SERIKALI imetoa takwimu za mahabusi waliohukumiwa kwa kesi ya dawa za
kulevya ambapo takwimu hiyo inaonyesha jumla ya watu 10 wamehukumiwa kwa
kipindi cha mwaka 2010,2012.
Hayo yamesemwa na Msemaji Mkuu wa Serikali ambaye ni Mkurugenzi wa Idara
ya Habari Maelezo Assah Mwambene leo jijini Dar es salaam alipokuwa
akizungumza na waandishi wa habari katika ukumbi wa Idara hiyo.
Alisema kuwa jumla ya washitakiwa wanne walihukumiwa kifungo cha maisha
jela Mahakama Kuu mkoani Mtwara baada ya kupatikana na hatia ya kukutwa
na kilo nne za dawa za kulevya aina ya heroin Mwaka 2010.
Mwaka 2012 Mahakama Kuu Mkoani Tanga iliwahukumu washitakiwa 5 kifungo
cha miaka 25 jela na kulipa faini ya TSh. 1,438,364,000/= kila mmoja
baada ya kupatikana na hatia ya kusafirisha kilo 92.2 za dawa za kulevya
aina ya heroin. Pamoja na hukumu hiyo, mahakama iliamuru utaifishaji wa
magari mawili yaliyotumiwa kusafirisha dawa hizo.
Mwaka 2012 Mahakama Kuu ilitoa hukumu ya miaka 20 jela kwa mshtakiwa
mmoja aliyekamatwa na kilo 3 za dawa za kulevya aina ya heroin mkoani
Kilimanjaro. Aliongezea kuwa “Kwa yeyote aliyekuwa anafikiria kufanya
biashara ya dawa za kulevya ajue muda wake umekwisha” alisema Mwambene.
Mwambene alisema kuwa tatizo hili litakuwa historia kwani ulinzi
umeimarishwa, hivyo ametoa rai kwamtu yeyote mwenye nia ya kufanya
biashara hiyo aache mara moja. Mkurugenzi huyo alisisitiza kuwa Serikali
imeweka jitihada kubwa ya kutoa elimu kwa watumiaji na waathirika wa
dawa za kuelevya ili waweze kubadili tabia zao za kutumia dawa hizo na
kuwa watu wema katika jamii