RAIS Jakaya Kikwete jana alipata wakati mgumu, baada ya kukutana na nguvu ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) jijini Mwanza katika ziara yake, huku Waziri wake wa Ujenzi, Dk. John Magufuli, naye akijikuta akizomewa mbele yake.
Mbunge wa Nyamagana, Ezekia Wenje, alivunja mwiko baada ya kujiunga katika msafara huo wa raia akiwa na gari lenye alama za Movement for Change (M4C) lililokuwa limefungwa bendera mbili za CHADEMA.
Hata hivyo maofisa usalama walipata wakati mgumu kulizuia gari hilo lisiwepo katika msafara huo, jambo lililozua tafrani kidogo katika uwanja wa Furahisha ambapo Kikwete alikuwa akihutubia mkutano wa hadhara.
Awali wakati wa uzinduzi wa wodi ya wazazi iliyoko eneo la Butimba, Rais alilazimika kumpa Wenje nafasi ya kuwasalimia wananchi baada ya Mkuu wa Mkoa, Evarist Ndikilo, kutaka kufanya hila ya kumnyima haki hiyo kama mbunge wa jimbo husika.
Baada ya viongozi wote kutambulishwa bila Wenje kutajwa, wananchi walianza kupaza sauti wakitaka mbunge wao naye atambulishwe.
Wenje baada ya kusimama alimshukuru Rais Kikwete kwa kumpa nafasi hiyo lakini akamwomba amvumilie kidogo atoe salamu maalumu ya wana Mwanza.
Kama kawaida ya CHADEMA kwenye salamu yao, Wenje aliwaomba wananchi wakunje ngumi kisha akawasalimu kwa kibwagizo cha peoples… nao wakamwitikia power!
Akiwa katika viwanja vya Furahisha ambapo Rais Kikwete alichelewa kuanza mkutano wake, Wenje alifika hapo na kushangiliwa kwa nguvu na wananchi huku polisi wakiwazuia bila mafanikio.
Ilipofika saa 12 jioni kabla Rais hajaingia uwanjani, wananchi hao walimtaka Wenje awahutubie huku wakidai bendera ya taifa ishushwe kwani muda wake ulikuwa umefika.
Kikwete aliingia uwanjani hapo saa 12:10 akiongozana na viongozi mbalimbali wa chama na serikali lakini wananchi hawakuonyesha kumshangilia badala yake walikuwa wakimwonyesha alama ya vidole viwili inayotumiwa na CHADEMA wakiimba ‘peoples…power’.
Katika hatua ya kushangaza wananchi hao walimshangilia kwa nguvu mbunge wa Ilemela, Highness Kiwia, aliyekuwa ameongozana na Rais huku wakiwazomea Meya wa Manispaa ya Ilemela, Henry Matata, ambaye hakufika kabisa mkutanoni hapo.
Matata alionekana mapema wakati Rais Kikwete akisomewa taarifa ya maendeleo makao makuu ya wilaya hiyo lakini hakufika uwanjani kabisa katika viti vya mbele alionekana naibu wake, Swila Dede.
Baadhi ya wananchi hao walisikika wakisema chini kwa chini kuwa Matata ni mwizi hawataki kumsikia lakini shangwe na nderemo zikajiri pale walipotambulishwa Wenje na Kiwia.
Rais Kikwete akiwa wilaya ya Ilemela, wananchi wengi waliokuwa wamesimama njiani walimwonyesha vidole viwili ikiwa ni alama CHADEMA.
Hata hivyo, hali hiyo ilionekana kumkera kiongozi huyo wa nchi pamoja na maofisa wa usalama, ambapo wana usalama wakiwemo polisi walionekana wakiwatisha na kuwazuia wananchi kunyoosha vidole viwili.
Magufuli azomewa
Waziri wa Ujenzi, Dk. Magufuli, alikumbana na jinamizi la kuzomewa mbele ya Rais baada ya kusimama jukwaani na kutaja jina la Matata, ambapo wananchi wengi walimzomea kwa miluzi huku wakimnyooshea vidole viwili.
Adha Magufuli alizomewa pia aliposema wabunge wa Ilemela na Nyamagana jijini hapa ni wana CHADEMA lakini ndani ya roho zao ni wana CCM.
Pia aliendelea kuzomewa aliposema kuwa iwapo Rais angehitaji kupokea kadi za CHADEMA zilizorudishwa angepokea nyingi.
“Mheshimiwa Rais, nampongeza Meya Matata (akazomewa), lakini pia wabunge wa Ilemela na Nyamagana wanachapa kazi vizuri, nje CHADEMA lakini ndani wao CCM (akazomewa).”
Akizungumza katika mkutano huo, Rais Kikwete alimpongeza mbunge wa Nyamagana kwa uchapakazi mzuri hasa kusimamia sekta ya elimu na kwamba wabunge wa namna hiyo wanastahili kuigwa.
Hata hivyo, alisema serikali yake imejipanga vizuri kuhakikisha usafiri wa reli, ndege, majini na barabara za lami vinaboreshwa maradufu kwa ajili ya maendeleo ya wananchi.
“Serikali yangu imeweka nguvu kubwa katika kuboresha sekta ya uchukuzi, ujenzi na nyinginezo. Hii ni kutaka kuwaletea wananchi wetu maendeleo ya kisekta,” alisema.
Baadhi ya mawaziri walioongozana na Rais mbali na Magufuli ni Naibu Waziri, Ofisi ya Makamu wa Rais, Charles Kitwanga, Waziri wa Kilimo, Chakula na Ushirika, Christopher Chiza, Waziri wa Maji, Prof. Jumanne Maghembe, Naibu Waziri wa Ujenzi na Dk. Charles Tizeba.