisiasa.
Hivyo ndivyo polisi wamefanya mara zote
Arusha, Songea, Morogoro na Iringa. Picha za video za mnato huonyesha
polisi wakilenga kwa bunduki, kufyatua risasi, kujeruhi na kuua na siku
inayofuata kamanda wa polisi wa mkoa au Inspekta Jenerali wa polisi au
msemaji wa Jeshi la Polisi husoma taarifa kukanusha wao kuhusika.
Polisi watasingizia wananchi au vyama vya siasa kisha serikali itadaka uongo huo na kunga’ng’ania kuwa ni ukweli.
Uongo wa Jeshi la Polisi umeikifu jamii,
unaifanya serikali ya Rais Jakaya Kikwete ionekane inanuka na chama
tawala kinachoishi kwa mkono wa chuma wa polisi kimeoza.
Hata mwaka jana polisi walifanya hivyo
dhidi ya wafuasi wa CHADEMA. Katikati ya maandamano yao mjini Morogoro,
walitekeleza amri ya kupiga, kujeruhi na kuua na picha za video
zilionyesha wakilenga na kisha kufyatua risasi ikamuua Ally Zona.
Kesho yake Kamanda Faustine Shilogile
alikanusha na kwa uhodari akadai Zona alipigwa na kitu chenye ncha kali
kilichorushwa kutoka kwa waandamanaji. Hapa alimaanisha CHADEMA ndio
waliomuua lakini hadi leo hakuna mfuasi hata mmoja wa chama hicho
aliyehojiwa mbali ya kushtakiwa.
Wakazi wa Nyololo, Iringa, wakasikia
uongo mtakatifu wa Jeshi la Polisi ambao ulitetewa na serikali. Huko
nako mikanda ya video ilionesha polisi wakimzingira, kumpiga, kumlipua
na kumuaa Daudi Mwangosi na kesho yake polisi wakadai kuna kitu
kilichorushwa kutoka mbali.
Hakuna mfuasi wa CHADEMA aliyenaswa isipokuwa polisi mmoja amefunguliwa mashtaka kukejeli wananchi.
Polisi hawajawahi kukiri kosa; wametetea
mauaji yote na kwa bahati mbaya sana serikali ya CCM nayo imetetea
uhalifu huo bila kujali inajimaliza au la.
Siku pekee ambayo serikali ilikataa
taarifa ya polisi ni Januari 2006 wakati Rais Jakaya Kikwete akiwa bado
mpya, na akifuata ilani ya uchaguzi ya chama chake juu ya kulinda raia.
Mwaka huo aliunda tume chini ya Jaji
Kiongozi mstaafu, Mussa Kipenka, kuchunguza mauaji ya wafanyabiashara
watatu wa Mahenge na dereva teksi mmoja jijini Dar es Salaam.
Tume iligundua kwamba vijana wale
walikuwa wametekwa na polisi eneo la Sinza, wakapelekwa katika msitu wa
Mabwepande ambako waliuawa kwa kupigwa risasi kama wahaini na wakaporwa
madini na fedha.
Kesho yake polisi walidai wafanyabiashara wale walikuwa majambazi, walipora fedha katika kiwanda kimoja.
Mmiliki wa kiwanda alipoulizwa alikiri
kuwepo tukio la wizi kiwandani lakini alikana kuwepo majibizano ya
risasi kama polisi walivyodai.
Sijui nini kilitokea. Tangu polisi
waumbuke katika tukio lile na kwa vile kila tume iliyoundwa, mfano
bungeni, iliibua uoza mkali, JK hakuthubutu tena kuridhia kuunda tume
kuchunguza tukio lolote lile dhidi ya polisi na amekuwa siyo tu
akikubaliana nao bali pia kutetea uongo wao kila walipoua raia.
JK hakutaka kuunda tume tukio la mauaji
yaliyofanywa na polisi Januari 5, 2011 dhidi ya wafuasi wa CHADEMA
mkoani Arusha. Alikubaliana na taarifa ya polisi kwamba CHADEMA ndio
waliokaidi amri na ndio waliohusika na mauaji ya watu watatu waliopigwa
risasi.
JK hakukumbuka tukio la Zona kupigwa
risasi maana polisi wanaonekana wazi wakilenga. Hakutaka kukumbuka tukio
la Mwangosi, na kwa kushukuru kazi nzuri ya Kamanda wa Polisi wa Mkoa
wa Iringa, Michael Kamhanda, aliyesimamia operesheni iliyosababisha kifo
cha mwandishi huyo wa habari, alihamishiwa makao makuu ‘kula bata’.
JK anaona heri lawama kuliko
kufedheheshwa na tume ya kuchunguza tukio la kutekwa, kuteswa kwa
aliyekuwa mwenyekiti wa Jumuiya ya Madaktari, Dk. Steven Ulimboka.
Polisi hawawezi kuendelea na kesi ya
Mkenya Joshua Mulundi aliyesingiziwa mchana kweupe kumteka Dk. Ulimboka.
Wamemfungulia kesi eti ya kuidanganya polisi. Wanachelewesha tu
kumfikisha kortini ofisa usalama aliyehusika na waliomtuma lakini
wanajua siku itafika hawatakuwa na uwezo kuzuia.
JK hakutaka kuumbuka hata kutekwa, kuteswa na kutobolewa jicho kwa mwenyekiti wa Jukwaa la Wahariri (TEF), Absalom Kibanda.
JK hataki na hataunda tume yoyote ya
kuchunguza matukio ya watu waliorusha mabomu katika kanisa Katoliki la
St. Joseph parokia ya Mfanyakazi Olasit mjini Arusha na pili siku chache
wakati wa mkutano wa CHADEMA.
Ule moyo alioanza nao kazi ya urais umepotea; anakubaliana na kutetea uongo wa polisi kwa sababu anajua wanatumwa kufanya hivyo.
JK anajua kuwa polisi walikuwa wanamsaka
kwa udi na uvumba Sheikh Ponda ili afunguliwe tena mashtaka ya
uchochezi. Watanzania hawamuungi mkono Sheikh Ponda kwa uchochezi kama
kweli ameufanya lakini mabomu ya machozi na risasi za nini wakati wa
kumkamata?
Hakuna njia za kistaarabu za kumwita
kiongozi huyo mwenye wafuasi maelfu kwa maelfu nchini. Polisi waliotumwa
na wakubwa zao kutoka Dar es Salaam wameshindwaje kumpa Sheikh Ponda
saa 12 au 24 au 36 au 48 ajisalimishe polisi Morogoro?
Ndivyo polisi wanavyowadhalilisha
Godbless Lema, au Mwenyekiti wa CHADEMA, Freeman Mbowe? Kwa nini polisi
haohao wasitumie njia za kistaarabu badala ya kutanguliza mabomu na
risasi kwa suala la Sheikh Ponda? Hata wakikanusha, nani atawaamini?
Tujiulize kwa nini hakukamatwa Zanzibar
wala Dar es Salaam alikofanya mihadhara mingi, ila Morogoro ndiko
wakubwa wanaagiza akamatwe? Polisi Zanzibar na Dar waliogopa nini?
Je, JK ameamua kuhamishia fikra za watu
kwa wahamiaji haramu na majambazi ili kuvuruga fikra za watu wasifikirie
uhalifu wa kisiasa unaofanywa na Jeshi la Polisi dhidi ya wananchi kwa
maslahi ya CCM?
Imeandikwa na Lwitiko Sr
Source: Tanzania Daima