Baada
ya kuwa katika mapenzi na mwanaume huyo kwa zaidi ya miaka 17,
wakipendana na kuitana majina yote mazuri unayoyajua yakiwamo kuambiwa
‘mpenzi wangu nakupenda, nikinywa maji nakuona kwenye glasi’…leo mapenzi
yamegeuka shubiri.Kuna
mikasa mbalimbali huwatokea watu katika suala zima la mapenzi, kiasi
cha kusababisha baadhi yao kutopenda tena kuingia kwenye jambo hilo
wakiliona kama ni kitu kisichofaa, ingawa ukweli unaweza kuwa sio
huo.“Sitaki tena wanaume, ni watu wabaya, wameniumiza moyo wangu mno,”
anasema Hawa Francis, mkazi wa Ubungo, Dar es Salaam. Sababu kubwa ni
kero ambazo amewahi kuzipata katika suala zima la uhusiano. Vivyo hivyo
wapo wanaume hawataki kuoa, kwa maelezo kuwa kuna wanawake wamewahi
kuwatesa.
Kama wewe
ni kati ya watu ambao umekata tamaa na suala la uhusiano, fahamu kuwa
si wewe pekee.Kuna kundi kubwa la watu wameshatendewa kiasi cha kufanya
wasiwe na raha tena.
Mkasa wa mwanamke kukatwa mkono
Ilikuwa
Agosti 7, mwaka huu, saa mbili usiku. Ilikuwa ni siku iliyobadili
historia ya maisha yake. Baada ya kuwa katika mapenzi na mwanaume huyo
kwa zaidi ya miaka 17, wakipendana na kuitana majina yote mazuri
unayoyajua yakiwamo kuambiwa ‘mpenzi wangu nakupenda, nikinywa maji
nakuona kwenye glasi’…leo mapenzi yamegeuka shubiri.
Mwanamke
huyo, Mchali Kihiyo (35), mama wa watoto sita, aliyepoteza viungo vyake
kutokana na ukatili wa kijinsia uliofanywa na mwanaume ambaye wamekuwa
na uhusiano nae (jina limehifadhiwa).
“Uhusiano
wetu ulikuwa mzuri, hata hivyo kwa sasa naona mambo yamekuwa magumu
kwangu, leo hii mimi sina mkono wa kushoto na nimeondolewa sehemu ya
viungo vyangu vya upande mmoja,”anasema Mchali,akibubujikwa machozi
kutokana na ulemavu alioupata.
Chanzo cha ulemavu
Anasema
maisha yao ya uhusiano yalikuwa ya furaha kwa kipindi chote lakini
yamegeuka shubiri baada ya mwanamume wake huyo kuonyesha dalili ya
kutompenda kama awali, hali ambayo anaitafsiri kama labda alikuwa na
mwanamke mwingine.
Mchali,
anasema mikasa na mateso ilianza miaka mitatu iliyopita baada ya kuhisi
kwamba mwanamume wake huyo amezaa na mwanamke mwingine. Ubaya zaidi
ulimtokea baada ya mtoto wa huyo mwanamke mwingine, kutumbukia kwenye
kisima cha maji na kisha kupoteza maisha.
“Kifo
cha mtoto huyo, ndicho kilichozaa tatizo hili la ukatili dhidi yangu na
kunisababishia ulemavu, kwa kuwa huyo mwanaume wangu na huyo mwanamke
aliyezaa nae, walidai kwamba mimi ndiyo nilimtupia majini marehemu mtoto
wao ili afe,”anasema mama huyo.
Vitisho kabla ya ulemavu
Mchali,
anasema mara baada ya msiba wa mtoto kumalizika, mwanamume wake huyo
alihamia kwa mke mdogo lakini akawa anarejea nyumbani na kumtukana huku
akitishia kufanya lolote analofikiri linafaa.
Anasema
baada ya mateso na vitisho kuzidi aliamua kuondoka kwa mumewe huyo toka
mwezi Aprili mwaka huu na kuamua kurudi kwa wazazi wake huku akiwaacha
watoto wake kwenye nyumba waliyokuwa wakiishi.
Anasema
alilazimika kuwaacha watoto kutokana na agizo la mumewe, aliyekataa
asiwachukue, hivyo akaanza maisha mengine ya upweke bila watoto huku
akiendesha maisha yake kwa biashara ya kuuza samaki.
Anasema
mwanzoni mwa mwezi huu, aliugua malaria na kukaa nyumbani bila kwenda
kwenye biashara zake. Agosti saba mwaka huu, alipata nafuu na kuamua
kwenda kumsalimia kaka yake, anayeishi mbali kidogo na nyumbani kwao na
ndipo yakamkuta yaliyomkuta.
Anaeleza
kuwa alikaa kwa kaka yake hadi muda wa futari wakafuturu na kushangaa
simu yake ikiita, kuangalia ni namba ya mpenzi wake huyo. Alipoipokea,
aliulizwa aliko, yeye alimweleza yuko kwa kaka yake na kumtaka amfuate
mnadani akale nyama kitendo ambacho anasema alipingana nacho.
Anasema
baadaye aliamua kurudi nyumbani na kusindikizwa na wifi yake hadi
karibu na nyumba yao ikiwa ni saa mbili usiku.Walipoagana, ghafla
akashangaa kusikia sauti ya mumewe ikimuita, alipogeuka alimwona, kisha
akamuuliza alikotoka na kumwambia alikuwa kwa kaka yake.
Kipigo na ulemavu
Anasema
mara baada ya kumjibu mwanamume huyo alianza kumpiga na hatimaye
alianguka chini na mumewe akatoa panga na kuanza kumkatakata sehemu
mbalimbali za mwili wake.
Hakika
hujafa hujaumbika. Mchali amecharangwa kwa mapanga kuanzia chini ya goti
mguu wa kushoto hadi kwenye makalio, amekatwa sehemu zaidi ya saba
mwilini.
Ni kama alitaka kumkata shingo
Anasema
kwa namna anavyoona ni kama alidhamiria kumuua akisema kuwa mara nyingi
akiwa na huo upanga alikuwa analenga kumtenganisha shingo. Alichofanya
mama huyo ni kuweka mikono shingoni kuzuia panga, kitendo
kilichosababisha mkono wake wa kushoto kukatwa kabisa.
Hawezi kukaa
Mwandishi
wa makala haya baadaye alimwomba mwanamke huyo angalau akae chini,
kwani muda mwingi wa mahojiano alikuwa amelala, ndipo alipojibiwa kwamba
hawezi kukaa kwa vile kuna nyama kubwa kwenye makalio ambayo
imeshindikana kushonwa.
Mama huyo
anasema wakati mumewe akimcharanga mapanga, mama yake mzazi aliendelea
kupiga ngolo (yowe) kuomba msaada, kaka yake alikwenda lakini akashindwa
kutoa msaada kwa kuwa shemeji yake huyo alikuwa akimkimbiza na panga.
Anasema
kelele za mama yake zilisaidia kuokoa maisha yake, kwa kuwa majirani
walijitokeza, hivyo mwanamume huyo akaanza kuwakimbiza akitaka kuwadhuru
kitendo ambacho mama huyo aliona ndiyo nafasi pekee kukimbilia ndani.
Matibabu
Mchali,
anasema baadaye ndugu zake, walitafuta usafiri na kufanikiwa kupata
matibabu katika Hospitali ya Rufaa ya KCMC ambako alilazwa kwa siku nne
na kurejea nyumbani kutokana na ushauri wa daktari anayemhudumia.
Kwa
mujibu wa mama huyo, daktari anayemtibu alimtaka Mchali akubali kutibiwa
majeraha akiwa nyumbani ili kuepuka maambukizi ya magonjwa nyemelezi
pamoja na kuepuka gharama za matibabu.
“Sina
uwezo wa kukabiliana na gharama za matibabu kwa kuwa siwezi kutembea,
nalazimika kukodi gari na kwa wiki naoshwa mara tatu. Nisaidieni ndugu
zangu, ndoa yangu imenifikisha hapa,” anasema.
Mchali na hali ya ukatili mkoani Manyara
Kamanda
wa Polisi mkoa wa Manyara, Akili Mpwapwa anasema mtuhumiwa bado
hajakamatwa kwa vile hajulikani aliko, huku akiahidi kuendelea
kulifanyia kazi suala hilo.
Akielezea
zaidi ukatili mkoani Manyara, anasema upo, japo ni mdogo ikilinganishwa
na mikoa mingine. Anaamini kuwa bado changamoto ni kubwa kwa wanawake
ambao wengi wao wamekuwa wakinyanyasika.
Sababu
kubwa za kunyanyasika kwa wanawake ni mfumodume. Akasisitiza kuwa Jeshi
la Polisi mkoani humo linaendelea kuelimisha jamii madhara ya ukatili na
kusema jitihada hizo zinapaswa kuigwa na wananchi na asasi nyingine
kuhakikisha ukatili wa kijinsia unatokomezwa.