Kiongozi wa Kanisa la Greek Orthodox duniani, Papa Theodor’s II ameamuru kufungwa kwa ukumbi uliopo ndani ya eneo la kanisa hilo lililopo Kiwanja Namba 7509 katika Barabara ya Ali Hassan Mwinyi jijini Dar es Salaam kufuatia kuwepo kwa picha za utupu za wanawake ukutani..
Papa huyo alifikia uamuzi huo Februari 19, mwaka huu baada ya kutua nchini ambapo alifanya mazungumzo na Rais Jakaya Kikwete.
Mbali na mazungumzo na JK, alipata nafasi ya kutembelea ukumbi huo ulio kwenye eneo la kanisa hilo ndipo ‘alikutana’ na picha za wanawake wa Kiafrika na Kizungu zikiwa zimetundikwa ukutani wakiwa kama walivyozaliwa.
Imeelezwa kuwa baada ya kutua nchini, papa huyo alilala katika nyumba iliyo karibu na kanisa na klabu hiyo na usiku wakati akisali alishangaa kuwaona wanaume, tena wenye mwonekano mzuri wakiingia katika eneo hilo la kanisa akasitisha sala.
Kilichomshangaza zaidi ni kuwaona wanaume hao wakiwa na wasichana wabichi na baada ya kufika klabuni walikuwa wakipiga kelele huku muziki ukisikika kwa sauti ya juu.
Kufuatia hali hiyo, aligundua kwamba watu hao walikuwa wakinywa pombe hadi usiku wa manane jambo ambalo ni kinyume na maadili ya imani hiyo.
“Kesho yake Papa Theodor’s aliamua kutembelea ndani ya klabu hiyo ndipo aliposhuhudia picha hizo chafu nyingi zikiwa zimetundikwa ukutani na chupa tupu za vinywaji vikali.
“Kuona hivyo papa alimuagiza kiongozi wa Bodi ya Wadhamini wa Kanisa, Dimitri Kimon akutane na mapadri wote mwezi wa nne (uliopita) na kujadili hilo nia ikiwa ni kurejesha usafi na kuondoa uchafu huo kanisani hapo.
“Katika mkutano huo waliamua kufunga na kuomba kisha kumtafuta wakili ili aweze kuwatoa waliokuwa wakiendesha ukumbi huo,” kilisema chanzo.
Chanzo kiliongeza kuwa, Julai 8, mwaka huu viongozi hao waliamua kufunga geti la kanisa hilo na kuimarisha ulinzi kwa kutumia kampuni ya ulinzi ili kuzuia wanachama wa klabu hiyo kuingia eneo hilo isipokuwa waumini.
Kiongozi wa kanisa hilo.
Habari zinasema viongozi wa kanisa hilo waliwaambia waliokuwa wakiendesha ukumbi huo kwamba kiongozi wao mkuu hakupendezwa na picha chafu za ukutani na alihoji endapo dini nyingine zikigundua uchafu huo wataelewekaje kwa jamii?
Kuna madai kwamba wengi waliokuwa wakiingia kwenye ukumbi huo ni vigogo katika ngazi ya mawaziri na wabunge ambapo waandishi wetu walibahatika kuona jina la mbunge mmoja likiwa limeorodheshwa katika kitabu cha waliokuwa wakiingia.
Mwanachama mmoja wa klabu hiyo ambaye hakutaka jina lake kuandikwa kwa madai kuwa si msemaji, alisema wanakusudia kufungua kesi mahakamani ili kupinga adhabu ya kufungwa ukumbi huo kwa kuwa wapo eneo hilo kwa muda mrefu.
“Sisi tupo katika eneo hili na tumefanya shughuli zetu siku zote hizo, tunashangaa leo kuona kanisa linatufungia geti. Ni lazima tutachukua hatua za kisheria,” alisema mwanachama huyo.
Mwandishi wetu alimpata wakili wa kanisa hilo ambaye pia ni Katibu Myeka, Edward Chuwa alipoulizwa kuhusu mgogoro huo alikiri kuwepo.
“Ni kweli kuna huo mgogoro kati ya kanisa na waendesha klabu hiyo lakini kwa kuwa mimi ni wakili naomba nisiseme chochote kwa sababu za kimaadili,” alisema Chuwa.
Naye wakili wa waendesha klabu hiyo, Evodi Mmanda alipopigiwa simu na kuulizwa kuhusu mgogoro huo naye alikiri kuwepo.
“Mgogoro huo naujua lakini kwa kuwa mimi ni wakili wao siwezi kusema chochote kutokana na maadili ya kazi yangu.” alisema Mmanda bila kusema ni lini kesi hiyo itasikilizwa.