Spika wa Bunge, Anne Makinda amesema hatishwi na mchakato wa
kumng’oa katika nafasi yake ambao umeanzishwa na Mbunge wa Nzega, Dk.
Khamis Kigwangalla kutokana na tuhuma za kukiuka kanuni za Bunge.
Kadhalika
Spika Makinda amepuuza hoja za Dk Kigwangalla akisema kuwa yeye
hajavunja kanuni yoyote, lakini akaweka bayana kuwa mbunge huyo wa Nzega
ana haki kwa mujibu wa Kanuni za Bunge kuendelea na kile anachokifanya.
“Kanuni
si zinamruhusu, utaratibu upo kwenye kanuni za Bunge kwa hiyo aendelee
na mchakato lakini mimi ninachosema sitetereki maana hakuna kanuni
yoyote ambayo nimeivunja,” alisema Makinda katika mahojiano maalumu na
Mwananchi ofisini kwake jana.
Wakati
Spika akitoa kauli hiyo, jana, Dk Kigwangalla alianza harakati zake za
kukusanya saini za wabunge, akitafuta kuungwa mkono katika hoja ya
kutokuwa na imani naye kwa madai kwamba amekuwa akikiuka kanuni.
Miongoni
mwa madai ya Dk Kigwangalla ni hatua ya Makinda kufanya uteuzi wa
Mbunge wa Bariadi Magharibi, Andrew Chenge kuwa Mwenyekiti wa Kamati ya
Bunge ya Bajeti, tofauti na kanuni zinazotaja wenyeviti kuchaguliwa na
wajumbe wa kamati.
Hoja nyingine ni
kamati hiyo ya bajeti kulipwa posho ya Sh430,000 wakati wajumbe wa
kamati nyingine wamekuwa wakipewa Sh130,000 pamoja na kumteua Mbunge wa
Kigoma Mjini, Peter Serukamba kuingia katika kamati hiyo ya bajeti
wakati mbunge huyo ni Mwenyekiti wa Kamati ya Miundombinu.
Jana
Dk Kigwangalla aliwasilisha hoja yake kwa Katibu wa Bunge na kuongeza
madai mapya yakiwamo ya kuagiza kwa mabavu majedwali ya mabadiliko ya
sheria kwenda kwenye kamati ya bajeti, kuvunja masharti ya kanuni ya 48
inayotoa maelekezo ya namna ya kuwasilisha na kujadili jambo la dharura
na kutumia madaraka yake vibaya kwa kuvunja masharti ya Sheria ya The
National Assembly (Administration) Act (Cap.115) ya mwaka 2008.
Makinda
akijibu hoja hizo jana alisema alifanya uteuzi wa Chenge kuongoza
Kamati ya Bajeti kwa sababu kamati hiyo ni mpya na haikuwapo katika
kamati za awali, hivyo ni wazo ambalo lilitokana na mawazo ya Bunge la
sasa.
“Tulikuwa tunafikiria jinsi Bunge
linavyoweza kuisadia Serikali ipate vyanzo vipya vya mapato. Kwa hiyo
tumehitimisha wazo hili kwa kuamua kuwa na Kamati ya Bajeti. Kamati hii
haikuwapo na wala utaratibu wake wa kikanuni haukuwapo. Niliamua na
kanuni zinanipa uwezo huo kwamba niteue mtu ambaye ninaamini anaweza
kuisimamia katika hatua za mwanzo ili tuone uzoefu utatufikisha wapi,”
alisema Makinda na kuongeza:
“Kamati
hii hata Serikali ilikuwa haikubaliani na sisi, lakini katika muda mfupi
wa utendaji wake umefanya kazi kubwa na kama tusingekuwa na Mzee Chenge
ambaye ni mzoefu na anafahamu vizuri utendaji wa Serikali basi
tungeshindwa na mimi siko tayari kuanzisha kitu halafu nikashindwa”.
Kuhusu
posho, Spika aliungana na kauli ya Katibu wa Bunge, Dk Thomas
Kashililah kwamba si wakati wote Kamati ya Bajeti imekuwa ikipewa malipo
zaidi, bali ni pale tu wanapofanya kazi nje ya siku na saa za kazi tena
kwa kibali chake.
“Lazima walete
maombi na waeleze kwa nini wanapaswa kufanya kazi kwa muda wa ziada au
siku za mapumziko na mimi nikisharidhia basi wanalipwa mara mbili ya
viwango vya kawaida na hiyo ni kwa mujibu wa taratibu na Kanuni zetu,”
alisema.
-----MWANANCHI