Sunday, July 13, 2014

Jenerali Mwamunyange awahakikishia usalama wananchi wa mpakani




Mkuu wa Majeshi nchini,  Jenerali Davis Mwamunyange, amewataka wananchi waishio pembezoni mwa ziwa Nyasa kuondoa wasiwasi kutokana na mgogoro wa mpaka kati ya Malawi na Tanzania.

Kauli hiyo aliitoa wakati akizungumza na wananchi wa kijiji cha Liuli wilayani Nyasa wakati wa ziara ya kutembelea vikosi na viteule vya jeshi mkoani Ruvuma.

Mwamunyange aliwataka wananchi hao kuendelea na shughuli za ujenzi wa taifa bila kuwa na hofu ya machafuko yoyote yale wanayohofiwa kutokea.

Alisema hizo ni changamoto za muda mrefu lakini serikali inafanya juhudi ya kuzitatua kwa njia ya amani.

Aliwashukuru wananchi wa kijiji cha Liuli kwa kutoa ushirikiano kwa kuwapokea askari wa JWTZ  kijijini hapo kwa ulinzi wa taifa na kwamba kuwapo kwao si chanzo cha ugomvi bali ni sehemu ya jeshi kulinda nchi na mipaka yake.

Naye Mkuu wa wilaya ya Nyasa, Ernest Kahindi, alilishukuru jeshi hilo kwa ushirikiano wao na wananchi wa wilaya hiyo kwa kupokea taarifa na kuzifanyia kazi hasa kauli za viongozi wa Malawi.

Katika hatua nyingine Mwamunyange aliwataka askari hao kuishi vizuri na wananchi huku akiwapa mfano wa majeshi ya Tanzania yaliyopo katika ulinzi wa amani nchini Lebanoni, Darfur na Kongo.

Alisema silaha pekee ya jeshi hilo ni ushirikiano mzuri na raia kwa sababu jeshi haliwezi kupata taarifa na kufanya kazi ipasavyo bila kuwa na ushirikiano mzuri na wananchi ambao ndio walipa kodi inayowafanya askari kuishi na kutekeleza majukumu yao ya kiulinzi.