Saturday, February 22, 2014

AIBU:MJAMZITO AMFUMANIA MUMEWE ASUBUHI MAENEO YA TANDIKA ....

NI kweli ukistaajabu ya Musa utayaona ya Firauni! Fumanizi la aina yake lilitokea juzikati asubuhi ya saa 2, Mtaa wa Mbwela, Tandika jijini Dar ambapo mjamzito aliyejulikana kwa jina la Semeni  alipata ‘kichaa’ cha muda baada ya kumfumania mumewe, Dullah akiwa na mwanamke  mwingine chumbani kwao, Risasi Jumamosi lina kisa kizima.
Akisimulia mkasa huo, Semeni mwenye ujauzito wa miezi 6 alisema kabla ya tukio aligombana na mumewe akarudi kwao kwa muda wa siku mbili lakini walikuwa wakiwasiliana mpaka asubuhi ya tukio ambapo alimpigia simu kumwambia anafuata nguo kwa vile anakwenda kliniki.
“Nilipokuwa njiani nilimpigia simu mume wangu, nikamwambia nimekaribia, lakini akasema yeye amekwenda Posta.
“Pamoja na majibu hayo, niliamua kwenda. Nilipofika nilikuta mlango umefungwa kwa ndani, nikampigia simu mume wangu, akasisitiza hakuna mtu, yeye yupo Posta.

“Nilichungulia na kuona funguo, nikajua kuna mtu ila hataki kunifungulia, hapo wasiwasi ukazidi kwamba huenda kuna jambo linaloendelea,” alisema Semeni.
Mwanamke huyo aliendelea kuanika kwamba kufuatia hali hiyo aliwaita majirani ambao ilibidi wamtishe mtu aliye ndani kwamba asipofungua watavunja mlango, ndipo mlango ukafunguliwa na kumkuta Dullah akiwa na mwanamke mwingine chumbani, lakini mumewe huyo alichoropoka na kukimbia.
“Nilishtuka, nikapiga kelele ya mshangao kutokana na kitendo alichokifanya mume wangu, kumleta hawara mpaka kwenye chumba tunacholala!
“Sijaamini kilichotokea! Yule ni mume wangu, amewezaje kumleta mwanamke ndani ya chumba tunacholala tena kuna wapangaji wenzangu wameshuhudia,” alisema mwanamke huyo huku akilia machozi.
Akaendelea: “Mimi hapa nyumbani siachiwi hela ya kula, kila siku nakula nyumbani kwetu,  nikijua labda mume wangu hana, kumbe anamalizia kwa hawara! Jamani inaniuma sana, kama hivyo bora amuoe basi tuje tuishi wote au aniache akae yeye.”
Akizungumza na gazeti hili kwa uso ‘uliochunwa’, mwanamke aliyedaiwa kufumaniwa, Mwanaidi huku akiwa ‘ametaitiwa’ ndani, alijitetea kuwa hakufahamu kama Dulla ana mke.
“Mimi aliniambia hana mke wala mtoto na ndiyo maana nilikubali kuanzisha uhusiano wa kimapenzi na yeye si vinginevyo, kama ningejua nisingekubali kuja, kwa hiyo siyo kosa langu,” alisema Mwanaidi.
Baada ya hali kutulia, baba mzazi wa Dullah ambaye anaishi jirani aliitwa kuamua ugomvi huo na kuamuru wote waende nyumbani kwake ambapo  aliagizia gari.
Wawili hao walipofika nyumbani kwa mzazi huyo walimshusha Semeni na kumtaka atangulie ndani, alipoingia tu, nyuma dereva alitakiwa kuondoka gari hilo kwa kasi  huku Mwanaidi akiwemo ndani ili kumnusuru.
Baada ya kubaini ‘triki’ hiyo, Semeni alijirusha chini kwa hasira na kujigalagaza kisha kulikimbiza gari hilo bila mafanikio.