Friday, July 5, 2013

MWENYEKITI WA UVCCM ARUMERU ATUPWA JELA MIEZI 6 KWA KOSA LA UTAPELI....!!

MWENYEKITI wa Umoja wa Vijana wa CCM (UVCCM) Wilaya ya Arumeru (UVCCM) , Boniphace Laizer amehukumiwa kifungo cha miezi sita  baada ya kupatikana na hatia ya utapeli wa shamba.
Laizer alikuwa akishitakiwa na wengine wawili. Laizer alilipa faini hiyo pamoja na mwenzake. Lakini, mshitakiwa mwingine, alikwenda jela baada ya kushindwa kulipa faini hiyo. Hukumu hiyo ilitolewa jana na Hakimu Moka Mashaga katika Mahakama ya Mwanzo ya Maromboso jijini Arusha.
Akisoma huku hiyo, Hakimu alisema amefikia uamuzi huo baada ya kuridhishwa na ushahidi uliotolewa na upande wa mlalamikaji, Barnaba Kiria.
Alisema Laizer akiwa na wenzake wawili, Adam Mosha aliyekwenda jela baada ya kushindwa kulipa faini na Daniel aliyelipa faini, mwaka juzi katika eneo la Ngaramtoni kwa Iddi, walimuuzia mlalamikaji shamba lenye ukubwa wa meta 15 kwa 18 kwa thamani ya Sh 5,000,000 huku akijua si mali yao.
Alisema baada ya makubaliano hayo, mlalamikaji alilipa Sh 4,760,000 kama malipo ya awali ya ununuzi wa kiwanja hicho na zikabakia Sh 240,000.
Alisema wakati mlalamikaji akisubiri kukamilisha malipo hayo, alipokea ujumbe mfupi wa maneno kutoka kwa Laizer, akimweleza eneo hilo alishaliuza kwa mtu mwingine aitwaye Alex na kwamba angemrejeshea fedha zake.
Alisema kutokana na ujumbe huo, alianza kumdai fedha zake, hali iliyozua malumbano ya muda mrefu.

SOURCE: HABARI LEO