SIKU chache baada ya kikundi cha Al Shabaab kudaiwa kuteka Jengo la Westgate nchini Kenya na kuua watu kadhaa na wengine kujeruhiwa wasiwasi wa magaidi kulipua tena nchi hiyo umetanda.
Tayari Marekani imetoa angalizo kwa Kenya kuhusu uvamizi huo na kuitaka isibeze kuchukua tahadhari kama ilivyofanya kwa tukio la Westgate na kusababisha madhara makubwa kwa wananchi.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa hivi karibuni na Baraza la Ushauri la Usalama wa Nje la Marekani ni kwamba kuna uwezekano mkubwa wa kutokea tena kwa shambulizi la ugaidi nchini Kenya.
Marekani imesema shambulio hilo litafanywa na kundi jipya la wanamgambo wa Kenya la Al Hijra ambalo linashirikiana na Al Shabaab na lengo lake ni kuharibu maeneo nyeti.
Kutokana na hali hiyo, Serikali ya Marekani imewataka raia wake kuwa makini wakati wanapokuwa kwenye maeneo ya umma katika miji ya Nairobi na Mombasa.
Tahadhari hiyo imekuja ikiwa ni siku kadhaa baada ya Al Shabaab kuishambulia Kenya mwaka huu na Uganda mwaka 2010 na kusababisha vifo vya watu 77 ambao walikuwa wanaangalia mchezo wa mpira kwa njia ya televisheni.
Tukio la Westgate lilisababisha Umoja wa Mataifa (UN), Uingereza, Marekani na mataifa mengine makubwa kuelekeza masikio nchini Kenya kutokana na kushtushwa na shambulio hilo