Yusufu Amani (39) aliyembaka mwanaye wa kumzaa kisha kumzalisha baada ya kutengana na mkewe akiwa kizimbani.
Yusufu akificha sura yake asipigwe picha baada ya hukumu ya miaka 30.Kulia ni mtoto aliyebakwa na baba yake kisha kuzalishwa akiwa na mtoto wake wakati wakitoka mahakamani. Kushoto ni mama mzazi wa binti aliyebakwa na kuzalishwa.
Yusufu akificha sura yake asipigwe picha baada ya hukumu ya miaka 30.Kulia ni mtoto aliyebakwa na baba yake kisha kuzalishwa akiwa na mtoto wake wakati wakitoka mahakamani. Kushoto ni mama mzazi wa binti aliyebakwa na kuzalishwa.
MAHAKAMA ya wilaya ya Mbeya imemhukumu kwenda jela miaka 30 mkazi wa Isanga Mkoani hapa baada ya kumtia hatiani kwa kosa la kumlawiti na kumzalisha binti yake wa kumzaa akiwa na miaka 15( jina linahifadhiwa).
Mwendesha mashitaka wa serikali Archiles Mulisa aliiambia mahakamani hiyo Mbele ya Hakimu Gilbert Ndeuruo kuwa Mshtakiwa huyo ni Yusufu Amani (39) anayedaiwa kumbaka mwanaye wa kumzaa kisha kumzalisha baada ya kutengana na mkewe.
Alisema kosa hilo ni kinyume cha sheria kifungu cha 154 (1)a na 155 sura ya 16 iliyofanyiwa marekebisho mwaka 2002, pamoja na kifungu cha 158(a) cha makosa ya kuzini.
Akisoma Hukumu hiyo Hakimu Ndeuruo alidai kuwa Mtuhumiwa alianza kujihusisha kimapenzi na mwanaye Mwaka 2008 baada ya kutengana na mkewe ambapo Mtuhumiwa aliachiwa watoto wote.
Aliongeza kuwa wakati huo binti huyo alikuwa na umri wa miaka 12 na alikuwa akisoma shule ya msingi darasa la Tano jambo ambalo wamedumu nalo kwa miaka minne hadi ilipogundulika kuwa binti alikuwa mjamzito Mei, 2012.
Alisema mbinu aliyokuwa akiitumia ni kumtishia binti asitoe taarifa kwa mtu yoyote na kwamba baada ya kugundulika kuwa na ujauzito alimwambia amsingizie kijana yoyote mtaani kwao.
Hakimu Ndeuruo alisema Mahakama ilimtia hatiani Mtuhumiwa kutokana na ushahidi wa Mhanga wa tukio hilo ambaye ni binti pamoja na ushahidi wa kitaalamu kutoka kwa Mkemia mkuu wa Serikali.
Alisema ushahidi wa Mkemia Mkuu wa Serikali baada ya kupima Vinasaba kutoka Mtuhumiwa, Mhanga na Mtoto aliyezaliwa ulidai kuwa Mshtakiwa ndiye baba halali wa Mtoto kutokana na Maeneo 15 ya vipimo vya Vinasaba kati ya Baba na Mtoto aliyezaliwa kufungana kwa asilimia 99.9.
Aidha kabla ya kutoa hukumu, Hakimu alimpa nafasi mtuhumiwa kujitetea ili apunguziwe adhabu au asiweze kuhukumiwa kabisa lakini hali ikawa tofauti baada ya Mtuhumiwa kujibu kuwa hana la kujitetea vyovyote itakavyokuwa anachotaka ni nakala ya hukumu.
Kutokana na kushindwa kujitetea Hakimu Ndeuruo alimhukumu kwenda jela miaka 30 na kwamba ana haki ya kukata rufaa katika Mahakama kuu endapo hakuridhika na hukumu hiyo.
Awali katika ushahidi wake Mahakamani hapo, Mtuhumiwa huyo alidai kuwa hakutenda kosa hilo bali alitengenezewa na Mkewe ambaye aliapa kumkomesha baada ya kukosana na kumpata mume mwingine jambo ambalo lilipingwa vikali na hakimu na kudai kuwa “mfa maji haachi kutapatapa”