Imezoeleka kwa raia wa kawaida kupekuliwa kwenye maeneo ya usafiri ili kuhakikiwa wasije kusafiri na vitu vya hatari ikiwemo silaha na madawa ya kulevya, huku viongozi wakipita ‘free’ lakini sasa Waziri wa Uchukuzi, Dk. Harrison Mwakyembe amebadili kibao.
Mwakyembe amebadili kibao hicho katika kipindi ambacho kuna tuhuma kwamba miongoni mwa waheshimiwa wanaounda Baraza la Mawaziri linaloongozwa na Rais Jakaya Kikwete ‘JK’, wapo wenye tabia ya kujihusisha na biashara ya madawa ya kulevya.
Kibao cha sasa kinasomeka kwamba ni zamu ya mawaziri wa JK wanaotajwa kujihusisha na uuzaji wa unga, kwa hiyo watakapokuwa wanasafiri kwenda kokote, iwe ndani au nje, lazima wakaguliwe na wakikutwa na ‘mzigo’ wataumbuka.
Tafsiri ya agizo la Mwakyembe alilolitoa wiki iliyopita kuwa viongozi wote watakuwa wanakaguliwa hususan watakapokuwa wanasafiri kupitia Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNIA), limetafsiriwa na wajuzi wa mambo kwamba alilitoa kisayansi ya intelijensia.
“Kama Mwakyembe angesema mawaziri wanaotuhumiwa wakaguliwe, ingeleta picha mbaya na asingekamatwa mtu. Ameagiza viongozi wote wakaguliwe ili kuweka usawa. Alitumia akilia sana katika tamko lake,” alisema mwanaharakati wa madawa ya kulevya nchini, Mbena Nyiboma.
Mwakyembe alisema, ili kuhakikisha ‘uhuni’ wa kusafirisha madawa ya kulevya unakoma, viongozi wote watakaguliwa, isipokuwa Rais, Makamu wa Rais, Waziri Mkuu, Spika wa Bunge na Jaji Mkuu. KILIO KUHUSU MAWAZIRI WA JK
Mawaziri, wabunge, mabalozi na viongozi wengine wa kitaifa, wana hati za kusafiria za kidiplomasia (Diplomatic Passport), kwa hiyo hupita katika milango ya watu mashuhuri (VIP) bila kukaguliwa.
Kutokana na hali hiyo, zipo tuhuma za muda mrefu kwamba baadhi ya mawaziri, mabalozi hata wabunge, wamekuwa wakitumia fursa hiyo vibaya kwa kusafirisha au kutumiwa kusafirisha madawa ya kulevya katika mabegi na ‘briefcase’ zao.
Taarifa za mitandao ya kijamii zilianza muda mrefu, baadhi ya mawaziri, wabunge na wafanyabiashara wenye heshima kubwa nchini, wakitajwa waziwazi kwa majina kuwa wanatumia ‘u-VIP’ wao vibaya, kusafiri na madawa ya kulevya katika mabegi yao.
Hivi karibuni, zipo barua (japo uhalali wake bado ni kitendawili) ambazo inadaiwa kuandikwa na wafungwa wa kesi za madawa ya kulevya Hong Kong, China, zilizoelekezwa kwa JK, zikitaja vigogo wa biashara hiyo haramu na miongoni mwa watajwa wamo mawaziri na wabunge. MBUNGE ALIVYOWAWASHIA MOTO MAWAZIRI
Katika vikao vya Buge la Bajeti 2013-2014, mwaka huu, Mbunge wa Mwibara (CCM), Kangi Ligora, aliwawashia moto mawaziri wa JK, akidai kwamba baadhi yao ni wauzaji wakubwa wa madawa ya kulevya.
Bila kumung’unya maneno, Kangi alisema kuwa tatizo hilo ni kikwazo kwa maendeleo ya uchumi wa taifa na akataka mawaziri wauza unga wadhibitiwe kwa usalama wa nchi.
Kangi, aliyasema hayo wakati akichangia mjadala wa hotuba ya bajeti ya Ofisi ya Waziri Mkuu kwa mwaka wa fedha 2013/2014 na akataka Kamishna wa Madawa ya Kulevya nchini naye awajibishwe kwa sababu ameonesha udhaifu wa kimapambano dhidi ya wauza unga.
Aliongeza kuwa serikali inawajua wauzaji wakubwa wa madawa ya kulevya, lakini inashindwa kuwakamata na kuwafikisha mahakamani kwa sababu ya rushwa, kwani watendaji wengi wanahongeka.
WAZIRI MKUU AKATOA KAULI YAKE
Kufuatia hoja ya Kangi, Mbunge wa Tumbe (Cuf), Rashid Abdallah, alimuuliza Waziri Mkuu, Mizengo Pinda, swali la papo kwa papo, akimtaka atoe ufafanuzi kuhusu tuhuma za mawaziri kujihusisha na baishara ya madawa ya kulevya.
Pinda, akimjibu Rashid, alikanusha tuhuma hizo, zaidi alimwomba Spika Makinda amtake Kangi ataje mawaziri wanaofanya biashara hiyo haramu.
MWAKYEMBE AMETHUBUTU
Uamuzi wa Mwakyembe, umejikita katika kukata mzizi wa fitina kuhusu usafirishaji wa madawa ya kulevya nchini.
Kwa jumla, taifa limekuwa likipakwa matope kutokana na uzembe wa udhibiti wa usafirishwaji wa madawa ya kulevya hususan JNIA, matokeo yake watu wanakamatwa nje ya nchi na kuifanya Tanzania ionekane ni nchi inayokumbatia biashara hiyo.
Takriban miezi miwili iliyopita, wasichana wawili Watanzania, Agnes Gerald ‘Masogange’ na Melisa Edward, walikamatwa katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Oliver Tambo, Afrika Kusini wakiwa na kilo 150 za madawa ya kulevya aina ya Crystal Methamphetamine yenye thamani ya Shilingi bilioni 6.8.
Kitendawili cha namna shehena hiyo kubwa ya madawa ilivyoweza kupita JNIA bila kugundulika na mamlaka husika, kiliteguliwa na Mwakyembe hivi karibuni, alipotaja watumishi wa Mamlaka ya Uwanja wa Ndege, waliohusika kusaidia kusafirisha mzigo huo kama walivyorekodiwa na Mfumo wa Kamera za Usalama (CCTV).
Baada ya kutegua kitendawili hicho, Mwakyembe amegeukia viongozi kwamba nao wakaguliwe ili kufanikisha mapambano ya jumla ya biashara ya madawa ya kulevya.