Thursday, August 22, 2013

LIPUMBA AIPONDA SEREKALI YA CCM NA KUDAI IMESHINDWA KAZI

Mwenyekiti wa Chama cha Wananchi (CUF), Profesa Ibrahim Lipumba ametupa kombora kwa Serikali ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), akisema imeshindwa kutekeleza ahadi zake na badala yake inatumia vyombo vya dola kuwakandamiza na kuwaumiza wananchi.

Lipumba pia aliishutumu Serikali kwa kuwakumbatia viongozi ambao wanatuhuma za ubadhilifu kwa kuwahamisha katika vituo vyao vya kazi, hivyo kuendelea kuzorotesha uchumi wa nchi na kusababisha hali ya ugumu wa maisha kwa wananchi.

Aliyasema hayo jana wakati akifugua mkutano wa Baraza Kuu la chama hicho, Dar es Salaam, ambapo alisisitiza kuwa ubadhilifu ambao unakumbatiwa na Serikali hiyo umedhihirishwa pia na Kamati ya Bunge ya Hesabu za Serikali za Mtaa (LAAC)ambayo imebaini kuwapo mtandao unaohusisha viongozi wa Serikali wanaotafuna fedha za umma.

“Hii ni Serikali ya kisanii sana maana kila inachokisema haitekelezi kwa mfano kule Mtwara wananchi wanaendelea kuteswa .

Alisema Serikali imeshindwa kutekeleza ilani yake ikiwamo kuwapatia maisha bora wananchi.

Profesa Lipumba pia alieleza kusikitishwa kwake na nguvu kubwa iliyotumika katika kumkamata Kiongozi wa Jumuiya ya Taasisi ya Kiislam Sheikh Issa Ponda, akidai kuwa licha ya kwamba naye kuna wakati huwa haungi mkono kauli zake, lakini haoni kama ni sahihi kumhukumu kwa kumshambulia kwa risasi.

Alisema hatua yake ya kuzungumzia mara kwa mara suala la Sheikh Ponda haimaanishi kuwa anafanya hivyo kwa kuwa ni Mwislamu mwenzake, bali anafanya hivyo kwa kutambua ni wajibu wake kutetea haki kwa wananchi wote.

Alisema ni wajibu wake kukemea na kulaani vitendo kama hivyo akisema vilianza kwa Mwandishi wa Habari wa Channel Ten, Mwangosi, vikafuata kwa Ponda na kwamba kesho vinaweza kumkuta yeye.

Kuhusu mchakato wa maoni kwenye Katiba Mpya, Profesa Lipumba, alikosoa akisema kuwa baadhi ya vipengele havijafafanua bayana kuhusu muundo wa Serikali na namna inavyoweza kujiendesha.

Source:Mwananchi