KATIKA Gazeti la Amani Toleo Namba 829 la Septemba
11-17, 2014, kulichapishwa habari ukurasa wa mbele iliyosomeka: “DIVA:
ZITTO NI MUME WANGU.” Ikikolezwa na dondoo ‘Adai ni mke anayetambulika
kisheria’ na ‘Asema hayuko tayari kuachana naye kirahisi,’ ambayo
uongozi wa gazeti umekusudia kwa nia njema kutoa ukweli juu ya habari
hiyo.
Ufafanuzi huu unalenga kumaliza mkanganyiko uliojitokeza hasa baada
ya kuwepo kwa madai kutoka kwa mhusika ambaye ni Loveness Malinzi (Diva)
kuwa, hakuzungumza na gazeti kile kilichoandikwa na kwamba alikuwa
anazushiwa; madai haya aliyawasilisha chumba cha habari kwa njia ya simu
na sehemu kuyaweka kwenye ukurasa wake wa kijamii wa Instagram.
Kama hilo halitoshi, Diva alikana kuzungumza na mwandishi wa habari
hiyo ambapo alisema mazungumzo yao yalihusu mwaliko wa Kipindi cha
Global TV Online ambacho kinarushwa na mtandao unaoendeshwa na Kampuni
ya Global Publishers inayomiliki pia Gazeti la Amani na si vinginevyo.
Malalamiko haya ya Diva yalikuja muda mchache baada ya gazeti kutoka
likiwa na habari hiyo ambapo jopo la wahariri wa Amani kabla ya
kuchapisha habari hiyo walijiaminisha kuwa ni ya kweli kutokana na
taarifa pamoja na vielelezo vya rekodi ya sauti ya mazungumzo
alivyoviwasilisha mwandishi kwenye dawati kuthibitisha kuwa alifanya
mazungumzo na mhusika kuhusiana na msingi wa habari nzima iliyoandikwa.
Kama tulivyoeleza, baada ya habari hiyo kutoka na kipande cha sauti
kuingizwa kwenye Tovuti ya Global Publishers, ndipo yalipoibuka madai
hayo huku baadhi ya wasomaji wakieleza kuwa ile siyo sauti ya Diva; hapo
ndipo uongozi wa gazeti ulipoamua kufuatilia ukweli na kubaini
yafuatayo.
Pamoja na ukweli kuwa Mheshimiwa Zitto Kabwe (Mbunge wa Kigoma
Kaskazini) na Diva wana ukaribu, mazungumzo kati ya mwandishi na
mwanadada huyo kuhusiana na kauli yake ya: “Zitto ni Mume Wangu,”
hayakufanyika na kwamba mwandishi alipika habari na kutengeneza sauti ya
Diva kwa lengo la kuwahadaa wahariri kwa nia mbaya!
Kwa msingi huo sisi kama chombo cha habari makini, kinachosimamia
weledi, kulinda na kuheshimu haki za binadamu; tunachukuwa nafasi hii
kumuomba radhi Diva, Mheshimiwa Zitto, sanjari na jamii kwa ujumla kwa
usumbufu wowote uliosababishwa na habari hiyo.
Aidha, uongozi unapenda kuutangazia umma kuwa, hatua kali za
kinidhamu zimeshachukuliwa dhidi ya mwandishi husika sambamba na onyo
kwa viongozi wote wa gazeti kwa udhaifu uliojitokeza katika habari hiyo.
Tunaomba jamii ielewe kwamba Global Publishers siku zote inasimamia
UKWELI na kamwe hairuhusu kabisa habari za uongo kuandikwa katika
magazeti yake.
Jamii iendelee kutuamini na kushirikiana nasi katika kusimamia weledi
wa uandishi wa habari. Milango ya kukosolewa iko wazi, hivyo kwa mwenye
malalamiko yoyote juu ya habari zetu, iwe ni uongo au kutotendewa haki,
asisite kuwasiliana na viongozi kwa hatua zaidi. Ndimi, Mhariri
Kiongozi, Magazeti Pendwa
credit:GPL