Wednesday, July 24, 2013

ASKARI WA FFU ALIYEFARIKI KWA AJALI YA GARI WAKATI AKIELEKEA KUTOA KICHAPO KUZIKWA KIGOMA..!!

Mwili wa askari wa Kikosi cha Kutuliza Ghasia (FFU), Fidelis Malyatabu, aliyepoteza maisha juzi asubuhi katika Kijiji cha Kilingi, Wilaya ya Siha mkoani Kilimanjaro, wakati yeye na wenzake 11 wakienda kuzima vurugu za wananchi waliokuwa wakiandamana kupinga wenzao kushikiliwa na Polisi, utazikwa Kasulu mkoani Kigoma.
 
 Ajali hiyo ilitokea Julai 22 mwaka huu, majira ya saa 6.45 mchana nje kidogo ya mji wa Sanya Juu, ilisababisha pia askari tisa wa FFU kujeruhiwa vibaya, akiwamo Mkuu wa Kikosi hicho, ASP Maira Noni ambaye hata hivyo, ameondolewa katika Hospitali ya Rufaa ya KCMC na kupelekwa Hospitali ya Misheni ya Seliani mkoani Arusha kwa ajili ya uchunguzi kwenye eneo la kichwa chake.

Askari huyo mwenye namba G 8656 aliagwa jana katika eneo la Polisi na kusafirishwa kwenda Wilaya ya Kasulu mkoani Kigoma kwa ajili ya maziko yanayotarajiwa kufanyika leo.

Kifo cha askari huyo kilisababishwa na dereva wa gari aina ya Toyota Land Cruiser, kushindwa kumudu kona na kisha kuacha njia na kupinduka.

Kamanda wa Polisi mkoani hapa, Robert Boaz,  inasema kuwa, kikosi hicho kilikuwa kikielekea katika Kijiji cha Karansi, Wilaya ya Siha kwa ajili ya kwenda kukabiliana na wananchi waliokuwa wakiandamana kupinga kushikiliwa kwa wenzao watano kwa saa kadhaa katika kituo kikuu cha Polisi Wilayani hapa.

Wananchi hao wanadaiwa kuwashawishi wakazi wenzao wa eneo hilo kuvamia shamba lenye ukubwa wa hekta 8.9 mali ya Shirika la Roho Mtakatifu ambalo linamiliki Shule ya Sekondari ya Kilasara ambayo ndiyo inayodaiwa kuibua mgogoro huo.

Hata hivyo, wananchi watano ambao walikuwa wanashikiliwa bado hawajaachiwa na kwamba kwa sasa hali ni shwari kijijini hapa.