Saturday, September 7, 2013

JK azindua shule, x-ray Mwanza





Rais Jakaya Mrisho Kikwete Mwanza. Rais Jakaya Kikwete amefungua shule ya kisasa ya msingi ya Ntulya Wilaya ya Misungwi, iliyotolewa zawadi kwa wanakijiji na taasisi kutoka Marekani.
Pia, Rais Kikwete amezindua huduma za x-ray kwenye Hospitali ya Wilaya ya Misungwi, siku yake ya kwanza ya ziara ya kikazi ya siku tano mkoani Mwanza.
Shule ya Ntulya iliyoko kilomita 47 kutoka mjini Misungwi, ina wanafunzi 466 na walimu 11 na ni zawadi ya Taasisi ya Africa School House ya Marekani kwa wanakijiji cha Ntulya ambako Mwanzilishi na Mkurugenzi wa taasisi hiyo, Dk Aimee Bessire ambaye amehudhuria sherehe za uzinduzi wa shule hiyo na mume wake, Mark Bessire walipata kuishi wakifanya utafiti kuhusu utamaduni wa Kabila la Wasukuma.
Shule hiyo ya kisasa imejengwa kwa matofali ya kuchomwa na ilijengwa kati ya 2008 na 2010. Ina madarasa 11, nyumba 10 za walimu na kisima cha maji safi. Kwa jumla shule hiyo ina uwezo wa kuwa na wanafunzi 600 kwa wakati mmoja.
Akizungumza kwenye sherehe hizo, Dk Bessire ambaye amezungumza kwa ufasaha lugha za Kiingereza, Kiswahili na Kisukuma, alisema kuwa shule hiyo imejengwa kwa jumla ya Sh1.038 bilioni, na kati ya hizo Sh980 milioni zilitolewa na Africa School House, Halmashauri ya Misungwi ilichangia Sh28 milioni na nguvu za wananchi zilichangia Sh30 milioni.
Taasisi hiyo ya Marekani pia imewajengea wanakijiji hao wa Ntulya, Kituo cha Afya kwenye eneo hilo la shule na Dk Bessire alisema kuwa taasisi hiyo ina mipango ya kujenga shule ya mfano ya sekondari ya bweni ya wasichana.
Dk Bessire pia alisema kuwa yataanzishwa madarasa kwenye shule hiyo kwa ajili ya watu wazima wasiojua kusoma na kuandika.