Saturday, September 14, 2013

Mbinu mpya za kusafirisha dawa za kulevya zabainika



Wakati vyombo vya sheria vikiendelea kupambana na biashara ya dawa za kulevya nchini, wasafirishaji hao kila siku wanaendelea kuwa wabunifu na kubuni mbinu mpya na za kutisha za kusafirisha dawa hizo kutoka eneo moja hadi lingine.
Imebainika kuwa miongoni mwa mbinu mpya wanazotumia ni kusafirisha dawa hizo kwa kutumia ndege za mizigo ambapo huweza kuweka dawa za kulevya kwenye mdoli, jarida, makopo ya maziwa ya watoto, vinyago vya kimakonde na kuutuma kama kifurushi kwenda sehemu nyingine.
Pia, wasafirishaji hao kwa sasa wanaweza kuvaa kama watawa (masista na mapadre) na kujifanya wameshika rozari zao wakisali na kumbe wamehifadhi dawa hizo ndani ya mavazi yao makubwa.
Pia, imebainika kuwa siku hizi si lazima kusafirisha dawa za kulevya zilizo tayari bali kemikali zinazotumika kutengeneza dawa za kulevya(kwa mfano amphetamine inayoweza kutengenezwa maabara), husafirishwa na baada ya kufika kemikali huchanganywa katika maabara za siri na dawa za kulevya huanza kusambazwa mitaani.
Kamishna Mkuu wa Polisi Kitengo cha Dawa za Kulevya, Alfred Nzowa alisema wasafirishaji hao wanabuni mbinu mpya kila kukicha lakini alitaja mbinu kuu ya kusafirisha mzigo mkubwa ni kwa njia ya meli au ndege za kukodi, za abiria au binafsi kupeleka mzigo kutoka nchi moja hadi nyingine.
“Dawa nyingi zinazosambazwa hapa zinakuja kwa njia ya meli. Zinapofika kwenye mipaka ya bahari ya nchi za Afrika Mashariki kama Mombasa na Dar es Salaam hupakuliwa na kuwekwa katika boti ndogo ndogo ziendazo kwa kasi na kusambazwa,” alisema Kamishna Nzowa.
Kwa mfano, ripoti ya mwaka 2013 ya Umoja wa Mataifa kitengo cha Uhalifu na Dawa za Kulevya (UNODC) inaeleza kuwa kwa sasa njia inayotumika kupitisha dawa za kulevya kufika Tanzania ni maeneo ya visiwani hasa Tanga na Zanzibar, ambapo wasafirishaji hutumia boti binafsi ndogo. Mzigo unaposhushwa hapa hupelekwa kama mizigo midogo midogo Dar es Salaam.
Nzowa alisema mbinu nyingine iliyobuniwa na inayotumiwa na wafanyabiashara wakubwa wa dawa za kulevya ni kusafirisha kwa kutumia ndege ndogo binafsi, ambazo huweza kupita bila kukaguliwa.
Nzowa alisema wasafirishaji hao wanaendelea kubuni mbinu nyingi kila siku ili kuwazidi ujanja wakaguzi walio katika viwanja vya ndege na katika mipaka, ambapo kwa sasa wasafirishaji wadogo wanaweza kuzificha katika soli za viatu, sehemu za siri au katika matiti.
“Tuliwahi kumkamata msichana mmoja wa Kifilipino ambaye kwa wakati mmoja alitumia mbinu tatu kuficha dawa aina ya heroin. Aliweka gramu 400 katika viatu, ambapo gramu 200 kiatu kimoja na gramu 200 katika kiatu cha kushoto. Alificha kiasi kingine kwenye matiti na kiasi kingine sehemu za siri,” alisema Nzowa.
Nzowa alisema wasafirishaji hao wanaendelea kubuni njia mpya kila siku, ambapo kwa sasa wamejikita zaidi kusafirisha kwa njia ya meli na ndege ili kuweza kusafirisha kiasi kikubwa bila kugundulika.
“Wale wasafirishaji wa ndani ya nchi wanatumia njia kama hizo za kumeza, lakini wale manguli wanatumia meli za kukodi na ndege binafsi. Wanaweza kusafirisha hata kilo 800 kwa wakati mmoja,” alisema Nzowa.
MWANANCHI: