Kwa mara ya kwanza katika historia ya Liberia, wanafunzi wote wamefeli mtihani wao wa mwisho wasekondari na hivyo kumaanisha kuwa hakuna hata mmoja ambaye atafuzu kuingia chuo kikuu.
Waziri wa elimu wa Liberia amesema ameshinda kufahamu ni kwa nini hakuna wanafunzi hao wamefeli kiasi hicho.Zaidi ya wanafunzi elfu ishirini na watano walianguka mtihani huo ambao ungewapa fursa ya kujiunga na chuo kikuu cha Liberia ambacho ni moja ya vyuo vikuu vinavyoendesha na serikali.
Lakini wasimamizi wa chuo hicho wameiambia BBC kuwa wanafunzi hao hawakuwa makini na ufahamu mzuri wa lugha ya Kiingereza ambayo ilitumiwa kuwatahini.
Taifa la Liberia linaendelea kujinasua kutokana na athari za mapigano ya wenyewe kwa wenyewe yaliyomalizika zaidi ya miaka kumi iliyopita.
Rais wa Liberia, Ellen Johnson Sirleaf, ambaye pia ni mshindi wa tuzo ya amani ya Nobel, amekiri kuwa mfumo wa elimu nchini humo bado ungali duni na unahitaji marekebisho ya dharura.
Mwandishi wa BBC mjini Monrovia, anasema shule nyingi nchini humo havina vifaa vya kimsingi na waalimu waliohitimu.
Lakini hii ni mara ya kwanza katika historia ya taifa hilo kwa wanafunzi wote kufeli mtihani huo licha ya kulipa ada ya usajili ya dola ishirini na tano.
Chuo hicho kikuu ambacho kina idadi kubwa ya wanafunzi hakitakuwa na wanafunzi wa mwaka wa kwanza wakati muhula mpya utakapoanza mwezi ujao.
Lakini wanafunzi wengi wanasema hawajaamini matokeo ya mtihani huo na waziri wa Elimu Etmonia David-Tarpeh, ameiambia BBC kuwa anatarajia kukutana na wasimamizi wa chuo hicho ili kujadili suala hilo.