Waziri wa
Uchukuzi, Dk Harrison Mwakyembe akionesha picha ya kijana Leonard
Jeremiah Monyo aliyekamatwa na kete 86 za madawa ya kulevya katika
Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere
Na Makongoro Oging’ na Haruni Sanchawa
MTANDAO
hatari wa unga nchini Tanzania umeshanaswa, kwa sasa unafanyiwa kazi
kwa kasi na Kitengo cha Kudhibiti na Kupambana na Madawa ya Kulevya,
chini ya kamanda wake, Godfrey Nzowa.
Habari
njema kuhusu kunaswa kwa mtandao wa unga, zinakuja baada ya Waziri wa
Uchukuzi, Dk. Harrison Mwakyembe kufanya kazi nzuri na kuwataja watu
ambao inadaiwa walihusika katika kupitisha madawa ya kulevya Uwanja wa
Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNIA), Dar es Salaam.
Sekeseke
kuu ni kukamatwa kwa Watanzania wawili, Agnes Gerald ‘Masogange’ ambaye
ni mwanamitindo na Melisa Edward, nchini Afrika Kusini, wakiwa na
madawa ya kulevya aina ya Crystal Methamphetamine, yenye uzito wa kg
120, Julai 5, mwaka huu.
Swali
kwamba walipitaje JNIA lilijibiwa na Mwakyembe Jumamosi iliyopita,
akafafanua namna Mfumo wa Kamera za Usalama (CCTV), zilivyonasa ‘uhuni’
uliofanyika, hivyo akawataja watumishi wa Mamlaka ya Uwanja wa Ndege
(TAA), Yusuf Daniel Issa, Jackson Manyonyi, Juliana Thadei na Mohamed
Kalungwana kuhusika, akaagiza wafukuzwe kazi na polisi kuwakamata.Baada
ya Mwakyembe, moto unaendelea kuwaka na uchunguzi wa gazeti hili
umebaini kuwa mtandao ulionaswa na Kitengo cha Kudhibiti na Kupambana na
Madawa ya Kulevya, unagusa mikoa yote nchini.
Katika mtandao huo, siri kubwa iliyovuja
ni majina na jinsi biashara hiyo haramu inavyoendeshwa mkoa kwa mkoa,
wilayani mpaka mitaani, vilevile wanamichezo na wasanii mbalimbali ambao
imeshabainika kwamba wengi wao wanatumika kusafirisha unga.
Imebainika kwamba mtandao huo,
uligundulika baada ya watu 2,075 kukamatwa katika kipindi cha Januari
hadi Juni mwaka huu (baadhi yao, picha zao zinaonekana ukurasa wa
mbele).
“Watu tuliowakamata kimsingi ni wale
wanaotumwa tu. Sasa wale ndiyo wamewataja mabosi wao, wameeleza siri
kubwa,” alisema Kamanda Nzowa na kuongeza:
“Haikuwa kazi rahisi, tulitumia mbinu za
kiaskari kuwafanya waeleze ukweli. Wamesimulia biashara hiyo
inavyofanyika, jinsi watu wenye fedha wanavyowatumia vijana kusafirisha
mizigo.
“Tulichobakiza sasa ni kuwakamata
wahusika na kuusambaratisha mtandao wenyewe. Hata sasa tunachokifanya ni
kupambana na huo mtandao wenyewe, mwisho tutausambaratisha kabisa.”
NI MWAKA WA VITA NZITO
Nzowa, alisema kuwa mwaka huu umeonekana
kuwa na vita nzito kwa sababu kuna lindi kubwa la watu ambao
wamejiingiza katika biashara ya madawa ya kulevya licha ya wengi
kukamatwa na hata baadhi yao kunyongwa katika nchi za China na Pakistan.
Alisema madawa ya kulevya yenye uzito wa
kilo 16,824 (tani 16.8) yamekamatwa kati ya kipindi cha Januari na
Juni, mwaka huu, idadi ambayo ni kubwa kuliko vipindi vyote vilivyopita.
Alifafanua kwamba wingi huo usitafsiriwe
tu kwamba biashara ya madawa ya kulevya inatanuka nchini, isipokuwa
itazamwe kwa jicho la pili kwa upana wake jinsi mapambano dhidi ya
biashara hiyo yalivyochochewa makali.
“Udhibiti umekuwa mkubwa sana.
Isichukuliwe tu kwamba biashara inazidi kushika kasi, hapana, haya ni
matunda ya kazi ya udhibiti ambayo inafanyika. Pengine huko nyuma
walikuwa wanapishana kwa wingi zaidi lakini mapambano yalikuwa dhaifu,
kwa hiyo wafanyabiashara hiyo haramu walikuwa wanajitanua tu.
“Ni wajibu wa kila mtu kumwambia
mwenzake aachane na hii biashara, tunapomkamata na ushahidi, hapo
anakuwa amekwenda na maji,” alisema Nzowa.
Akichambua zaidi, Nzowa alisema takwimu
za madawa ya kulevya aina ya heroin zilizokamatwa katika kipindi hicho
ni kilo 30 na washitakiwa ni 45, kati yao wanawake ni wanne.
Alisema, cocaine walikamata kilo nne na
watuhumiwa ni 18 ambao ni wanaume watupu na dawa aina ya ephedrine
walikamata kilo 12 mshitakiwa ni mmoja mwanaume na bangi ilikamatwa kilo
9,999 na watuhumiwa ni 1,478, kati yao wanawake ni wawili.
Aliongeza kuwa licha ya kukamata bangi,
polisi waliweza kuharibu ekari 300 za mmea huo katika mikoa ya Arusha,
Tanga na Mara wilayani Tarime.
Kamanda Nzowa akaongeza kwamba polisi wanafanya kazi hiyo nzuri kwa kushirikiana na raia wema.
“Hivi sasa tuko makini sana kwa wasanii
na wanamichezo wanaotaka kusafiri kwenda nje ya nchi kwa sababu
tumegundua kuwa wanatumika kutokana na umaarufu wao,” alisema Nzowa.
Akifafanua zaidi, kamanda huyo alisema
wana taarifa kwamba hivi sasa kuna dawa za kulevya za majimaji, hivyo
wanaofikiria kusafirisha hizo kwa njia hiyo wanapaswa kujua kuwa
watagundulika.
“Hii ni vita ambayo kila anayelitakia mema taifa hili anapaswa kushiriki kupambana na dawa za kulevya,” alisema Kamanda Nzowa.
KWA NINI VIJANA WENGI WANAKIMBILIA UNGA?
Mtafiti maarufu na mwelimishaji wa
maisha ya vijana na jamii kwa jumla, James Mwang’amba, alisema kuwa
vijana wengi wanaingia katika wimbi la biashara ya madawa ya kulevya kwa
sababu ya kukata tamaa.
“Ukifuatilia maisha ya vijana kwa sasa,
utagundua kwamba wengi wao wamekata tamaa. Wanahisi hawana njia ya
kutoka kimaisha ndiyo maana wanaona fursa yoyote inayokuja mbele yao
inafaa hata kama ni hatari.
“Kila
mtu anatamani sana maisha ya juu, awe na kipato kikubwa, sasa kwa vile
haoni njia nzuri za kufikia ndoto zake, anaamua kujiingiza kwenye
usafirishaji wa madawa ya kulevya ili apate fedha za haraka ili naye awe
mtu fulani,” alisema Mwang’amba na kuongeza:
“Tatizo kubwa ni hii tofauti ya kipato.
Kuna tofauti kubwa sana kati ya wenye nacho na wasio nacho, hii ni
hatari sana. Sasa jamii kwa vijana ni hatari zaidi kwa sababu damu
inachemka na kuona kila kitu ni rahisi kufanya.
“Hakuna sababu nyingine kwa nini vijana
wengi wanakuwa wauza unga, ukweli ni tamaa ambayo inachochewa na hasira
ya kuwa na maisha duni wakati wanawaona wengine wakiwa matajiri
wakubwa.”