Naibu Spika wa Bunge, Job Ndugai, akizungumza na waandishi wa habari
mjini Bagamoyo Mkoa wa Pwani jana, wakati wa kufunga mafunzo kwa kamati
ya Bajeti , PAC na LAAC mafunzo yaliyoendeshwa na Ofisi ya Mdhibiti na
Mkaguzi Mkuu wa Fedha za Serikali. Kushoto ni Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu
wa Fedha za Serikali, Ludovic Utouh. Picha na Emmanuel Herman
Bagamoyo. Kamati za Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC), Serikali za Mitaa
(LAAC), Bajeti, pamoja na Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za
Serikali (CAG) zimependekeza kutungwa kwa sheria ya kufilisi mali za
watu watakaobainika kutafuna mali za umma.
Hayo yalielezwa jana na Naibu Spika, Job Ndugai wakati akizungumza na
waandishi wa habari baada ya kufunga mafunzo ya Kamati hizo
yaliyoandaliwa na ofisi ya CAG, kufafanua kuwa sheria zilizopo
haziwabani wanaotafuta fedha zinazotokana na kodi za wananchi, ni vyema
sasa kukawa na sheria ya kufilisi mali zao.
“Ni kweli sheria zetu zimekuwa haziwabani watu wa aina hii, wazo la
kufilisi wanaotafuna mali za umma ni moja kati ya maazimio 24 ya Kamati
hizi zilizopata mafunzo kwa siku tano” alisema Ndugai na kuongeza;
"Watu wamekuwa wakifungwa kwa muda na baadaye kuachiwa, hiyo ni
changamoto kubwa ambayo ipo kwa sasa, huo ni mjadala wa wote ambao
unahitaji jibu la pamoja.”
Alisema hata mfumo wa sasa wa jinsi Kamati za fedha zinavyoisimamia
serikali katika matumizi hauko sahihi, kutokana na ukaguzi wa hesabu za
serikali hufanyika baada ya fedha kutumika.
“Hii ina maana kwamba kamani madhara yatatokea fedha zinakuwa
zimeshaliwa na wakati huohuo huduma iliyopaswa kutolewa inaweza
isitolewe ama itolewe kwa kiwango cha chini” alisema
Alisema mfumo huo ni tofauti na ule wa Marekani ambapo bunge lake lina
nguvu ya kudhibiti matumizi ya fedha kabla hayajafanyika au kukagua
fedha katika mwaka huohuo, kusisitiza kuwa hiyo ni tofauti na Tanzania
ambapo fedha zinazokaguliwa zinakuwa za mwaka mmoja au miwili iliyopita.
“Wakati umefika sasa wa bunge kuwa na utaratibu kama wa Marekani ili
kuondoa ubadhilifu na kuleta usimamizi tija katika matumizi ya fedha za
umma” alisema Nduga