MWANAUME mmoja aliyeelezwa kuwa ni tajiri mwenye nazo mjini, amezua tafrani na kusababisha timbwili la nguvu kwa dakika kadhaa baada ya kugonganisha wanawake wawili waliodaiwa kuwa chini ya miliki yake kwa wakati mmoja, subiri hapohapo tukujuze!
ANGALIA SINEMA
Hali ya hewa ilikuwa ya kuridhisha kabisa katika eneo la uwanja wa ndege wakati paparazi wetu akiwa kwenye sehemu maalum ya kusubiria abiria wanaotua uwanjani hapo wakitokea nje ya nchi.
Paparazi wetu alikuwa akimsubiri mgeni wake lakini kama ilivyo kawaida ya wanakikosi cha Oparesheni Fichua Maovu ‘OFM’ alikuwa na zana zake za kazi kama kawaida.
VARANGATI LA NGUVU
Kamera za Risasi Mchanganyiko zilishuhudia wanawake wawili wakikunjana na kupigana makonde huku mmoja akimshutumu mwenzake kumwibia mumewe (haikujulikana kama ni wa ndoa). Alisema: “Wewe mpumbavu mwizi wa waume za watu, nitakukomesha leo. Si umezoea kuiba waume za watu? Sasa utanijua mimi ni nani?”
MSHANGAO NI HUU!
Sekeseke wakati likiendelea, yule mwanamke ambaye alikuwa akidai kuibiwa mumewe kwa muda mrefu na mwanamke huyo, watoto wake wawili walikuwa naye sambamba huku wakijaribu kumtuliza ingawa kiumri ni wadogo.
Mwanamke aliyedaiwa kuchukua mume wa mwenzake naye alikuwa na mtoto wake mmoja ambaye alikuwa akimvuta akitaka kumtoa mikononi mwa mwanamke aliyedaiwa kuwa mmiliki rasmi wa tajiri huyo.
“Hawa watoto sijui wamekuja na huyu jamaa? Maana wanaonekana kama wanasoma shule moja na wapo na vifaa vyao vyote vya shule. Hapa hata haileweki jamani,” alisikika dereva teksi mmoja aliyekuwepo eneo la tukio.
Mashuhuda walisema, awali tajiri yule wakati anatoka katika sehemu maalum ya abiria wanaoingia nchini, alikimbiliwa na mwanamke yule anayedaiwa kuwa kimada na kumpokea kisha kumbusu na kumpa pole kwa safari.
“Tatizo lilianzia pale yule mwanamke mwembamba mwenye nguo nyekundu alipoenda kumpokea jamaa. Alimfuata na kumkumbatia kisha akambusu, basi hapo tafrani ikatokea. Yule mke wa jamaa alikwenda haraka na kumvamia kisha kuanza kumpiga,” alisikika mmoja wa mashuhuda hao.
Wakati tafrani ile ikiendelea, mwanaume huyo aliwaingilia kati na kuwaamulia, jambo lililozidisha watazamaji wa sinema hiyo ya bure kushangaa.
Katika hali ya kushangaza, tajiri huyo aliwananga watu waliokuwa wakimshangaa akisema: “Sasa kipi cha ajabu? Ni mwanaume gani hapa ambaye hajawahi kufumaniwa? Haya ni mambo ya kawaida, endeleeni na shughuli zenu nitamaliza hii ishu mwenyewe.”
Baadaye yule mwanamke aliyedaiwa kuwa ndiye mke halali wa tajiri yule, aliondoka naye wakiwa na watoto wao wawili, mwingine akaondoka na mtoto wake.