Sunday, August 4, 2013

CHANNEL TEN WASHANGAZWA NA POLISI KUANDAMA WAANDISHI..



SIKU moja baada ya Mpigapicha wa Kituo cha Televisheni cha Chennel Ten, Eliah Ruzika kudai kupigwa na polisi, uongozi wa Kituo hicho umeshangazwa waandishi wake kuandamwa na Jeshi la Polisi na kusema watatoa msimamo wao wa malalamiko kwa jeshi hilo kesho.
Aidha, Polisi wa Kituo cha Tazara wamekanusha kumpiga mwandishi huyo na kudai kuwa walifika kumuokoa mara baada ya kuzingirwa na wananchi wakidhani ni mwizi ndipo walipomfunga pingu lakini baada ya kubaini ni mwandishi wa habari walimfungua na kumtaka kuondoka.
Akizungumza jana na gazeti hili, Mhariri Mkuu wa kituo hicho, Dina Chahali alisema tukio hilo limewatisha na kuwasikitisha ikiwemo kuwakumbusha vitendo vilivyofanywa na Polisi kwa waandishi wao marehemu Daudi Mwangosi wa Mbeya pamoja na mwandishi wao Munir Zakaria wa Zanzibar.
“Baada ya tukio hili tumejiuliza tuna tatizo gani na polisi? Lakini tutakutana Jumatatu (kesho) na kutoa msimamo wa ofisi wa malalamiko rasmi kwa Jeshi la Polisi kwani mwandishi wetu aliitwa kufanya kazi kwa nini wamfunge pingu kama mwizi,” alihoji Chahali.
Alisema baada ya kipigo mwandishi wao aliumia mguu na kuzungushwa kupata hati ya Polisi ya utambulisho ya matibabu (PF3) ili akatibiwe kwani alienda Kisutu karibu na ofisini kwao alipokimbilia walimwambia hawatoi na kwenda Kituo kikuu cha Polisi ambapo alielezwa kwenda katika kituo palipotokea tukio.