MTOTO aitwaye Mwajuma Haji (16)
ambaye amelazwa katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili anayesumbuliwa na
ugonjwa wa kusinyaa kwa viungo yuko katika hali mbaya baada ya baadhi
ya ndugu kudaiwa kutaka auawe ili kutoa uchuro katika familia.
Kwa mujibu wa mama mzazi wa mtoto
huyo, Tatu Musa baadhi ya ndugu (siyo wote) wamekata tamaa ya kumuuguza
mtoto huyo na kupendekeza heri mtoto huyo akatishwe maisha yake.
“Mwanangu haumwi wala hajawahi kuumwa
ila ghafla alianza kusinyaa na kukosa nguvu, kinachoniuma baadhi ya
ndugu zangu wamekata tamaa wanataka wamuue, waniachie mwanangu,” alisema
mama huyo huku akilia mfululizo.
Mwandishi wetu amemshudia mtoto huyo akiwa amesinyaa viungo kiasi cha kutoweza kufanya kitu chochote zaidi ya kulala.
Mama mzazi wa mtoto huyo alisema kuwa
alijifungua mtoto huyo akiwa na afya njema lakini alipofikisha umri wa
miaka mitatu hali ikabadilika na viungo vyake kuanza kusinyaa.
Mama huyo amedai kwamba kutokana na
hali hiyo hakuweza tena kufanya shuguli za kumwingizia kipato zaidi ya
kukaa na mwanaye kijijini kwao, Kiamange, Bagamayo mkoani Pwani bila ya
kupata matibabu ya uhakika.
Alisema kwamba maisha ya mtoto wake
yameendelea kuwa mabaya bila ya kupata msaidizi kutokana kutengwa na
baadhi ya ndugu zake waliokata tamaa ya kumuuguza.
Aidha, Mama Mwajuma amedai kwamba
kuna wakati alikuwa akimfungia ndani mwanaye kuanzia asubuhi ili aende
kulima na kupata chochote, lakini aliporudi nyumbani alimkuta katika
hali mbaya sana.
Kutokana na mazingira kuwa magumu,
mama huyo alidai kwamba hakuwa na msaidizi wa kuweza kumwachia mwanaye
ili aweze kuhangaikia kipato.
Mbali na mtoto huyo, mama huyo
alibahatika kupata mtoto mwingine ambaye sasa ana umri wa mwaka mmoja na
nusu lakini baada ya kujifungua mwanaye mkubwa akatokwa na vidonda
mgongoni.
Baada ya mtoto huyo kusumbuliwa na
ugonjwa huo kwa muda mrefu alishauriwa kumpeleka Muhimbili na kumuacha
mwanaye mdogo kwa majirani.
Baada ya muda alipata taarifa kwamba
mtoto wake mdogo anaumwa, ikabidi akamchukue na kumleta Muhimbili ili
aishi naye ingawaje hairuhusiwi kwa mtoto kuishi wodini.
“Nina wakati mgumu, kwa kuwa nina
watoto wawili sina cha kufanya kwa kuwa huyu mwingine hajiwezi kwa
chochote zaidi ya kumsaidia kwa kila kitu, mbaya zaidi ndugu
wamenitenga,” alisema huku akibubujikwa machozi.
Ndugu Mtanzania mama Mwajuma yuko
katika hali mbaya sana, kama unataka kumsaidia mtoto wake tuma mchango
wako kupitia namba 0754 021 301