Mwanafunzi wa kidato cha nne katika Shule ya Sekondari Mbande iliyopo Mbagala, Dar, Doricy Tryphone (18) amefariki dunia ghafla akiwa katika mtihani wake wa Hisabati wa kumaliza kidato cha nne, mwaka huu.
Tukio hilo la kuhuzunisha lilitokea Novemba 5, mwaka huu, Mbagala jijini Dar, wakati Doricy akifanya mtihani na wanafunzi wenzake.Ilisemekana kuwa akiwa katikati ya mtihani huku ‘akisovu’ namba, ghafla binti huyo mzuri na mwenye mvuto alizidiwa na kuishiwa nguvu, jambo lililowalazimu walimu na wasimamizi wamkimbize katika zahanati iliyopo jirani na shule hiyo.
Habari zilieleza kuwa baadaye hali ilizidi kuwa mbaya, ikabidi ahamishiwe kwenye Hospitali ya Temeke ili kuokoa uhai wake.
Akizungumza kwa masikitiko makubwa huku akitokwa machozi, dada wa marehemu Doricy, Esther Tryphone alisema kuwa alipofikishwa hospitalini hapo, mdogo wake alikuwa ameshafariki dunia, huku vipimo vikionesha kuwa alikufa kwa kuzidiwa na sukari mwilini.
Dada huyo alieleza kuwa, Doricy alikuwa akisumbuliwa na ugonjwa wa kisukari kwa muda mrefu tangu akiwa darasa la sita, lakini baadaye alipata nafuu kabla ya ugonjwa huo kurejea ghafla siku hiyo na kuuchukua uhai wake.
Baada ya kutokea kwa msiba huo, mwili wa marehemu Doricy ulizikwa Novemba 7, mwaka huu, katika Makaburi ya Chang’ombe jijini Dar huku wanafunzi wenzake wakijitokeza kwa wingi kumsindikiza mwenzao katika safari yake ya mwisho