Absalom Kibanda
MAHAKAMA ya Hakimu Mkazi Kisutu,
imemuona aliyekuwa Mhariri Mtendaji wa gazeti la Tanzania Daima, Absalom
Kibanda na wenzake wanaokabiliwa na kesi ya uchochezi, kuwa wana kesi
ya kujibu.
Hakimu Mkazi Waliarwande Lema, alitoa uamuzi huo jana baada ya upande wa mashitaka kufunga ushahidi wa mashahidi watatu.
Washitakiwa hao wanakabiliwa na
mashitaka ya kuandika na kuruhusu kuchapisha makala ya uchochezi,
inayodaiwa kuwahamasisha askari wa majeshi mbalimbali nchini, kutotii
amri ya wakuu wao.
Mbali na Kibanda washitakiwa wengine ni
mwandishi wa makala hiyo iliyochapishwa Novemba 30, mwaka juzi, Samson
Mwigamba na aliyekuwa Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya Mwananchi,
Theophil Makunga.
Baada ya upande wa mashitaka kufunga
ushahidi, wakili wa Upande wa Utetezi, Isaya Matambo, aliomba Mahakama
iwape Mwenendo wa Kesi ili waandae majumuisho ya hoja kuwa washitakiwa
hawana kesi ya kujibu, hata hivyo Hakimu Lema alikataa kutoa nafasi
hiyo.
Alisema baada ya kupitia ushahidi
uliowasilishwa mahakamani hapo, ameona washitakiwa wana kesi ya kujibu
na watatakiwa kuanza kujitetea Septemba 3 mwaka huu.
Aidha alisema atatoa hati ya kukamatwa
kwa Mwigamba, endapo hatawasilisha vilelezo kuthibitisha sababu za
kutofika mahakamani alizotoa kwamba anaumwa.
Alitoa onyo hilo baada ya mdhamini wa
Mwigamba, Rose Moshi kudai mshitakiwa hajafika mahakamani kwa kuwa
anaumwa na amelazwa katika Hospitali ya St Thomas Arusha.
Kibanda na Mwigamba wanadaiwa kuchapisha
makala hayo, Makunga anadaiwa akikaimu nafasi ya Mkurugenzi Mtendaji wa
Kampuni ya Mwananchi, aliruhusu kampuni yake kuchapisha gazeti la
Tanzania Daima, likiwa na makala hiyo inayodaiwa kuwa ya uchochezi.
Gazeti hilo lilikuwa na makala iliyokuwa
na kichwa cha habari “Waraka maalumu kwa askari wote, iliyoandikwa na
Mwandishi wa Safu ya Kalamu ya Mwigamba, Samson Mwigamba.