Mshambuliaji nyota wa zamani wa timu ya soka ya Simba na Taifa, Joseph
Kaniki ‘Golota’ na bondia Mkwanda Matumla wanashikiliwa Addis Ababa,
Ethiopia wakituhumiwa kusafirisha dawa za kulevya.
Kwa mujibu wa gazeti la Mwananchi Kaniki na Matumla walikamatwa Agosti
31, mwaka huu kwenye Uwanja wa Ndege wa Bole, Addis Ababa wakati
wakijiandaa kupanda ndege ya Shirika la Ndege la Ethiopia tayari kwa
safari ya kuelekea Paris, Ufaransa.
Kaimu Balozi wa Tanzania nchini Ethiopia, Samuel Shelukindo
alithibitisha jana kwamba wanamichezo hao wanashikiliwa nchini humo na
Polisi wa Kitengo cha Uchunguzi wa Makosa ya Jinai.
Wanamichezo hao wamepandishwa kizimbani katika Mahakamu Kuu ya Ethiopia
iliyoko kwenye eneo la Arada, Addis Ababa kujibu tuhuma za kubeba kilo
saba za dawa hizo haramu. Mkwanda anadaiwa kubeba kilo nne wakati Kaniki
akidaiwa kubeba kilo tatu. Kama watapatikana na hatia, wanaweza
kufungwa kifungo cha miaka tisa hadi 15.
Alisema uwezekano wa kesi ya Kaniki na Matumla kurudishwa Tanzania haupo
kwa kuwa nchi hizi mbili hazina utaratibu wa kubadilishana wafungwa.
“Wameshikiliwa hapa Ethiopia kwa zaidi ya siku 10 sasa, sisi tulipigiwa
simu na polisi wa hapa Alhamisi iliyopita kujulishwa kwamba kuna
Watanzania wawili wameshikiliwa kwa tuhuma za kukutwa na dawa za
kulevya, tulipokwenda tukamkuta ni Kaniki na Matumla,” alisema
Shelukindo.
“Wao wenyewe wanaeleza kwamba walipitia Mombasa na huo mzigo walipewa na
mtu mmoja. Lakini Kaniki yeye anajitetea kwamba huyo aliyewapa huo
mzigo pale Mombasa anajuana vizuri na Mkwanda. “Kwa hiyo alichofanya
yeye ni kuubeba tu. Walikuwa wapitie hapa Addis wakashuke Paris,
Ufaransa ndipo warudi Sweden kwa njia zao wanazojua wenyewe. Walipofika
hapa Mkwanda alifanikiwa kupenya akapanda ndege lakini Kaniki akanaswa
na mbwa ndipo akajitetea kwa polisi kwamba lile begi lilikuwa lake
lakini mizigo mingine ilikuwa ya Mkwanda.
“Ndipo hapo sasa Mkwanda akashushwa kwenye ndege wakashikiliwa na
Jumatatu ya wiki iliyopita wakapandishwa kwenye Mahakama ya hapa
kutajiwa kesi yao lakini hawakupewa nafasi ya kujitetea. Kesi itatajwa
tena Jumanne (leo) na Jumatano (kesho) na uchunguzi wa polisi bado
unaendelea.”
Wanamichezo hao walidai kwamba walikabidhiwa mizigo hiyo kwenye Uwanja
wa Ndege wa Mombasa walipokuwa wakikabidhiwa pasi za kupandia ndege
baada ya kupita sehemu zote za ukaguzi.
Kukamatwa kwa wanamichezo hao kumezidi kuongeza idadi ya Watanzania
maarufu waliotiwa mbaroni nje ya nchi katika siku za karibuni
wakituhimiwa kwa makosa hayo.