Wakuu wa shule za serikali zilizofanya vibaya kwenye matokeo ya mtihani wa kidato cha sita mwaka huu pamoja na Maofisa elimu wa Mikoa wamepewa muda wa mwezi mmoja ili kubaini chanzo cha shule zao kuwa na ufaulu hafifu.
Baada ya kubaini chanzo hicho cha ufaulu hafifu wanatakiwa kutoa taarifa kwa katibu mkuu Tawala za mikoa na serikali za mitaa-TAMISEMI.
Miongoni mwa shule ambazo wakuu wake wametakiwa kujieleza ni pamoja na shule ya Tambaza iliyopo jijini Dar es salaam na shule ya Iyunga ya Mkoani Mbeya, ambapo muda huo wa mwezi mmoja umeanza leo.
Akizungumza na waandishi wa habari leo jijini Dar es salaam, katibu Mkuu Tamisemi Jumanne Sagini amesema, kushuka kwa ufaulu kwa shule hizo kumewashtua watu wengi, kwani shule hizo zimejengewa uwezo mzuri wa vifaa pamoja na miundombinu.
Hata hivyo Sagini amesema, idadi ya wanafunzi 22,685 waliofaulu masomo ya sayansi kwa mwaka huu wa 2014 ni kubwa kwa zaidi ya wanafunzi 3,939 ikilinganishwa na wanafunzi 18,746 waliofaulu masomo hayo mwaka jana.
Amesema kuwa ufaulu huo umeipa changamoto Serikali na imekuwa ikifanya kila jitihada kuhakikisha kuwa kila mwanafunzi ambae amefaulu na kupata alama stahiki katika masomo aliyoyachagua anapata shule.
Aidha amewataka wazazi wa wanafunzi waliokuwa wamepangiwa kusoma masomo ya sanaa ilihali ufaulu wao ni katika masomo ya sayansi, kutokuwa na wasiwasi kwani serikali imebaini changamoto hiyo na kuifanyia kazi