Dereva aliyeuawa ametajwa kwa jina la Ramadhani Giza, mkazi wa Gongolamboto na majeruhi alifahamika kwa jina la Mwarami Mshana mkazi wa Ubungo Maziwa.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kinondoni, Camillius Wambura.
Akisimulia tukio hilo, Hamdan Rajabu ambaye aliporwa fedha hizo pamoja na vocha za simu zenye thamani ya Sh. 400,000 alisema majambazi hao walifika mtaani hapo usiku wakiwa na bunduki na moja kwa moja walimfuata dukani na kumuaru awape fedha.
Alisema wakati akitoka nje ya duka lake mlangoni alikutana na jambazi moja na kumwamuaru arudi ndani ya duka na kumpa fedha haraka. Aliongeza kuwa baada ya kuambiwa hivyo alishikwa na butwaa na ghafla jambazi huyo alimtolea bastola mbili na bunduki moja iliyokatwa kitako na kumtaka alale chini kifudifudi.
Rajabu alisema baada ya kuona hali imekuwa ngumu, alilazimika kutii amri na kulala na kwamba aliambiwa atoe fedha zote za mauzo ya siku hiyo.
“Niliambiwa niwape fedha na wakati huo jambazi mwingine alikuwa ameingia ndani na hivyo kufanya idadi ifikie wawili na niliwaambia wafungue droo na kuchukua chochote watakachokikuta humo na ndipo walipofungua na kukusanya mauzo yote yaliyofikia Shilingi laki sita,” alisema.
Alisema kabla ya kumaliza uporaji huo, waliona gari la TBC alilokuwa akiendesha marehemu ambalo lilikuwa limeegeshwa pembezoni mwa barabara likiwasha taa na kuonyesha dalili za kuondoka ndipo jambazi mwanamke alipomfyatulia risasi na kumuua papo hapo.
Mashuhuda wa tukio hilo waliongea na paparazi wetu kuwa tukio hilo lilikuwa kama sinema kwa kuwa kila jambazi alikuwa akifanya kazi yake kwa umakini huku madereva waliokuwa wamewabeba majambazi hao wakiwa wamebaki kwenye piki piki bila kuzizima.
Majeruhi huyo amelazwa katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili na kwamba hali yake inaendelea vizuri.
Marehemu alikuwa kwenye gari lenye namba za usajili STK 355 Toyota Land Cruiser mali ya shirika hilo lililokuwa limeegeshwa karibu na eneo la tukio akiwa na mwanamke aliyefahamika kwa jina la Mwanakombo Daud (41), mfanyabiashara na mkazi wa eneo la Ubungo maziwa.
Katika tukio hilo majambazi hayo yalimjeruhi kwenye kiuno Mharami Rajabu (25) ambaye ni dereva wa gari kenye namba za usajili T.404 BLZ Mitsubish Fuso aliyekuwa ameegesha gari eneo hilo la tukio.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kinondoni, Camillius Wambura, alisema dereva huyo aliuawa na majambazi wanne ambao walivamia duka la Namanga Shopping Center linalomilikiwa na Hamdan Rajabu (45).
Wambura alisema majambazi hao walifanikiwa kupora vocha za simu zenye thamani ya Sh. 400,000 na fedha taslimu na kwamba wakati wote wa tukio hilo la uporaji likiendelea jambazi mwanamke ndiye alikuwa kiongozi wao wa kulinda eneola nje.
Alisema kufuatia tukio hilo, Polisi wanaendelea na msako mkali wa kuwasaka wahalifu wanaojihusisha na ujambazi wa kutumia silaha, unyanganyi wa kutumia nguvu, wauzaji wa madawa ya kulevya pamoja na uhalifu mwingine.