STAA wa filamu za Kibongo, Coletha Raymond ‘Koleta’ kwa mara nyingine tena amekumbwa na tuhuma za kukwepa kulipa deni la shilingi 400,000 analodaiwa na staa mwenzake, Husna Iddi ‘Sajenti’..
Kwa mujibu wa chanzo chetu, Koleta alikopa nguo kwenye duka la Sajenti kwa maelezo kwamba angelipa jioni ya siku hiyo lakini mpaka sasa ni miezi saba imepita bila msanii huyo kulipa deni hilo.
Ikazidi kudaiwa kuwa hata Sajenti anapompigia simu Koleta ili kumuulizia kuhusu deni hilo, msanii huyo hapokei simu, hali inayotoa tafsiri kwamba anataka kumdhulumu.
Mwandishi wetu alimtafuta Sajenti ili kupata uhakika kama kweli anamdai Koleta ambapo alifunguka kama ifuatavyo:
“Sijawahi kumuona mtu msumbufu kama Koleta na sasa naanza kuamini maneno ya watu kwamba ana asili ya utapeli,” alisema Sajenti.
Akaongeza kuwa anamdai Koleta tangu mwaka jana na imefikia hatua sasa hapokei simu yake.
“Kinachoniuma ni pale anaposhindwa kupokea simu yangu, nikitumia simu asiyoijua anapokea na akijua ni mimi ananipa ahadi za uongo,” alisema Sajenti.
Mwandishi wetu alimsaka Koleta na kumsomea tuhuma zake ambapo alikubali kudaiwa na Sajenti ila akakanusha kutopokea simu zake, akadai kwamba ameshaongea na msanii huyo ili alipe deni hilo kwa awamu.