Thursday, October 3, 2013

HUDUMA YA TRENI YA JIJI YASITISHWA KWA MUDA BAADA YA KICHWA CHA TRENI KUPATA AJALI

Uongozi wa Kampuni ya Reli Tanzania (TRL) Unasikitika  kuwaarifu Wakazi wa Jiji na Wananchi kwa ujumla kusitishwa huduma treni ya Jiji ( Dar- Ubungo Maziwa) kwa siku ya leo ya Alhamis Oktoba 03, 2013. Hatua hiyo imechukuliwa  kufuatia ajali ya kichwa cha treni hiyo  kugongwa na lori jana Oktoba 2, 2013 saa 12:30 jioni katika makutano ya reli Buguruni. 

Ajali hiyo  imesababisha kuharibika kichwa cha treni na kuhitaji matengenezo kabla ya kuendelea na huduma. Uongozi wa TRL unaahidi kusimamia matengenezo kwa wakati ili huduma za treni za Jiji zirejee mapema kesho Ijumaa Oktoba 04, 2013. Kufuatia ajali hiyo hakuna mtu aliyejeruhiwa zaidi ya lori kupinduka na kuharibika kichwa cha treni.

Imetolewa na Afisi ya Uhusiano , 

Kwa niaba ya Mkurugenzi Mtendaji  
Mhandisi Kipallo Amani Kisamfu,
Dar es Salaam

Oktoba 03, 2013.