Dk. Philis Nyimbi anayedaiwa kuzaa na Nabii Mwingira. |
RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk. Jakaya Mrisho Kikwete, ameingilia kati sakata la Mtume na Nabii Josephat Mwingira kudaiwa kuzaa na mke wa mtu.
Habari ambazo Tumezithibitisha ni kwamba baada ya Dk. Morris kufungua mashtaka akimtuhumu Mwingira kuzaa na mkewe, Dk. Philis Nyimbi, alikamatwa na maofisa wa uhamiaji kisha kupewa hati ya kutimuliwa nchini.
tumebaini kuwa JK ndiye aliyezuia hati hiyo na mpaka sasa, Dk. Morris, raia wa Liberia, yupo nchini akiendelea na harakati zake za kusaka haki kisheria kuhusiana na madai yake hayo.
Rais Jakaya Mrisho Kikwete.
JK ALIMFIKIAJE?Inaelezwa kuwa wakati Dk. Morris alipokamatwa, alitokea msamaria mwema (jina tunalo) anayejua ‘njia za kupita’ kufika Ikulu ambaye alimfikishia JK mkanda mzima wa sakata hilo la Mwingira.
“… (anataja jina la msamaria mwema), alimwambia JK kuwa nchi inaelekea katika aibu, Dk. Morris ni mtu anayetambulika Umoja wa Mataifa (UN) hasahasa Shirika la Afya Ulimwenguni (WHO).
“JK baada ya kusimuliwa kila kitu, alichokifanya ni kuingilia kati na kuzuia Dk. Morris asifukuzwe nchini,” kilisema chanzo chetu na kuongeza:
Mtume na Nabii Josephat Mwingira.
“Vilevile JK aliomba namba ya Dk. Morris kisha alimtumia SMS na baadaye wakaongea, akamhakikishia yupo salama nchini lakini kuhusu madai yake kuhusu mkewe, aendelee kufuata sheria.”HATI YAKE BADO INASHIKILIWA NA UHAMIAJI
Habari zaidi zinaweka kweupe pamoja na JK kuzuia Dk. Morris asitimuliwe nchini, bado maofisa wa uhamiaji Mkoa wa Pwani, wanashikilia hati yake ya kusafiria (passport) mpaka leo.
Dk. Morris alipoulizwa kuhusu hilo, alikiri: “Ni kweli wanaishikilia. Niliwaomba wale maofisa wanipe nyaraka inayoonesha passport yangu wanaishikilia. Niliogopa wanaweza kunigeuka. Waliniandikia, kwa hiyo sina wasiwasi.”
Cheti cha ndoa ya Dk. Morris na mkewe Dk. Philis.
SAKATA LENYEWE LIPOJEToleo lililopita la gazeti hili, tuliandika habari yenye kichwa Mume: Mwingira amezaa na mke wangu.
Katika habari hiyo, gazeti hili lilisimamia tuhuma zilizofunguliwa na Dk. Morris kwenye Kituo cha Polisi Kati (Central), Kibaha, Pwani, akidai Mwingira amezaa na mkewe.
Shauri hilo lilifunguliwa kwa kichwa JALADA LA UCHUNGUZI, nambari KBA/PE/20/2011, mtuhumiwa akiwa Josephat Mwingira.
Habari yetu iliyopita, mke wa Dk. Morris, Dk. Philis, alidai alizaa nje ya ndoa baada ya kutekelezwa na mumewe, ingawa alikataa kumtaja mwanaume aliyezaa naye.
Zaidi ya hapo, Dk. Philis alisema Dk. Morris hakuwa mwaminifu kwenye ndoa, kwani alidiriki kumsaliti kwa binti mwenye umri chini ya miaka 18 ambaye wao kama mke na mume, wangeweza kumzaa.
Mtoto wa Nabii Mwingira aliyezaa na Dk. Philis. |
DK. MORRIS NA MWANDISHI WETU
Katika kumchimba zaidi Dk. Morris, mwandishi wetu alifanya naye mahojiano kama ifuatavyo;
MWANDISHI: Ni kweli ulimtelekeza mkeo ndiyo maana akaamua kusaliti na kuzaa nje ya ndoa?
DK. MORRIS: Si kweli hata kidogo, amenisingizia, naomba amuogope Mungu.
MWANDISHI: Una ushahidi wowote kuwa ulikuwa unamjali mkeo?
DK. MORRIS: Ushahidi upo wa kutosha. Anazungumzia kipindi cha kuanzia mwaka 2006 mpaka 2011, ni kipindi ambacho nilikuwa naishi Marekani kikazi WHO.
Kipindi hicho, nilikuwa namtumia mke wangu dola za Kimarekani 2500 (zaidi ya shilingi 4,000,000) kila baada ya wiki mbili lakini kuna wakati nilikuwa nampa zaidi ya hizo.
Gazeti hili lilioneshwa nakala ya karatasi za kibenki zikionesha jinsi alivyokuwa akimuingizia fedha mkewe aliyekuwa na akaunti katika Benki ya Standard Chartered Moshi (namba ya akaunti tunaihifadhi), yeye akiwa Marekani akitumia Bank of America kuanzia mwaka 2006.
MWANDISHI: Hebu niambie, Dk Philis bado ni mke wako? Yeye anasema wewe siyo mumewe.
DK. MORRIS: Ni mke wangu halali wa ndoa takatifu. Nilifunga naye ndoa katika Kanisa la St Alban, Dar Desemba 23, 2001, nikiwa na umri wa miaka 39 na yeye (mkewe) akiwa na miaka 30.
Ndoa hiyo niliigharamia sana tangu mavazi ya wapambe wangu na wa mke wangu. Ilikuwa siku ya furaha kabisa. Sikupenda wakwe zangu wapate shida.
MWANDISHI: Ukiwa Marekani ulipata habari zozote za kuwa mkeo ni mjamzito au kajifungua?
DK. MORRIS: Hapana, sikuwa na habari kabisa juu ya jambo hilo na ndiyo maana nilikuwa nikimtumia fedha za kutosha.
Kuna siku moja aliniambia anataka kwenda kufanya utafiti Afrika Kusini, akawa anataka dola 2500 siku hiyohiyo aliyoniambia. Nilimwambia taratibu za fedha Marekani ni ngumu. Nilikwenda ofisini kwangu nikaomba malipo ya awali ya mshahara wangu, nikamtumia dola za Kimarekani 3,000 (shilingi milioni 4.8 kwa cheji ya sasa).
MWANDISHI: Uliporejea Tanzania, ilikuwaje ukajua mkeo amezaa nje ya ndoa?
DK. MORRIS: Nakumbuka usiku mke wangu alianza kulia. Nilishangaa nikamuuliza kwa nini unalia, akanijibu kwamba anaomba nimsamehe kwa sababu amezaa nje ya ndoa.
MWANDISHI: Baada ya kusikia hivyo ulijisikiaje?
DK. MORRIS: Niliishiwa nguvu kabisa, nikamuuliza kwa nini amefanya usaliti huo? Nilimuuliza ni nani amempa mimba, akaniambia ni mwanaume mmoja injinia ambaye alidai yupo Marekani kwa wakati huo.
MWANDISHI: Hayo ulikuwa unamuuliza mkiwa wapi Dar au Kibaha?
DK. MORRIS: Tulikuwa Moshi, nikiwa Marekani mke wangu aliniambia yupo Moshi anachukua shahada ya pili (Master) ya udaktari, na nilikuwa namtumia fedha za pango la nyumba, lakini pale nilimkuta hotelini, kesho yake tukarudi Dar.
MWANDISHI: Baada ya kufika Dar mambo yalikuwaje?
DK. MORRIS: Mke wangu aliniambia kuwa ni lazima nimsindikize kwa Nabii Mwingira ili akaombewe kwa ushetani alioufanya wa kuzaa nje ya ndoa.
MWANDISHI: Ulikubaliana naye?
DK. MORRIS: Nilimkubalia tukaenda kwa sababu wakati huo nilikuwa sijajua kuwa yeye ndiye mbaya wangu. Tulimkuta na akatukaribisha ofisini kwake.
MWANDISHI: Mambo yakawaje?
DK. MORRIS: Mwingira alituombea, wakati akituombea Mwingira mwenyewe alilia sana.
MWANDISHI: Ukaja kumtuhumu vipi tena Mwingira kuwa amezaa na mkeo?
DK. MORRIS: Subiri kwanza, kesi ikishakuwa mahakamani yote yatakuwa wazi. Nitataka pia tupimwe kila kitu, DNA pamoja na Ukimwi.
MWANDISHI: Vipi madai ya wewe kutimuliwa nchini?
DK. MORRIS: Namshukuru sana Rais Kikwete, ni kiongozi mzuri, alinisaidia sana. Namuamini, nampenda na nawaomba Watanzania wampende kiongozi huyu, ni mpenda haki.
MWINGIRA BADO SHIDA
Jitihada za waandishi wetu kumpata Mwingira bado hazijazaa matunda, kwani kila njia inayotumika, wasaidizi wake hawataki kabisa kiongozi huyo wa Kanisa la Efatha, afikiwe na kuhojiwa kuhusu madai haya.
Hata hivyo,halijakata tamaa, litaendelea kumsaka mpaka apatikane na kujibu tuhuma hizo.