Wednesday, August 21, 2013

HATI ZA NYUMBA KUHAMIA MFUMO WA DIJITALI


KAMATI ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC), imeitaka Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, kurekebisha hati zote za nyumba nchini kutoka mfumo wa Analojia kwenda mfumo wa Dijitali.
Akizungumza jana jijini Dar es Salaam, Mwenyekiti wa Kamati hiyo Zitto Kabwe, alisema wameitaka Wizara hiyo kubadilisha hati hizo na kuziunganisha na namba ya mlipa kodi.

“Tumewarudisha tunataka waje na majibu ya maagizo tuliyowapa. Kuna viwanja 160 vilitolewa bila kujulikana vya nani, tumewaagiza Januari 2014 waje na majibu, hiyo itakuwa ni njia rahisi ya kuweza kukusanya kodi nchini,” alisema Zitto.

Zitto alisema serikali inahitaji kuwa na mapato mengi zaidi kuliko kutumia vyanzo vingine, ambapo itawezesha kila mwananchi kulipa kodi kwa wakati na kupata namba ya mlipa kodi.

Pia waliitaka Wizara hiyo kushughulikia migogoro ya Ardhi inayojitokeza mara kwa mara pamoja na kuweka wazi viwanja vilivyo wazi.