Tuesday, October 15, 2013

Ufoo Saro alikimbilia kwa fundi wa samani



Ufoo Saro


FUNDI wa samani, mkazi wa Kibamba Kibwegere , ndiye aliyemhifadhi mwandishi wa habari wa ITV, Ufoo Saro katika kibanda chake na kwenda kumtafutia usafiri kwa ajili ya kumpeleka hospitali.
Akizungumza na gazeti hili jana, fundi huyo ambaye hata hivyo hakuwa tayari kutaja jina lake, alisema Ufoo alifika katika eneo wanalofanyia kazi akiwa amejishika tumbo kama mtu mwenye maumivu na kumuomba amsaidie kupata usafiri utakaomfikisha Hospitali ya Tumbi.
Kibanda hicho kiko meta kama 100 kutoka nyumbani kwao na inadaiwa alikimbilia hapo kujiokoa na mzazi mwenziwe, Anthery Mushi, aliyekuwa ameshamuua mama yake mzazi, Anastazia Saro (58).
“Alikuja na kunieleza huko nyumbani kumeshaharibika, akilalamika kuwa amepigwa risasi na hajui ndugu zake wapo katika hali gani kwa kuwa muuaji bado alikuwa akizungukazunguka ndani ya nyumba,” alisema fundi huyo.
Alisema ilikuwa ngumu kwao kuendelea kumhoji kutokana na hali aliyokuwa nayo Ufoo kwa wakati huo.
“Hata yeye baada ya kuona tunamuuliza sana maswali, aliingia katika moja ya chumba cha duka (anamuonesha mwandishi hicho chumba) na kukaa katika kiti, huku akiugulia maumivu na nilichokifanya ni kusimamisha pikipiki na kumwagiza dereva ampeleke kwanza Kituo cha Polisi Mbezi Mwisho, ili apatiwe PF 3, hata hivyo Ufoo alitaka apelekwe hospitali moja kwa moja,” aliongeza.
Kwa mujibu wa shuhuda huyo ilibidi wakubaliane na matakwa ya Ufoo ambapo pikipiki hiyo ilimbeba na kuondoka naye kwenda hospitali.
Alisema baada ya Ufoo kuondoka, ilimbidi aondoke na kwenda katika moja ya nyumba iliyopo jirani na nyumba ya akina Ufoo na kumuita mmoja wa jirani aliyemtaja kwa jina la Ustadhi, na kumuuliza kama anajua suala lolote linaloendelea katika eneo hilo.
Hata hivyo anadai jirani yake pia alikiri kusikia milio ya risasi kutoka katika nyumba hiyo, bila kujua ni ya nini na ndipo alipomueleza kuhusu Ufoo kupigwa risasi ambapo wote kwa pamoja waliamua kusogea jirani kujua nini kinachojiri.
Ufoo bado yuko katika Hospitali ya Taifa Muhimbili na mama yake anatarajiwa kusafirishwa leo kwa maziko yatakayofanyika katika kijiji cha Shali, Machame mkoani Kilimanjaro.
Mama yake Ufoo anatarajiwa kuagwa nyumbani kwake leo saa tano asubuhi ambapo saa saba mchana mwili utapelekwa katika Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), Usharika wa Kibwegere kabla ya kuanza safari ya kwenda Moshi baadaye leo.
SOURCE:HABARI LEO