MKOA wa Morogoro na vitongoji vyake kwa sasa umegubikwa na simanzi
kubwa baada ya watu watano wa familia moja kufariki kwa mpigo katika
ajali ya gari.
Ajali hiyo iliyohusisha gari ndogo aina ya Toyota Cardina, yenye
namba za usajili T 180 AWT na Fuso namba T324 AWL lililokuwa
likiendeshwa na John Mombozi likitokea Dar es Salaam, ilitokea Oktoba
13, 2013, eneo la Visiga, Kibaha mkoani Pwani.
NI MHADHIRI WA SUA
Watu waliofariki katika ajali
hiyo ni pamoja na mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Kilimo Sokoine (SUA)
aitwaye Mwaitulo Suma Andalwisye aliyekuwa dereva wa gari ndogo na
wanawe watatu; Gamalieli Mwakyami, Happiness Mwakyami na Jeremy Mwakyani
pamoja na mtumishi wao wa ndani, Elita Mpagama.
Simanzi imeivaa
familia hiyo ambayo kwa sasa imebaki na baba tu aitwaye Jimmy Wilson
Mwakyami, mwajiriwa wa Kiwanda cha Sukari Kilombero, Morogoro ambaye ni
Injinia.
IDD YA BALAA
Habari zilizopatikana eneo la msiba
zinasema kwamba, Bi. Mwaitulo (36) alikuwa akielekea jijini Dar es
Salaam ambapo angeiacha familia yake nyumbani kwa mama yake mdogo,
Sister Mwakatogo ili wale Sikukuu ya Idd wakati yeye akiwa safarini
Kampala, Uganda kikazi.
Ilielezwa kuwa, kwa sababu mumewe alikuwa kazini Kilombero,
walikubaliana aichukue familia hadi Dar kwa bibi yao ili aiche hapo
halafu yeye aendelee na safari yake ya Uganda.
“Huyu dada jamani
ananiuma sana...unajua alipata safari ya kikazi kwenda Kampala, sasa
akaona si busara kuwaacha watoto peke yao nyumbani, baada ya kushauriana
na mumewe ndiyo akaamua kuwachukua akawaache kwa bibi yao, akirudi
awapitie - kumbe Mungu alishapanga yake.
“Inauma sana. Mimi namuonea huruma zaidi huyo mumewe. Inahuzunisha
sana. Kuondokewa na familia nzima siyo jambo dogo. Mungu atamwekea
wepesi na kumpa moyo wa ustahimilivu,” alisema jirani mmoja kwa sharti
la kutoandikwa jina lake gazetini kwa kuwa si msemaji wa familia.
SIMULIZI YA MAJONZI
Kati ya mambo yaliyozidisha
majonzi katika ibada ya kuwaombea marehemu hao, Oktoba 15, mwaka huu
nyumbani kwao, Sua mjini hapa ni namna ndoto za watoto waliofariki
pamoja na mama yao zilivyozimika kama mshumaa kwenye upepo mkali.
Mtoto wa kwanza katika familia hiyo, Gamalieli (8) alikuwa anasoma
darasa la nne katika Shule ya St. Marry’s mjini hapa, Happiness (5)
alikuwa chekechea na Jimmy akiwa na umri wa miaka miwili tu wakati
mtumishi wao wa ndani akiwa na miaka 18.
KIU YA ELIMU
Mhadhiri huyo alikuwa mama bora wa
kuigwa katika familia za Kitanzania kwa kuwa alikuwa akipigania sana
elimu. Kabla hajaanza kazi chuoni hapo, alipata elimu yake hapohapo, pia
hadi mauti yanamkuta alikuwa akiendelea kusoma.
Mwaka 1999
alijiunga chuoni hapo akitokea Shule ya Sekondari Loleza, Mbeya ambapo
alihitimu Shahada ya Kwanza katika Kilimo cha Bustani ‘Bachelor of
Science in Horticulture’ mwaka 2003 na kuajiriwa hapohapo kama Mhadhiri
Mkufunzi.
Katika kujiendeleza zaidi mwaka 2007 alianza masomo ya
Shahada ya Uzamili katika Mimea na Vipando ‘Master of Science in Crop
Science’ ambapo alihitimu mwaka 2009 – akapandishwa cheo na kuwa
Mhadhiri kamili.
Mpaka mauti yanamkuta alikuwa akisaka Shahada ya Uzamivu ‘Doctor of Philosophy – PhD’ chuoni hapo.
BABA ASHINDWA KUZUNGUMZA
Gazeti la Ijumaa
lilimshuhudia mume wa marehemu Mwaitulo, Jimmy (mwenye shati ya
michirizi) ambaye ajitihadi kujikaza na kupita mbele ya majeneza yote
huku machozi yakimbubujika.
Ijumaa lilitaka kuzungumza naye mawili
matatu kuhusiana na namna alivyoupokea msiba huo, lakini hakuweza
kutokana na kuzidiwa na huzuni.
SAFARI YA MBEYA
Kaimu Mkuu wa SUA, Utawala na
Fedha, Profesa Jayro Matovelo alisema chuo kimepokea msiba huo kwa
mshtuko mkubwa na kwamba marehemu alikuwa mchakapazi sana.
Baada ya
ibada na kutoa heshima za mwisho kwa marehemu hao, msafara wa kuelekea
nyumbani kwao, Kyela, Mbeya ulianza mishale ya saa 9 alasiri.
SOURCE:GPL