Sunday, November 10, 2013

Ziara ya Rais Geita: Afisa Usalama bandia anaswa akimsogelea Kikwete




GEITA: Katika hali ambayo inazidisha mashaka juu ya Usalama wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Jakaya Kikwete, Mtu mmoja ambaye hajatambulika nia yake, amefanikiwa kujipenyeza katika msafara wa Rais na kujifanya miongoni mwa walinzi wa msafara. 
Mtu huyo ambaye baada ya kunaswa amekutwa na vitambulisho bandia, alifanikiwa kujipenyeza katika mkutano wa kwanza wa ziara ya Rais wilayani Bukombe mkoani Geita, ambapo kulikuwa na sherehe za uzinduzi wa barabara ya Lami ya Bwanga hadi Uyovu Lunzewe yenye urefu wa km 45 ambayo ujenzi wake ulizinduliwa na Rais Jakaya Kikwete siku hiyo Novemba 9 mwaka huu.
Akiwa kama afisa usalama alikuwa akizuia baadhi ya watu kufika maeneo maalum yaliyoandaliwa mahususi kwa ulinzi, lakini pia alikuwa akipitapita kukagua baadhi wa watu wakiwamo na waandishi wa habari huku akiwapanga namna ya kukaa vyema kabla msafara wa Rais kuwasili eneo la tukio.
Katika mkutano huo wa kwanza alifanikiwa kupita salama kwani baada ya mkutano huo kumalizika, aliweza kupata usafiri na kuondoka na msafara umbali wa km 53 na kufika Ikulu ndogo ya Bukombe, ambako msafara uliitulia kwa muda na wageni kupata chakula, kisha kuelekea katika mkutano wa pili wa hadhara  mjini Ushirombo.
Hata hivyo, huko hakuweza kufanikiwa, Jeshi la Polisi mkoani Geita kwa shirikiana na Maofisa Usalama wa Taifa, lilifanikiwa kumtia mbaroni mtu huyo kama inavyoonyesha (Pichani Juu) akiwa ameshikwa chini na Ulinzi wa Askari polisi na afisa usalama akitolewa katika ya mkutano wa Rais Kikwete uliofanyika katika Uwanja wa Kituo cha mabasi Ushirombo.
Mtu huyo ametambulika kwa jina la Kwamani Juma anakadiriwa kuwa na umri kati ya 43-46, alikamatwa Novemba 9 mwaka huu, eneo la Ushirombo katika mkutano wa hadhara akiwa amejipanga kama maaofisa Usalama karibu na jukwaa kuu alilokuwa amekaa Rais Jakaya Kilwete.
Kamanda wa Polisi mkoa wa Geita Leonard Paul amethibitisha kukamatwa kwa afisa huyo bandia, alisema "Ndiyo… amekamatwa, si umeona kwenye mkutano kilichotokea, sasa unataka nieleze nini zaidi," alielza Kamanda Paul.
Kukamatwa kwake kulifanya wanaomjua kuanza kueleza wasifu wake na mmoja wapo akiwa ni Afisa Utamaduni wa Wilaya ya Bukombe, Julius Kambarage ambaye kutokana na kumfahamu mtu huyo alistajaabu kumuona akiwa amejipenyeza jukwaani hali ambayo ilimfanya kutoa taarifa kwa wahusika.
"Mimi nilikuwa MC, pale kwenye uzinduzi wa Barabara (Lunzewe) nilipomuona niliwaeleza watu wa usalama, sikujua walifanyiaje kazi, lakini nlistajaabu amefika tena Ushirombo,  ila safari hii nilimuona wakati akikamatwa, naona atakuwa Tapeli huyu" alieleza Afisa utamaduni huyo.
Mtu huyo mpaka akikamatwa alionekana akiwa mtanashati,  aliyevalia Kaunda Suti, miwani na kuonekana nadhifu, ina anadaiwa katika ukaguzi kitambulisho alichokutwa nacho kilikuwa kimeandikwa jina lake na huku kikuonyesha kuwa na Muhuri unaosomeka ‘Ulinzi na Usalama wa Taifa’.
Naye Diwani wa Kata ya Uyovu Yusufu Fungameza (Chadema), alieleza kumtambua mtu huyo na kudai ni mkazi wa Kata yake lakini amekuwa akitajwa na kulalamikiwa kuhusika na matukio ya utapeli kwa wananchi.
"Huyu bwana namfahamu sana, ni mkazi Kata yangu lakini amekuwa akinihusisha na vote do vya utapeli, yapo matukio kadhaa ya kulalamikiwa kutapeli watu pale Uyovu amewahi kumtapeli mfanyabiashara mmoja," alieleza.