Watoto wakicheza pembezoni mwa Ziwa Victoria.
Picha hii inaonesha mfereji (kulia) unaotoka Soko Kuu la Mji wa
Bukoba ukiwa umebeba vinyesi kutoka maeneo mbalimbali likiwemo Gereza la
Bukoba, Uchafu unaotoka katika gereza hilo hupitia Shule ya Msingi Rumuli kabla
ya kuungana na mfereji huo ambao hukutana na Mto Kanoni, kama inavyoonekana
pichani.
Na Mwandishi Wetu
"Kwa kweli hakuna moyo wa
uzalendo katika suala la kutunza mazingira ya Ziwa Victoria, kama leo hii
ukiwauliza Magereza taka ngumu na kinyesi wanamwaga wapi, huwezi kupata jibu,
wanarukaruka tu,” Magongo- Mfuatiliaji na Mtathmini Mradi wa KADETFU
SERIKALI imeweka sheria mbalimbali zinazolenga kutunza mazingira
ikiwemo Sheria ya Mazingira Namba 20 ya mwaka 2004
.Pia mwaka 2009, Serikali ilipitisha Sheria Namba 11 ya rasilimali
za maji na Sheria Namba 12 ya Huduma za Maji na Usafi wa Mazingira ambazo kwa
pamoja zinalenga kulinda na kutunza nyanzo vya maji
.Sheria hizi zinatoa adhabu, mfano katika kifungu cha 52(1) cha Sheria Namba 12 ya Huduma za Maji na Usafi wa Mazingira, kinatoa faini ya kiwango cha shilingi milioni moja au kifungo cha miezi 12 au vyote kwa pamoja kwa mtu yeyote atakayesababisha uchafuzi wa chanzo cha maji.
.Sheria hizi zinatoa adhabu, mfano katika kifungu cha 52(1) cha Sheria Namba 12 ya Huduma za Maji na Usafi wa Mazingira, kinatoa faini ya kiwango cha shilingi milioni moja au kifungo cha miezi 12 au vyote kwa pamoja kwa mtu yeyote atakayesababisha uchafuzi wa chanzo cha maji.
Hata hivyo, licha ya kuwepo sheria hizo bado kumekuwa na uchafuzi
mkubwa wa mazingira katika Bonde la Ziwa Victoria unaofanywa na wananchi,
viwanda, mahoteli pamoja na taasisi mbalimbali za serikali na zile zisizo za
Kiserikali.
Jeshi la Magereza mjini Bukoba Mkoa wa Kagera ni miongoni mwa
taasisi za umma ambazo kwa kiasi kikubwa zinadaiwa huwa zinahusika katika
kuchangia kuchafua mazingira ya Ziwa Victoria kupitia utiririshaji wa vinyesi
katika Ziwa Victoria.
Kupitia gereza lililopo Bukoba Mjini, uchunguzi umebainisha kuwa,
gereza hilo limekuwa likitapisha kinyesi kwenye mtaro unaotoka katika gereza
hilo, ambao unapita nyuma ya mfereji unaokatiza katika Kanisa la Kisabato la
Seventh Day Adventist kuja Barabara ya Uganda iliyopo Mtaa wa Rumuli.
Kinyesi hicho, huwa kinaingia katika mfereji unaotoka katika Shule
ya Msingi Rumuli kupitia Soko Kuu na kuungana na Mto Kanoni ambao unapeleka
moja kwa moja taka hizo ziwani.
Katika uchunguzi uliofanywa na Majira katika mfereji unaotoka
Shule ya Msingi Rumuli na kuungana na mfereji unaotoka gerezani ni kama mita
200 hadi 300 kuingia ziwani kupitia mto Kanoni ambapo umebainisha utiririshaji
wa vinyesi ovyo.
Uchunguzi huo ulikuwa ni mwendelezo wa kuangalia uchafuzi wa
mazingira Ziwa Victoria unaofanywa na Jeshi la Magereza kwa kumwaga vinyesi vya
wafungwa na ongezeko la magugu maji ziwani humo.
Ambapo katika makutano ya mfereji wa Rumuli na gereza, eneo hilo
la makutano hayo kumezibwa ili kusiweze kuonekana kwa urahisi wakati wa
kutemesha kinyesi hicho.
Gazeti hili liliweza kufanya uchunguzi na kujionea mtaro ambao uko
pembezoni mwa Barabara ya Uganda unaotokea gerezani karibu na Kanisa hilo,
ambao ulikuwa ukitiririsha na umejaa maji taka ambayo yalikuwa yakitoa harufu
kali, ambayo unaweza kuifananisha na mzoga wa mnyama aliyekufa kwa muda katika
maeneo hayo.
Baada ya kugundua hali hiyo gazeti hili liliweza kufanya mahojiano
na baadhi ya wananchi wakiwemo wadau wa mazingira wa maeneo hayo, ambao nao
walionesha kuguswa na tatizo hilo.
Tatizo ambalo wanasema linafanya hali ya hewa kuwa mbaya wakati wa
masika, ambapo gereza hilo hutumia mwanya huo kutapisha kinyesi hicho jambo
ambalo linaleta usumbufu mkubwa kwa wakazi hao.
WANANCHI WANENA
Mmoja wa waumini wanaosali katika Kanisa la Wasabato la Seventh
Day Adventist ambaye alijitambulisha kwa jina la Editha Rweyimamu anasema,
harufu mbaya inayotoka gerezani hapo hasa wakati wa mvua imekuwa ikisababisha
waumini kushindwa kupata usikivu wa neno la Mungu pindi wanapokuwa kwenye
ibada.
“Wakati huu wa kiangazi hali kidogo huwa shwari (nzuri), lakini
maji taka hayo huwa wanatiririsha kidogo sana ila wakati wa mvua unashindwa
hata kutafakari hii harufu ni ya kitu gani, kwa maana harufu huwa ni nzito na
inaenea kanisa zima,” alisema Rweyimamu.
Naye Jumanne Issa ambaye anajihusisha na biashara ya kuuza vitabu
kwenye eneo hilo kwa miezi nane sasa anasema, amekuwa akishuhudia harufu ya
vinyesi kutoka katika mfereji unaotoka gerezani, huku kila mtu anayepita karibu
na mfereji huo akilazimika kufunga pua.
Wakati mwananchi huyo akisema hivyo, mwandishi wa makala haya
alifanikiwa kupita kila eneo ambalo linazunguka Gereza na kushuhudia maji taka
hayo yakitiririka kutoka mfereji wa Gereza kupitia Barabara ya Uganda, ambayo
yanakutana na mfereji wa Shule ya Msingi Rumuli na kuingia Mto Kanoni, ambao
unapeleka maji moja kwa moja ziwani.
“Harufu inatuathiri sana, tunashangaa kuona serikali imelifumbia
macho, tunaomba watafute njia ya kumwaga kinyesi hicho sio kupeleka ziwani
mahali ambapo tunapata chakula na maji ya kunywa,” alisema muuza vitabu huyo.
WADAU WA MAZINGIRA
Wakizungumzia suala hilo kwa nyakati tofauti, wadau wa mazingira
katika Manispaa ya Bukoba nao walisema kuwa, gereza hilo limekuwa likitiririsha
kinyesi mwaka mzima mfululizo na kuingiza Mto Kanoni ambao unapeleka maji
ziwani.
Michael Cleophans ambaye ni katibu mkuu wa taasisi
inayojishughulisha na masuala ya mazingira ya Envirocoment mjini Bukoba
anasema, gereza hilo limekuwa likitiririsha kinyesi kupitia mfumo ambao si
rasmi wa kunyonya vyoo vilivyotitia, yakiwemo maji taka kutoka kwenye vyumba
vya wafanyakazi na kuyatiririsha kwenye mfereji kupitia kanisa hilo la
Wasabato.
Anasema, suala hilo wamekuwa wakilijadili mara kwa mara katika
vikao vyao vya mazingira, lakini limekuwa likichukuliwa sana kisiasa.
“Kutokana na vitisho vikali kutoka kwao (gereza), watu wamekata
tamaa na taasisi zingine za kiserikali zinazoshughulika na mazingira, walisema
watalifuatilia, lakini hadi leo (mwishoni mwa wiki) zimeendelea kuwa kimya,”
anasema mdau huyo.
Aidha, anasema kuwa pamoja na kwamba hakuna miundombinu ya mfumo
wa maji taka katika Manispaa ya Bukoba isiwe sababu ya wao kukwepa gharama za
kulipia magari ya kunyonya maji taka hayo na kuyapeleka kumwaga katika eneo
ambalo limetengwa na Manispaa kwa ajili hiyo.
Naye Justus Magongo ambaye ni Mfuatiliaji na Mtathmini Mradi
katika Shirika la Maendeleo Kagera (KADETFU) anasema kuwa, taasisi nyingi
katika Manispaa ya Bukoba ikiwemo Magereza zinahusika katika uchafuzi wa
mazingira kutokana na ukosefu wa miundombinu.
Anasema kuwa, wao kama taasisi isiyo ya kiserikali wanafanya kazi
pale ambapo serikali haiwezi kufika.
“Tumeweza kufanya semina kwa viongozi wa taasisi mbalimbali na
Magereza wakiwemo, ili kutoa hamasa katika kupunguza tatizo hili, lakini cha
ajabu hakuna utekelezaji wowote uliofanyika.
“Kwa kweli hakuna moyo wa uzalendo katika suala la kutunza
mazingira ya Ziwa Victoria, kama leo hii ukiwauliza Magereza taka ngumu na
kinyesi wanamwaga wapi huwezi kupata jibu wanaruka ruka tu,” anasema Magongo.
MRADI WA LVEMP II
Mratibu wa Mradi wa Ziwa Victoria Awamu ya Pili (LVEMPII) Manispaa
ya Bukoba, Richard Salu alikiri kufahamu kuwa kuna mtaro unaotoka Magereza
kuingia Mto Kanoni unaotiririsha uchafu ingawa bado hawajajua ni uchafu wa
kiasi gani ambao unaingizwa ziwani.
“Nafahamu sana, ila hiki ni kituo cha serikali, hivyo pindi
itakapobainika tutakaa nao meza moja ili kuwashauri maji taka hayo yaweze
kutibiwa kabla hayajaingia ziwani au waunganishe kwenye mfumo wa maji taka wa
manispaa ambao bado haujajengwa,” anasema Salu.
Hata hivyo, uchunguzi wa gazeti hili ulibainisha kuwa licha ya
kutokuwepo kwa mfumo wa maji taka katika mji wa Bukoba mkoani Kagera, Manispaa
imetenga eneo la Nyanga nje kidogo ya mji huo kwa ajili ya kumwaga huo uchafu,
lakini watu wamekuwa hawatumii, badala yake wamekuwa wakisubiria mvua ikinyesha
waruhusu kinyesi hicho kiweze kutapishwa.
OFISA MAZINGIRA BUKOBA
Ofisa Mazingira katika Manispaa ya Bukoba , Hamza Kambuga
alipohojiwa kuhusiana na suala hilo alikiri Magereza kutapisha kinyesi, japo
kuwa wana makaro ya maji taka ambayo yanadaiwa huwa yanazidiwa kutokana na
kuwepo kwa idadi kubwa ya wafungwa.
Anasema kuwa, wakati gereza linajengwa (mwaka 1937) lilikadiriwa
kuwa na wafungwa wachache ( wafungwa 360) hivyo gereza lilikuwa dogo.
Kwa kuwa, wakati huo ilikuwa ni ngumu kujenga mfumo wa maji taka
mkubwa wa kiasi hicho kama inavyohitajika hivi sasa, hivyo tangu wakati huo
mfumo wa gereza haujapanuliwa na miundombinu iko vilevile na wafungwa wakizidi
kuongezeka.
Anasema kuwa, tatizo hilo wanaliona lakini changamoto yake ni
kubwa hali hiyo inaweza kutatuliwa endapo mfumo wa maji taka utajengwa ambapo
wataweza kuunganisha moja kwa moja.
Hata hivyo, Kamishna Msaidizi wa gereza hilo, ACP Nkonjelwa
alipohojiwa na mwandishi wa makala hii juu ya idadi ya lini gereza hilo
lilianzishwa na idadi ya wafungwa kipindi hicho hadi leo alisema kwa kifupi; “
lilianzishwa mwaka 1937, likiwa na uwezo wa kuchukua wafungwa 360, kwa sasa
hivi wapo 437 ambapo wafungwa ni 213 na mahabusu 224,” alisema ACP huyo.
MAABARA BUKOBA
Gazeti hili liliweza kuonana na Mkuu wa Maabara katika Manispaa ya
Bukoba, Marco Vitta ambaye alithibitisha kuwa, gereza hilo limekuwa likihusika
katika utapishaji wa kinyesi hicho ziwani (kupitia maeneo ambayo yametajwa hapo
juu).
Anasema kuwa, kwenye kipindi cha mvua maji taka hayo yanakuwa
hayaonekani moja kwa moja kutokana na kinyesi hicho kuchukuliwa na maji moja
kwa moja ila wakati wa kiangazi hali inakuwa ni mbaya zaidi, vinyesi vinakuwa
vinatapakaa.
Anasema kuwa, mwanzoni hali hiyo haikuwa mbaya sana katika kipindi
cha nyuma kutokana na Magereza kutokuwa na wafungwa wengi, lakini hali imekuja
kubadilika hivi karibuni katika miaka ya 2000 hali hii inaonesha kuwa gerezani
kuna msongamano wa wafungwa.
“Huenda hapo awali katika kipindi cha nyuma, Magereza ilikuwa
ikitapisha kwa mwaka mara moja kutokana na idadi ndogo ya wafungwa waliokuwepo
(360), lakini hivi sasa kutokana na wingi wa wafungwa unakuta ‘septic’ (mfumo
wa maji taka) zinajaa ndani ya miezi mitatu hadi nne hivyo wanachofanya ni
kutapisha kinyesi,” anasema Vitta.
Anaongeza kuwa, suala hili la gereza kutapisha kinyesi ziwani limekuwa
ni gumu kupatiwa ufumbuzi kutokana na kwamba hiyo ni taasisi ya kiserikali.
“Hivyo ni jukumu la serikali kulitafutia suluhu japo hili, vipimo
vya kimaabara vinavyofanyika kila mara kwa maabara kuchukua sampuli za majitaka
hayo kutoka Magereza zinaonesha maji taka yanayotiririshwa kutoka kwao ni
kinyesi kitupu,” anasema Mtaalamu huyo.
MKUU WA MAGEREZA
Gazeti hili lilimtafuta Mkuu wa Magereza Mkoa wa Kagera (RPO)
ambaye pia ni Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Magereza Mkoa wa Kagera, Yusuph
Kimanji (amestaafu tangu Julai Mosi, mwaka huu) ili aelezee suala hili kwa
upana zaidi.
Mkuu huyo, alidai kuwa Manispaa ya Bukoba imekuwa ikishindwa
kuweka mkakati wa muda mfupi na mrefu wa jinsi gani ya kuwa na mfumo wa maji
mjini Bukoba.
“Jambo hili (kutiririsha vinyesi ziwani) si kweli, wanaisema
Magereza kwa sababu wanaichukia taasisi hii, lakini ukweli ni kwamba maji taka
katika majengo yote Bukoba yanapita katika Mto Kanoni na kuingia ziwani,”
anasema Mkuu huyo wa gereza.
Alipoulizwa kuhusiana na maji taka yanayotiririka kutoka kwenye
gereza hilo, alikana na kusema kuwa wao hawahusiki na utiririshaji wa maji
taka.
“Kama tungefanya hivyo, tusingehusika katika kuombea fedha suala
la kunyonya maji taka toka serikalini.
“Tangu nimeingia katika ofisi hii mwaka 2007, mwezi Julai niliona
kuna matatizo ya mfumo wa maji taka, katika mji wa Bukoba na ndio maana
niliamua kuweka utaratibu wa kuombea fedha jambo hili,” anasema Kimanji.
Hata hivyo, alimuonesha mwandishi wa makala hizi nyaraka ambazo
zinazoonesha fedha walizoomba katika kupindi cha mwaka 2010/2011 ambapo
walipokea sh. milioni 6.5.
Mwaka 2011/2012 zilikuwa ni sh. milioni 7.1 ambazo zote zilikuwa
kwa ajili ya kunyonya maji taka kutoka katika maeneo ya Magereza na mwaka
2012/2013 walipokea sh. milioni 5.6.
Fedha ambazo zilikuwa kwa ajili ya kukarabati mfumo wa maji taka
ambao bado wanautekeleza ili kuhakikisha kuwa hakuna maji yanayopotea na kwenda
kuzagaa nje.
Alipoulizwa kuhusiana na hali aliyoikuta wakati anakabidhiwa gereza
hilo, Mkuu huyo alikataa kuzungumza na kudai kwamba hawezi kuongelea masuala ya
nyuma kwani kwa wakati huo hakuwepo na hawezi kujua kilichokuwa kinaendelea.
“Sitaki kuongelea suala hilo, ila anayestahili kubeba lawama ni
manispaa, kwa nini haina nfumo wa maji taka na pia haina magari ya kunyonya
maji taka na badala yake tunaenda kukodi magari ya watu binafsi,” anasema
Kimanji.
Katika kuthibitisha kauli yake kuwa, hawamwagi kinyesi ziwani
kupitia Mto Kanoni, gazeti hili liliamua kuwatafuta madereva waliopewa dhamana
na Manispaa ya Bukoba ya kunyonya maji taka katika mji huo ili waweze
kuthibitisha kama huwa wanatumiwa na taasisi hiyo ya Magereza ili kunyonya maji
taka na vinyesi.
Lengo ni kutaka kujua kama ni kweli Magereza hawahusiki au katika
uchafuzi wa ziwa na pia kuhakikisha kama kweli fedha ambazo wanaletewa na
serikali kwa ajili ya kunyonya maji taka kama zinatumika ipasavyo kama
alivyosema.
SAUTI ZA MADEREVA
Miongoni mwa madereva ambaye hakutaka kutaja jina lake na kampuni
anayoiwakilisha gazetini kwa kuhofia kupoteza wateja wake alimweleza mwandishi
kuwa, taasisi hiyo ya Magereza huwa inawakodi kunyonya maji taka kwa mwaka mara
moja.
“Ni kutoka katika makaro ya magereza hiyo,” anasema Dereva huyo.
Anasema kuwa, mara ya mwisho kukodiwa na magereza ilikuwa ni
Oktoba, mwaka jana hadi leo hii hawajawahi kukodiwa.
Pia Dereva huyo anasema kuwa, pindi wanapokodiwa huwa wanapewa
mkataba wa kubeba awamu 10 ambapo wao wanachaji kila moja sh. 120,000.
Anasema kuwa, maji taka hayo huwa wanayanyonya katika makaro
matano yaliyopo katika gereza hilo na pindi wanapokuwa wananyonya huwa
wanapunguza punguza kutoka katika karo moja na huwa hawatoi yote ili
kuhakikisha tripu 10 zinatimia na mengine yanayobaki wakati wa mvua Magereza
wenyewe huwa wanatapisha katika mtaro, kwa kutumia ndoo ambapo kazi hiyo
hufanywa na wafungwa.
“Mwaka huu tangu uanze hatujawahi kukodiwa na Magereza, mara ya
mwisho wametukodi mwaka jana mwezi Oktoba na huwa wanatukodi mara moja kwa
mwaka ambapo huwa wanatupa mkataba wa tripu 10 tu, ambazo huwa tunapunguza
punguza kutoka katika makaro ya gereza hilo,” anasema Dereva huyo.
Kutokana na maelezo ya dereva huyo anasema kuwa, kila tripu moja
huwa wanatoza sh. 120,000 hivyo kwa tripu 10 ni sawa na shilingi milioni 1.2
ndizo ambazo zinatumika kutoka katika fedha ambazo Mkuu wa Magereza Bukoba
alizitaja.
Kwa kuwa, wanapatiwa kutoka serikalini kila mwaka jambo ambalo
linaonesha kuwa hazitoshelezi katika kukidhi mahitaji ya unyonyaji taka na yale
yanayobaki kwenye septank yanasubiri kutapishwa wakati wa mvua kama
ilivyothibitishwa na dereva huyo.
WAHUSIKA NA WALINZI ZIWANI
Mratibu wa Mradi wa Mazingira wa Ziwa Victoria Awamu ya Pili
(LVEMPII), Omary Mwamuyanza anasema kuwa ni kweli Magereza huwa wanamwaga
kinyesi cha wafungwa ziwani japo si peke yao wako wengi.
Anasema kuwa, wao kama mradi wa Hifadhi ya Mazingira ya Ziwa
Victoria pamoja na kujua kuwa Magereza na taasisi nyingine zinachafua mazingira
hawana mamlaka ya kuwachukulia hatua bali huwa wanawaeleza manispaa ili
watekeleze suala hilo.
“ S i s i h a t u n a s h e r i a y a kuwachukulia hatua ila watu
kama NEMC (Baraza la Mazingira nchini) na Manispaa ndizo ambazo zinatakiwa
kutusaidia katika suala zima la kuwachukulia hatua, sisi tunasaidia katika
kutekeleza mradi ikiwa ni pamoja na kujenga mfumo wa maji taka katika mji huo
ambao utagharimu zaidi ya dola milioni1.5, ambao utakamilika ndani ya miezi 18
ijayo,” anasema Mwamuyanza.
Anasema kuwa, uchafuzi wa mazingira ya Ziwa Victoria bado ni
changamoto kubwa kwani wananchi pamoja na taasisi nyingi hawako tayari kubadili
tabia za kutiririsha vinyesi ziwani hadi inawalazimu mara kwa mara kuwaelimisha
na mradi unatumia gharama nyingi, lakini hawako tayari kupokea ushauri.
MSIMAMO WA NEMC
Gazeti hili lilimtafuta Mratibu wa Kanda ya Ziwa katika Baraza la
Taifa la Usimamizi wa Mazingira (NEMC), Anna Mdamo ambaye ofisi zake zipo
jijini Mwanza ili aweze kujibu ni kwa nini Gereza la Bukoba limekuwa likichafua
ziwa kwa kumwaga kinyesi cha wafungwa ziwani na sheria za kulinda mazingira
zikiwepo.
Mdamo alisema kuwa, wao kama kanda hawajathibitisha kama Magereza
wanachafua ziwa alisema kuwa, mtu anayetakiwa kuthibitisha kuwa Magereza
wanachafua ziwa kwa kumwaga kinyesi ziwani ni Ofisa Mazingira wa Manispaa ya
Bukoba.
“Sina taarifa zozote kuhusiana na gereza kutiririsha kinyesi
ziwani, hatujafanyia kazi na wala hatujaletewa malalamiko, ila pindi
tutakapoambiwa na kuthibitisha kuwa wanahusika katika suala zima la uchafuzi wa
mazingira tutaenda kuonana nao na kuwachukulia hatua,” aliongeza.
Uchunguzi unaonesha kuwa, uchafuzi wa mazingira ndani ya Ziwa
Victoria unaofanywa na wananchi zikiwemo taasisi mbalimbali za serikali hasa
Gereza la Bukoba kwa kutirisha kinyesi ziwani ni tatizo ambalo linaathiri
watumiaji wa ziwa pamoja na viumbe hai kwa ujumla.
Inakadiriwa kuwa, ziwa hilo linategemewa na wakazi zaidi ya
milioni 35 kutoka nchi za Kenya, Uganda, Tanzania, Rwanda na Burundi ambapo
ziwa hilo lina ukubwa wa mita za mraba 194,000 huku Tanzania ikimiliki asilimia
44 ya eneo lake lote