KIFO cha kikatili cha mwanafunzi aliyeuawa siku chache baada ya
kuhitimu kidato cha nne katika Shule ya Sekondari Luguruni na mkazi wa
Kimara Golani, Dar, Sharifa Rajab (18) bado ni simanzi nzito katika
familia yake.
Sharifa aliuawa kikatili Novemba 22, mwaka huu, Kimara Golani jijini
Dar na mtu anayedaiwa ni mpenzi wake ajulikanaye kwa jina la Abdul (22)
ambaye ni dereva wa bodaboda.
SIMULIZI YENYE MAJONZI
Akizungumza kwa
masikitiko makubwa, baba wa marehemu, Rajab Abdallah alisema siku ya
tukio asubuhi, yeye na mke wake wakiwa kazini, Sharifa aliondoka
nyumbani hapo bila taarifa na kuwaacha wadogo zake tu.
“Tuliporudi
jioni, mimi na mama yake tulianza kuhangaika kumtafuta bila mafanikio.
Mwisho tuliamua kurudi kulala japokuwa usingizi ulikataa. Unajua tena
mtoto ni mtoto. Huwezi kupata usingizi wakati mwanao hujui aliko.
“Tulipanga siku iliyofuata kwenda kutoa taarifa polisi, lakini
ilipofika saa kumi na moja alfajiri, tuliletewa ujumbe kwamba kuna mwili
wa mwanamke umekutwa kwenye chumba cha jirani.
“Ilikuwa vigumu
kusema kwamba mwili huo ni wa mtoto wetu Sharifa, tuliamini kifo kipo,
lakini watakufa wengine si mtoto wetu Sharifa.
“Hata hivyo, tulifunga safari kwenda kuuangalia mwili huo. Sikuamini
hata kidogo nilipogundua kwamba ni mwanangu ndiye alilala kitandani,
amekufa kwa kuchomwa kisu kooni na kwenye mbavu zote, kitanda chote
kilijaa damu. Sharifa alikuwa si Sharifa tena bali marehemu Sharifa,”
machozi yanamlengalenga.
Anaendelea: “Inaniuma sana! Mbaya zaidi nilijua chumba hicho ni cha
kijana ambaye ni dereva wa bodaboda, anaitwa Abdul. Nikajiuliza ina
maana alikuwa ni mpenzi wake? Sikupata jibu.”
TABIA YA MAREHEMU
Baba wa marehemu aliongeza
kuwa, kwa kipindi chote cha uhai, Sharifa hakuwahi kuonesha dalili
kwamba alikuwa katika uhusiano wa kimapenzi, alikuwa ni msiri sana.
MTUHUMIWA WA MAUAJI AACHA UJUMBE
Habari zaidi
zilidai kuwa, baada ya mtuhumiwa huyo kutekeleza mauaji ya binti huyo
aliacha ujumbe wa maandishi akisema kuwa watu wasihangaike kumtafuta
kwani na yeye anakwenda kujiua.
Hata hivyo, mtuhumiwa hakwenda
kujiua, badala yake alifika Kituo Kikuu cha Mabasi ya Mikoani (UBT)
kutafuta usafiri wa kurudi kwao Tanga lakini alipokosa aliamua
kujisalimisha katika Kituo cha Polisi Ubungo na kukiri kuua.
Mmoja wa viongozi wa serikali ya mtaa (hakutaka kutaja jina lake)
alisema mtuhumiwa huyo alipohojiwa polisi alisema hajui kilichotokea,
akaomba apewe nafasi akamzike mpenzi wake huyo.
KAMANDA WA POLISI
Kamanda wa Mkoa wa Kipolisi
Kinondoni, ACP Camilius Wambura alithibitisha kutokea kwa mauaji hayo
ambapo alisema kwa mujibu wa mtuhumiwa alifanya kitendo hicho kutokana
na wazazi wa msichana huyo kukataa yeye asimuoe na tayari alikuwa na
mchumba mwingine.
Marehemu Sharifa alizikwa Novemba 24, mwaka huu katika Makaburi ya
Golani Nzasa, Dar. Mungu ailaze roho yake mahali pema peponi. Amina.
GPL