Sunday, October 27, 2013

NEY WA MITEGO APIGWA MARUFUKU NA BASATA KUVAA “MLEGEZO........


 Ney wa Mitego

ney wa Mitego ni msanii wa Hip-Hop.Sifa yake kubwa aliyonayo ni pamoja na “kusema chochote”. Kwa lugha za mjini wanasema Ney anakuchana tu. Haogopi. Nyimbo zake mbili ambazo hivi sasa zinamuweka kwenye chati ni Muziki Gani alioshirikiana na Diamond pamoja na ule wa Salamu Zao.
Pamoja na kuwa msema chochote, Ney wa Mitego anayo pia sifa ya kuwa msanii mvaa mlegezo mkubwa. Kwako wewe msomaji ambaye yawezekana hujui mlegezo ni nini; ni hii style ya vijana wa siku hizi kuvaa suruali na kuzishusha kwa nyuma na kuacha chupi au boxers zao zikionekana. Mlegezo una historia ndefu na ambayo imeshazungumziwa mara nyingi katika vyombo mbalimbali vya habari.Historia yake inasemekana kuanzia nchini Marekani katika jela. Hiyo ni makala nyingine inayojitegemea.
Sasa inaelekea Ney Wa Mitego naye kapata mtu ambaye anaweza kumwambia chochote. Ni Baraza La Sanaa La Taifa(BASATA) ambao, kwa mujibu wake mwenyewe Ney wa Mitego na taarifa iliyoripotiwa katika vyombo mbalimbali vya habari, wamemwandikia barua wakimtaka kuacha mara moja tabia yake ya kuvaa mlegezo.BASATA, bila shaka, wanaona mlegezo wa Ney kama uchocheaji wa anguko la kimaadili miongoni mwa wasanii. Binafsi nimewahi kujiuliza maana halisi na uzuri wa fasheni hii ya mlegezo na sikupata jibu. Ningempata Ney ningemuuliza kwa undani zaidi kuhusu hili.
Wakati nikisubiri kwa hamu kuona jinsi Ney Wa Mitego atakavyotekeleza amri au ombi hilo la BASATA, nabaki na swali moja au mawili kichwani. Vipi wasanii wengine (ambao ni wengi tu) wanaovaa pia mlegezo BASATA litawaandikia pia barua?Na Je,BASATA watamfanya nini NEY endapo atakaidi agizo hilo?
Kisha lipo suala pana zaidi la maadili miongoni mwa wasanii nchini wakiwemo wale wa kike ambao pamoja na kutovaa mlegezo kama wa Ney,wao wana “mlegezo” wa nguo fupi kupita kiasi au zile zinazoacha asilimia 80-90 ya miili yao wazi. Sijui hili BASATA wanaliangaliaje. Kuna mengi.Tutaongea siku moja…