Sunday, July 21, 2013

TAHADHARI: SAMAKI WALIOVULIWA KWA MABOMU NA SUMU WATAPAKAA KWENYE MASOKO JIJINI DAR ES SALAAM

Wakazi wa jiji la Dar es Salaam, wameambiwa wachukue tahadhari na umakini wakati wa kununua samaki nyakati za jioni, kutokana na madai kuwa baadhi ya wachuuzi huvua kwa kutumia mabomu.

Tahadhari hiyo imekuja baada ya NIPASHE Jumapili kufanya uchunguzi wa muda mrefu, ambapo imegundua samaki hao wanauzwa nyakati hizo kukwepa kugundulika.
Imefahamika licha ya Serikali kuwa na kampeni ya kusaka watu wanaojihusisha na uvuvi huo, bado hali imekuwa mbaya katika maeneo ya pwani ya bahari ya Hindi.
Maeneo yanayotajwa kukithiri kwa uvuvi wa mabomu ni Pwani ya Bagamoyo, Kawe katika Manispaa ya Kinondoni na Buyuni eneo la Kigamboni, Manispaa ya Temeke.



Baadhi ya wavuvi waliofanikiwa kuzungumza na gazeti hili kwa masharti ya kutotajwa majina yao kwa usalama, walisema watu wanaojihusisha na uvuvi haramu wanatumia mbinu nyingi za kuingiza samaki sokoni.
Walisema watu wengi kutokana na kuanza kuwabaini samaki wa aina hiyo, wavuvi wanawauza kwenye maeneo ya mikusanyiko ya watu nyakati za jioni bila ya kugundulika kwa urahisi.
MBINU CHAFU
Mmoja wa wavuvi hao, alisema njia nyingine iliyobuniwa ni kuwaweka kwenye majokofu ili kuwafanya wawe wagumu kama wanavyokuwa samaki waliovuliwa kihalali.
"Samaki wa mabomu anakuwa laini kutokana na kuvunjwavunjwa na mlipuko, pia macho yao yanaonekana mekundu kutokana na kuvilia damu", alisema na kuongeza "Samaki wadogo wanauzwa kwa wakaanga samaki pale pale ufukweni."
Alisema, samaki wakubwa wanahifadhiwa kwenye jokofu kwa muda wa siku moja ili kuwagandisha na barafu.
"Ugumu wa barafu inasababisha kutopindika kirahisi, ni vigumu kumgundua kama amevuliwa kwa bomu," aliongeza kusema.
SOKO LA FERI
Katibu Mkuu wa Soko la Kimataifa la samaki la Feri, Mbaraki Kilima, akizungumzia suala hilo, alisema kwamba wamefanikiwa kudhibiti samaki hao wasiingie kwenye mzunguko wa ndani ya soko hilo.
Hata hivyo, alikiri kuna kipindi wanaingizwa kinyemela, lakini wengi wao wanauzwa nje ya soko hasa maeneo ya kivuko cha Kigamboni.
"Ni kazi ngumu kuwakabili wahusika kwa sababu wana vitisho, kilichobaki tunakuwa makini samaki kuingia hapa kwetu pekee," anasema Kilima.
NI VIGUMU KUWAKAMATA
Baadhi ya wavuvi hao walisema ni vigumu kukamatwa kutokana na kuwa na mtandao mkubwa.
Walisema endapo kunatokea zoezi la kuwakamata, wanapata taarifa mapema, hivyo ni rahisi kwao kukimbia.
"Kuna watu wanashirikiana nao sehemu mbalimbali, viongozi hata polisi, hata sisi inatuwia vigumu kuwataja kwani tunaweza kuhatarisha maisha yetu,", alisema mmoja wao.
AFISA UVUVI TEMEKE AZUNGUMZA
Afisa Uvuvi wa Manispaa ya Temeke, Teddy Chuwa aliakiri kuwepo kwa hali hiyo, ambapo alitoa takwimu ya watu zaidi ya 50 wamekamatwa na kupelekwa Mahakamani.
Alisema wamekuwa na operesheni maalum za kuwakamata watu hao na kupelekea kupungua kwa matukio ya aina hayo kwa asilimia 70.
Chuwa alifafanua kwamba kuna madhara ya kula samaki waliovuliwa kwa mabomu japo hayajitokezi kwa haraka, hivyo alionya watu kutowanunua.
Afisa huyo, alisema katika mazingira ya bahari, mabomu hayo yanaharibu matumbawe ambayo ni mazalia ya samaki pamoja na kuharibu ikolojia ya viumbe wanaoishi majini.
TFDA WAZUNGUMZA
Afisa Uhusiano wa Mamlaka ya udhibiti wa Chakula na Dawa (TFDA) Gaudensia Simwanza, akizungumzia suala hilo alisema, kwamba bado hajapata taarifa kuingia kwa samaki hao sokoni.
"Sisi tunafanya kazi ya kuangalia samaki wanaoingia sokoni, lakini sijapata taarifa yoyote kama kuna wa aina hiyo, ngoja niwasiliane na idara ya chakula halafu nitatoa taarifa," alisema Simwanza.
Hata hivyo, alisema kuwa udhibiti wa samaki hao unafanywa na idara ya uvuvi kwa Halmashauri za jijini Dar es Salaam, endapo zoezi hilo likiendeshwa kwa umakini samaki hao siyo rahisi kuingia sokoni na kuuzwa kiholela.

CHANZO: NIPASHE