Tuesday, September 17, 2013

Watu 15 watiwa mbaroni kwa shambulio la tindikali


 
WATU 15 wanashikiliwa na polisi Zanzibar kwa tuhuma za kuhusika na matumizi haramu ya tindikali. Kukamatwa kwa watu hao kunatokana na tukio la mwishoni mwa wiki la kumwagiwa tindikali Padri wa Kanisa Katoliki Parokia ya Machui, Joseph Mwang’amba katika maeneo ya Mlandege mjini Zanzibar. Kamanda wa Polisi wa Mjini Magharibi Zanzibar, Mussa Ali Mussa hakutaka kutaja majina yao jana kwa vile uchunguzi unaendelea.

Alisema katika operesheni hiyo jeshi hilo linawahoji waliopata vibali vya kuwa na tindikali wamepewa na nani waweze kuwakamata na kuwafikisha katika vyombo vya sheria.

“Tunawaomba wananchi waendelee kutuunga mkono katika mapambano haya kwa kutupa taarifa za watu wanaojihusisha na uhalifu wa kutumia tindikali kwa kuwadhuru watu wengine.

“Mapambano dhidi ya jinamizi la tindikali ni makubwa na ni zaidi ya wengi wanavyofikiria. Tuvumiliane kwani upo uwezekano mkubwa wa mapambono haya kuwahusu jamaa zetu na wakati mwingine hata viongozi katika serikali,” alisema.

Alisema matukio yaliyopita ya kuwamwagia tindikali watu wasiokuwa na hatia ikiwamo kesi ya Sheikh Soraga, upelelezi wake umekamilika na jalada limefikishwa kwa mkurugenzi wa mashtaka kwa ushauriwa sheria.

Kamanda Mussa alisema suala la raia wawili wa Uingereza upelelezi wake upo hatua za mwisho.

Alisema jeshi la polisi kwa kushirikiana na ofisi ya mkemia mkuu na taasisi nyingine imeanzisha operesheni maalum yenye lengo la kupunguza matumizi holela ya tindikali nchini.

Kamanda alisisitiza kuwa operesheni hiyo itawalenga waingizaji tindikali nchini, wasambazaji, wauzaji na watumiaji holela.

Hata hivyo, alisema bado kuna changamoto kubwa kuhusu udhibiti wa moja kwa moja wa tindikali ikizimgatiwa inatumika katika viwanda na sehemu nyingine za mitambo